Martina Chambiri Mwimbaji wa Tanzania ee nchi, yangu ee!

Ngongo

JF-Expert Member
Sep 20, 2008
18,921
31,161
“TANZANI ee, nchi yangu ee, yapendeza ee, karibu muione, sura yake yavutiaa, kila konaa, kwa maziwa na bahari, nchi kavu na mipakaa…”

Hii ni sehemu ya wimbo maarufu sana ambao ulipendwa na watu wengi hasa watoto, vijana na hata watu wazima ndani na nje ya nchi katika miaka 1994 na 1995.

Nyakati hizo vituo mbalimbali vya televisheni na redio vilikuwa vikiupiga wimbo huo na vipo ambavyo vilikuwa vikiutumia wimbo huo kuwavutia watoto ambao walikuwa wakialikwa kushiriki katika vipindi vyao vya redio na televisheni ambavyo moja kwa moja vilikuwa vikishirikisha watoto.

Sababu kubwa ambazo zilichangia watu kuupenda wimbo huo ni mbili. Mojawapo ni kwamba wimbo huo unasifia Tanzania kwa uhalisia wake, rasilimali zilizopo nchini ambazo pindi wageni wanapotembelea wanavutiwa kuziona, pamoja na uzuri wa Taifa la Tanzania ambalo limejaaliwa duniani kuwa na vivutio vya kila aina zikiwemo mbuga za wanyama, ardhi zenye rutuba, maliasili kama madini ya thamani na kadhalika.

Sababu nyingine ya pili ambayo iliwafanya watu kuupenda sana wimbo huo, ni ukweli kuwa uliimbwa na mtoto mdogo wa miaka minne kutoka barani Afrika tena nchini Tanzania ambapo pia alilenga kuisifia nchi yake.

Hapa namzungumzia Martina Chambiri ambaye miongoni mwa Watanzania wengi jina hili siyo geni, Martina aliimba wimbo huo katika tamasha maalumu la watoto liliofahamika kama Zecchino d'Oro ambalo lilifanyika nchini Italia katika mji wa Bolognia mwaka 1995. Zecchino d'Oro ni tamasha la kimataifa la nyimbo za watoto ambalo limekuwa likifanyika kila mara nchini Italia tangu mwaka 1959.

Katika tamasha la 1995, watoto wengi wa umri wa Martina kutoka nchi mbalimbali duniani walihudhuria na wimbo huo wa Tanzania ee ambao yeye aliuimba, uliingia tano bora na kushika nafasi ya tatu.

Mwanzoni kabla ya kufanya naye mahojiano haya, nilikuwa najua kuwa msichana huyo anafahamu sana kuimba lakini jambo lingine ambalo nililigundua wakati wa mahojiano ni kwamba pia amejaaliwa kuwa na kipaji cha kujieleza kwa ufasaha na upeo wa kufahamu mambo mengi.

Martina alizaliwa Januari 1990 katika Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam. Wakati akiwa na umri wa miaka minne alianza chekechea katika Shule ya masista ya Clara Nursery School, iliyoko Kawe ambako ndiko nyumbani kwao.

‘’Nakumbuka tulikuwa shuleni sista akasema kuna mashindano ya kuimba, tukashindanishwa wote na mimi pale shuleni nikawa mshindi na hivyo nikapata nafasi ya kushiriki katika tamasha hilo,” anasema.

Anakumbuka wimbo huo ulitungwa na mwalimu wa muziki katika shule hiyo anayemtaja kwa jina la Mwalimu Julius Kapinga, na yeye ndiye aliyefanikiwa kuuimba kwa ufasaha. Aliimba wimbo huo kwa lugha mbili yaani Kiitaliano na Kiswahili, ambapo sehemu ya Kiitaliano ilitungwa na waandaaji wa shindano hilo wakiongozwa na mama mmoja anayemkumbuka kwa jina moja la Mariella ambaye kwa sasa ni marehemu.

Kabla ya kufanyika kwa tamasha hilo, alikwenda Italia kujifunza ambapo alichanganyika na washiriki wenzake ambapo walitakiwa kuimba kwa kupokezana.

Yeye (Martina) alikuwa akiimba ubeti (verse) na wenzake waliimba kiitikio (Chorus). Wakati akiwa nchini huko katika ziara hiyo ya mafunzo, alifundishwa jinsi ya kulitawala jukwaa wakati akiimba pamoja na kuzoea kuimba kwenye umati.

Baada ya ziara hiyo ya mafunzo, Martina alirudi nchini na alitakiwa tena kurudi Italia mwaka huo huo kwa ajili ya tamasha lenyewe ambapo Tanzania ilishika nafasi ya tatu huku nafasi ya pili ikichukuliwa na Pedro kutoka nchini Costa Rica.

Mshindi wa kwanza anamkumbuka kwa jina moja la Eugenia kutoka Urusi. Baada ya ushindi huo alirudi nyumbani kuendelea na masomo yake na alitumiwa tena mwaliko kurudi Italia kwa ajili ya kutumbuiza katika tamasha la wanawake la Women’s Festival ambapo alifanikiwa kukonga nyoyo za watu wengi.

“Baada ya kumalizika kwa matamasha hayo nchini Italia, niliporudi hapa nyumbani bado nilikuwa na shauku kubwa ya kuimba na kuendeleza kipaji changu kwa sababu ninaweza kuimba na ninapenda sana,” anasema.

Baada ya kurudi nyumbani, alikutanishwa na baba mmoja anayemkumbuka kwa jina moja la Gideon ambaye alimtungia nyimbo sita zote zikihusu mazingira na zikarekodiwa na kutengeneza album moja.

“Sababu kubwa ya kutungwa kwa nyimbo hizo zilizokuwa na mada zinazohusu mazingira ilikuwa kuihamasisha jamii kuhusu umuhimu wa kuhifadhi na kutunza mazingira kwa faida ya vizazi na vizazi,” anasema.

Baada ya kuimba nyimbo hizo za mazingira, sauti ya Martina ilipotea katika anga za muziki mpaka mashabiki wake wakawa wanajiuliza kulikoni, maana wengi walikuwa na shauku ya kufahamu hatima yake katika tasnia hiyo ya muziki na hasa kutokana na uwezo mkubwa aliouonesha katika matamasha yaliyofanyika nje ya nchi.

Lakini hali hiyo ilitokana na umri aliokuwa amefikia na majukumu ya shule yaliyokuwa yakichukua muda wake mwingi. Ni wakati huo ambapo alianza shule ya St. Constantine iliyoko Arusha na kujikuta akirushwa kutoka darasa la kwanza hadi darasa la tatu.

Anasema ilibidi mawazo yake mengi yahamie shuleni zaidi kuliko katika uimbaji. Baada ya hapo wazazi wake wakaamua kumhamisha shule hiyo na kumuandikisha shule ya St. Mary’s Tabata ambako alisoma na kuhamia St. Mary’s iliyopo eneo la Mbezi Beach ambako alimalizia darasa la saba katika shule hiyo hiyo.

Anasema pamoja na kufaulu vizuri kujiunga na shule za serikali, wazazi wake waliamua afanye usaili katika shule za Marian, Kifungilo na St. Francis.

Alifanikiwa kupata nafasi katika shule ya Marian na kuanza kidato cha kwanza mpaka alipomaliza kidato cha nne mwaka 2007. “Nilipenda sana masomo ya biashara, nilipomaliza kidato cha nne nikafaulu kwa kupata daraja la kwanza pointi 14.

Katika masomo ya Hesabu, Commerce na Book-keeping nilifaulu vizuri na kwa kuwa niliyapenda, nikaamua kusomea masomo hayo kidato cha tano,” anasema.

Binti huyo anasema anafurahia kuwa wazazi wake hawakumlazimisha kusomea masomo ambayo hataki isipokuwa hawakusita kumpa ushauri kwa kile ambacho yeye alikuwa anachagua kukifanya.

“Baba yangu alikuwa akipenda sana niimbe na nishiriki kwenye michezo, na mimi napenda sana michezo na hasa kuogelea, ila mama alikuwa akiuliza ni kwa nini nisisome masomo ya sayansi, ila masomo ambayo nilichagua walikubaliana na mimi kisha wakaniambia niyasome kwa bidii ili nifaulu vizuri,” anafafanua.

Alipomaliza kidato cha nne akafanya usaili Shule ya Sekondari Loyola na kufanikiwa kupata nafasi ya kujiunga na kidato cha tano ambapo mwezi uliopita alifanya sherehe na wenzake ya kumaliza kidato cha sita.

Mhitimu huyo wa kidato cha sita anasema kuna tofauti kubwa kati ya shule ya bweni na kutwa kama alivyojionea Shule ya Sekondari Marian na Shule ya Sekondari Loyola kwa kuwa Marian ilikuwa ya wasichana watupu na Loyola ilikuwa mchanganyiko, lakini jambo la msingi lilikuwa ni kuhakikisha anasoma kwa bidii.

Martina anasema jambo muhimu ambalo anamshukuru Mungu ni kumpatia wazazi ambao walishirikiana kumpatia malezi mema na kumjengea misingi ya kumpenda Mungu na hivyo kumuwezesha angalau kufikia sehemu ya malengo yake.

Katika maisha yake anasema hawezi kusahau mshituko mkubwa sana aliowahi kuupata alipopata taarifa ya kifo cha baba yake mzazi mwaka jana kilichotokana na ajali ya gari mkoani Lindi.

“Ulikuwa mshituko ambao siwezi kuuelezea, baba yangu alipenda sana maendeleo yangu na alikuwa anaeleza ni jinsi gani anajisikia fahari kuwa na mtoto kama mimi, lakini hakuna jinsi ni mipango ya Mungu. Namuombea Mungu ampumzishe kwa amani,” anasema.

Anawashangaa watu wanaomuona kuwa ni mpole sana, lakini ukweli ni kwamba anasema siyo mpole hata kidogo ni mtundu, lakini pia ni mchangamfu na msikivu sana. Anasema hata wakati akiwa shuleni alikuwa ni mtundu lakini jambo kubwa alilokuwa akiliwekea kipaumbele ni kuhakikisha anasoma kwa bidii sana ili afikie malengo ambayo alikuwa amejiwekea.

“Unapokuwa shuleni unatakiwa usome kwa bidii, lakini pia muda mwingine ujitahidi kushiriki kazi nyingine nje ya masomo kama vile michezo mbalimbali, hii nayo inasaidia sana,” anasema.

Martina kwa sasa kamaliza kidato cha sita, anasema anatarajia kwa uwezo wa Mungu kufanya vizuri na hatimaye kukamilisha ndoto yake ya kufanya kazi kama Mkaguzi wa Mahesabu (Auditor) na pia anayo hamu kubwa kufanya kazi za Masoko na Matangazo.

Anasema kazi hizo anatamani angezifanya katika kampuni yake binafsi. Angependa kufanya shahada yake ya kwanza hapa nyumbani, na kisha shahada ya pili asomee nchi za Uingereza au Canada ambako kwa mtazamo wake anasema anaweza kupata elimu bora.

Martina hayuko nyuma katika masuala ya uongozi, anasema anatamani kuwa kiongozi kwa kuwa anao uzoefu alioupata Loyola ambako alikuwa kiranja wa habari na alitunukiwa cheti na uongozi wa shule hiyo.

Pia ana uzoefu wa kukabili watu mbalimbali na kuwashawishi kufadhili masuala mbalimbali kama alivyofanya wakati wanaandaa jarida la shule yao linalofahamika kama Loyolight Magazine.

“Nilitafuta wadhamini mbalimbali ambao walifadhili uchapishwaji wa gazeti letu la shule kwa mwaka 2009, nashukuru tulipata wadhamini wengi na kufanikisha uchapishwaji wa gazeti letu la Loyolight,” anasema.

Anawashauri vijana wa Kitanzania popote walipo kuweka malengo yao ya kimaisha mbele kwa kusikiliza ushauri wa wazazi ambao ni muhimu katika maisha yao, waepukane na shinikizo la rika kwani mwisho wake siyo mzuri.

Kwa upande wa wazazi, anawashauri pindi wanapogundua vipaji vya watoto wao waviendeleze, na wasiwashinikize watoto wao kusomea masomo wasiyoyaweza, wawashauri kwa kujali matakwa ya watoto hao.

Martina anasema anatamani kukutana na Rais Jakaya Kikwete, lakini anakiri kuwahi kushikana naye mkono wakati akiwa mdogo sana wakati huo Kikwete akiwa Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa.

“Jambo muhimu ambalo ningemwambia Rais Kikwete ni kwamba viwepo vituo vingi vya kulelea watoto na katika vituo hivyo watoto hao wapewe elimu ya kujitegemea na pia wawezeshwe kimichezo, haya yote yatawasaidia sana katika maisha yao ya baadaye,” anasema.

Martina anakiri kuwa bado anapenda kuimba, lakini kwa sasa anataka kupata sehemu ambako atafanya mafunzo kwa vitendo kutokana na masomo yake.

“Napenda muziki, ila sijui ni lini nitaimba tena kama ilivyokuwa mwanzo, kitu kingine ninachopenda ni kuogelea na kuangalia mchezo wa basketball ukichezwa uwanjani, mimi ni shabiki sana wa mchezo huo,’’ anasema.

Huyu ndiye Martina Chambiri, anakumbukwa sana kwa kipaji chake cha uimbaji akiwa mdogo sana katika umri wa miaka minne, na pia kwa ujasiri wake wa kusimama mbele ya kadamnasi na kuimba bila woga.

Source:Habarileo

My take.

kabinti kalikuwa juu sana miaka 1994 - 1996 nyimbo yake Tanzania ee ilikuwa ikinifurahisha sana hasa tukizingatia umri aliokuwa nao wakati hule.Nimefurahi pia kujua kabinti bado kanaendelea na shule.Mungu ambariki Martina Chambiri natamani kuwa na binti kama Martina.Nimesikitika kusikia baba yake katangulia mbele ya haki hope mama atachukua majukumu ya kukusomesha bila kutetereka hatimae atimize ndoto yake ya kuwa Auditor.
 
Good Martina...Ila habari ya kifo cha baba yake kimenistua. Namfahamu personally ingawa ni muda mrefu hatukuwahi kuwasiliana. Jamaa alikuwa akiitwa Keneth Chambiri..Pole sana kwa kumpoteza baba yako..He was really good guy..!
 
“Ulikuwa mshituko ambao siwezi kuuelezea, baba yangu alipenda sana maendeleo yangu na alikuwa anaeleza ni jinsi gani anajisikia fahari kuwa na mtoto kama mimi, lakini hakuna jinsi ni mipango ya Mungu. Namuombea Mungu ampumzishe kwa amani,” anasema.
nampa pole saaaana, na Mungu akapate kumbariki, aliinua sana nnchi yetu kwa kipaki chake.
 
Nimependa tabia yake pamoja na jitihada zake anazofanya, natamani mabinti wote wangefuata mfano wake. Pole kwa kuondokewa na baba Martina.
 
i am very happy kwamba kuna watu wanrejea mafaili ya stars wetu wa vipindi vya nyuma... nasubiri varda arts group!!
 
hapa naomba nisiwe mchoyo......HONGERA MTANI......labda utaimba kanyimbo kuwaambia ndugu zako wakurya wapunguze jazba.....watani zangu WAHEHE SIKU HIZI WAMEPUNGUZA kujinyonga na KULA KALE KAMLINZI KETU KA USIKU.....hope nawe ukiimba itasaidia......!"ushauri kwa wasanii wa ki-bongo"....nyie mnaojiita sijui JIDE,sijui tonya,sijui nani nani...SHULE KWANZA JAMANI.....! PIGENI SHULE HATA MKISIMAMA MBELE YETU HAMTAKUWA NA UJUMBE MMOJA TU WA MAPENZI.......mtakuwa na jumbe "ZILIZOENDA SHULE"
 
........Ohhh Martina Chambiri namkumbuka sana huyu msichana, enzi hizo za utoto hata mie nilikuwa napenda sana wimbo wake huo wa Tanzania eeTanzania eee nchi yangu ee nakupenda eeeeee!!
Nimefurahi leo kusoma habari zake hapa kuwa anaendelea vizuri huko alipo........na anafanya jitihada kwenye masomo yake.

Nakuombea kila la heri usome bachelor yako bongo na uende ukasome masters yako huko UK,USA au Canada kama mwenyewe ulivyosema hapo, yote yanawezekana ilimradi uwe na malengo na juhudi.
 
........Ohhh Martina Chambiri namkumbuka sana huyu msichana, enzi hizo za utoto hata mie nilikuwa napenda sana wimbo wake huo wa Tanzania eeTanzania eee nchi yangu ee nakupenda eeeeee!!
Nimefurahi leo kusoma habari zake hapa kuwa anaendelea vizuri huko alipo........na anafanya jitihada kwenye masomo yake.

Nakuombea kila la heri usome bachelor yako bongo na uende ukasome masters yako huko UK,USA au Canada kama mwenyewe ulivyosema hapo, yote yanawezekana ilimradi uwe na malengo na juhudi.


usikilize hapa wimbo wa tanzania eh.. anaanza kuimba kwa kiswahili kuanzia dk 3.30 . https://www.youtube.com/watch?v=p2zYpWJNJiw Mimi leo nimeukumbuka huu wimbo nikausearch nikakutana na hii thread na nikafanikiwa kuupata youtube. Please check. Inspirational song. Naijua Tanzania zaidi kuliko Tanganyika..I love my country
 
Huyu binti si ndiyo yule ambaye mama yake ni mtangazaji wa kituo cha Channel Ten?
 
........Ohhh Martina Chambiri namkumbuka sana huyu msichana, enzi hizo za utoto hata mie nilikuwa napenda sana wimbo wake huo wa Tanzania eeTanzania eee nchi yangu ee nakupenda eeeeee!!
Nimefurahi leo kusoma habari zake hapa kuwa anaendelea vizuri huko alipo........na anafanya jitihada kwenye masomo yake.

Nakuombea kila la heri usome bachelor yako bongo na uende ukasome masters yako huko UK,USA au Canada kama mwenyewe ulivyosema hapo, yote yanawezekana ilimradi uwe na malengo na juhudi.
Nimependa "Location" yako hapo juu kulia...
 
hqdefault.jpg
 
New gen hawamjui huyu. Na watanzania kwa kutothamini vya kwetu mpaka huyu binti kaanza kufutika kwenye historia amefanya makubwa kuipaisha Tanzania kimataifa kwa umri alioukuwa nao. She deserve to be recognized once again as hall of famer
 
Back
Top Bottom