Marekani yapaswa kukabiliana kihalisi na changamoto ya ubaguzi wa rangi

ldleo

JF-Expert Member
Jan 9, 2010
1,010
1,034
5df22f804.jpg

Tarehe 21 Machi ni Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi. Katika miaka ya hivi karibuni, nchi za magharibi haswa Marekani, zimepuuza suala la ubaguzi wa rangi katika nchi zao, na kuchukulia suala hilo kama njia ya kisiasa ya kuingilia mambo ya ndani ya nchi nyingine, kitendo ambacho kimeleta athari mbaya katika juhudi za kupambana na ubaguzi wa rangi duniani.

Kaulimbiu ya Siku ya Kimataifa ya Kutokomeza Ubaguzi wa Rangi ya mwaka huu ni “Wito wa Kuchukua Hatua dhidi ya Ubaguzi wa Rangi”. Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres amesema, Waafrika na Waasia na watoto wao, wazawa, wahamiaji na wakimbizi wanakabiliwa zaidi na ubaguzi wa rangi, na kutoa wito wa mshikamano wa jamii zote dunia.

Katika mkutano wa maadhimisho ya siku hiyo ulioitishwa na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Marekani, kwa mara nyingine tena, iliilaumu na kuipaka matope China kuhusu suala la Xinjiang, na kunyooshea kidole nchi nyingine nyingi kwa kisingizio cha haki za binadamu. Waziri wa Mambo ya Nje wa nchi hiyo Antony Blinken alisema, Marekani itaweka vikwazo dhidi ya maafisa wengine wa China wanaohusika na suala la Xinjiang. Lakini kile kinachoitwa “mauaji ya kimbari” na “ubaguzi wa rangi” mkoani Xinjiang ni uongo usio na msingi wowote, na ni njama ya kisiasa iliyofanywa na Marekani.

Nini maana ya “Mauaji ya kimbari”? Marekani inajua vizuri. Historia ya kuanzishwa kwa nchi hiyo ni historia ya mauaji ya kimbari dhidi ya Wahindi Wekundu, ambao ni wazawa halisi wa bara la Amerika. Wakoloni wa Magharibi walioingia Bara la Amerika walidai kuwa waligundua bara jipya, wakimaanisha kutowachukulia Wahindi Wekundu walioishi barani Amerika kwa maelfu ya miaka kama binadamu. Waliwaua na kupora ardhi zao. Baada ya kuasisiwa kwa Marekani, nchi hiyo haikuacha mauaji dhidi ya Wahindi Wekundu, bali serikali ya nchi hiyo ilitunga sera, na kuwaua Wahindi Wekundu kwa makusudi. Mauaji hayo yalisababisha kupungua kwa kasi kwa idadi ya Wahindi Wekundu nchini humo kutoka milioni 5 ya mwaka 1492 hadi laki 2.5 mwanzoni mwa karne iliyopita.

“Ubaguzi wa rangi” ni nini? Marekani inapaswa kujiuliza zaidi. Marekani ilianzishwa kwa msingi wa mfumo wa watumwa wa Afrika. Hadi sasa, Wamarekani wenye asili ya Afrika wanaathirika zaidi na ubaguzi wa rangi. Dunia haijasahau kauli ya George Floyd aliposema “siwezi kupumua" wakati akiuawa na polisi mzungu. Ripoti iliyotolewa na Gazeti la The Lancet inaonyesha kuwa, kuanzia mwaka 1980 hadi 2018, takriban watu 30,800 waliuawa na polisi nchini Marekani, ambapo uwezekano wa watu wenye asili ya Afrika kuuawa na polisi ni mara 3.5 ya uwekezano wa Wazungu.

Tangu kulipuka kwa janga la COVID-19, chini ya uchochezi wa baadhi ya wanasiasa, matukio ya uhalifu wa chuki dhidi ya Waasia nchini Marekani umeendelea kuongezeka. Matukio hayo mjini New York yaliongezeka kwa asilimia 361 mnamo mwaka 2021 ikilinganishwa na mwaka 2020. Zaidi ya hayo, magereza mengi ya binafsi nchini Marekani yanawatendea vibaya wafungwa wenye rangi na wahamiaji, na mauaji dhidi ya watu wenye asili ya Afrika na wengine wa makabila madogo kutokana na ubaguzi wa rangi yanatokea mara kwa mara.

Ubaguzi wa rangi pia unaonekana katika ripoti za vyombo vya habari vya nchi za magharibi. Tangu kutokea kwa vita ya Ukraine, kauli kama vile kwamba “watu hawa wanaokimbia vita sio kama wakimbizi wa Syria”, “hii sio Afghanistan, hii sio Iraqi, vita inafanyika Ulaya iliyostaarabika” zimetokea mara kwa mara katika vyombo vya habari vya nchi za magharibi. Nyuma ya kauli hizo, ni wazo sugu la ubaguzi wa rangi la Wazungu.

Ubaguzi wa rangi ni maradhi sugu duniani. Kama sehemu inayoathiriwa zaidi na ubaguzi wa rangi, nchi za Magharibi haswa Marekani zinapaswa kubadili wazo lao la “Wazungu wako juu zaidi”, kuacha kutumia ubaguzi wa rangi kama silaha ya kisiasa dhidi ya nchi nyingine, na kurudi kwenye njia halisi ya kukabiliana na changamoto ya ubaguzi wa rangi.
 
Back
Top Bottom