Naunga mkono kuwa mazingira yetu ya biashara ni mabaya sana, yamezingirwa na ubabaishaji na rushwa. Lakini sikubaliani kabisa na maelezo yako kuwa ni waislam tu ndiyo wanaokwamishwa na wakristu katika shughuli zao za biashara, ukweli ni kuwa sisi sote tunakwamishwa sana na watendaji wa namna hii, uwe muislam, uwe mkristo, huna dini, sisi sote tunaumizwa na hilo. Na hata katika ofisi hizo hakuna cha mfanyakazi mkristo au musilam ambaye hapokei rushwa kwa sababu ya dini yake, kama anafanya hivyo ni kutokana na uadilifu wake binafsi. Wapo wakristo wanaopokea rushwa, wapo waislam wanaopokea rushwa, wapo wasio na dini ambao wanapokea rushwa, halikadhalika wale wasiopokea rushwa nao wamegawanyika hivyo hivyo. Iwe kwenye ujambazi ni hivyo hivyo - kuna waislam wengi tu ambao ni majambazi, na pia wapo wakristo wengi pia majambazi. Kama waislam wangekuwa wasafi kama unavyotaka tuamini basi hata miradi ya taasisi za kiislam ingekuwa inastawi lakini mingi inakufa kutokana na uendeshaji mbaya, wizi na ubinafsi. Tunachomhitaji JK ni kwamba aondoe watendaji wabaya katika serikali yake, wazembe, wevi, mafisadi na wasio na uwezo - bila ya kuangalia makabila yao au dini zao. Na ufahamu kuwa Watanzania wengi tulimchagua JK 2005 kuleta mabadiliko kutoka kwenye mfumo ambao tulikuwa tumeuchoka. Naye akaja ikaonekana anafurahia yaliyopo - Jk angeona Watanzania jinsi tunavyomwuunga mkono kama angewapeleka akina Lowasa, Mramba, Rostam Aziz, Karamagi, n.k. gerezani, ndiyo angejua kuwa sisi hatupo kwaajili ya ukristo au uislam bali tupo kwaajili ya ustawi wa Taifa. Wakristo wengi hatuna shida kama Taifa hili likiongozwa na marais waislam hata kwa miaka 50 mfululizo alimradi awe ni Rais ambaye anasimama pamoja na wanyonge dhidi ya waovu. Hata kama Rais atatoka Parokia au usharika wangu, kama anashirikiana na wezi, mafisadi, na watu wazembe, asahau kuwa naweza kumwunga mkono katika maovu yake maana katika uovu wake ni mateso kwa watu wote.