Kundi la waasi la MRDC latuhumu kupambana na jeshi la Rwanda
Image captionMajor Callixte Sankara
Mamlaka nchini Rwanda zimetupilia mbali uvumi kuhusu kuwepo ukosefu wa usalama maeneo yanayozunguka msitu wa Nyungwe, ambapo kundi jipya la waasi wa MRCD linalodai kuwa linataka kuangusha uongozi wa Rais Paul Kageme linasemekana kuwa na ngome yake.
Akiongea na wenyeji wa wilaya wa Nyaruguru, inspekta mkuu wa polisi Emmanuel Gasana alisema kuwa licha ya majambazi wachache kuvuka na kuingia Rwanda na kuwapora watu eneo moja la Nyaruguru hali hiyo ilikuwa imeshughulikiwa vilivyo na vikosi vya usalama na majambazi hao kukimbilia eneo walitoka.
Kundi la MRCD (Rwanda Democratic Movement for Change) limetangaza rasmi uasi dhidi ya serikali ya Rwanda. Msemaji wa kundi hilo meja Callixte Sankara ameiambia BBC kwamba ni mwezi mzima sasa tangu majeshi ya kundi lake yakipigana na majeshi ya Rwanda katika msitu wa Nyungwe kusini mwa nchi hiyo ,na kwamba majeshi yao yamehusika katika mashambulizi ya mwezi uliopita katika kijiji cha Nyabimata karibu na msitu huo.
Je, huyu kiongozi wa kundi jipya la waasi Meja Callixte Sankara ni nani?
Ni machache yanayojulikana kuhusu Callixte Sankara, mtu aliyejitangaza kama naibu kamanda na msemaji wa kundi jipya la waasi la Rwanda Movement for Democratic Change.
Meja Callixte Sankara, kama avyojitambulisha kwa vyombo vya habari, ni mwanajeshi aliyekuwa mshirika wa karibu wa rais Paul kagame kwenye kundi la Rwanda Patriotic Front (RPF) katika harakati za kupigania ukombozi.
Alikuwa askari mwenye cheo cha chini baada ya RPF kushinda vita vya msituni na kuchukuwa hatamu za uongozi kufuatia baada ya kifo cha rais Juvenal Hybiamamana kwenye shambulzi la ndege.
Haijulikani kwanini Meja Sankara alikosana na utawala wa kagame, lakini alifungwa jela na mahakama ya kijeshi kwa kipindi kisichojulikana kutokana na kile kilichotajwa kama utovu wa nidhamu.
Image captionMRCD linadaiwa kuwa ngome yake kwenye msitu wa Nyungwe
Baadaye alitoroka nchi na kukilmbilia taifa jirani la Tanzania alikotiwa mbaroni.
Juhudi za utawala wa Kigali wa kutumia waranti bandia za kutaka Dar es salam kumrudisha Meja Sankara Rwanda, ziligonga mwamba na hatimaye serikali ya Tanzania ilimwachilia mhuru na kumwezesha kusafiri uhamishoni Ufaransa.
Callixte Sankara badaye alijiunga na chama cha Rwanda National Congress (RNC) kilichioanzishwa mwaka wa 2010 na waliokuwa washirika wanne wa karibu wa rais Kagame, miongoni mwao mkuu wa zamani wa jeshi Jenerali Kayumba Nyamwasa.
Baada ya miaka kadha, ubishi ulizuka ndani ya chama cha RNC na kusababisha Meja Sankara na Jenerali Kayumba Nyamwasa kutafautiana.
Meja Callixte Sanaka alisomea uanasheria katika chuo kikuu cha Rwanda.Anatoka kabila la Tutsi na ni mjombake kiongozi wa upinzani aliyekizuizini nchini Rwanda Diane Rwigara.
Wakati huo huo kumekuwa na taarifa kuhusu ukosefu wa usalama katika baadhi ya maeneo ndani kwenyewe nchini Rwanda.
Mashambulizi ya kutumia guruneti yameshuhudiwa katika kipindi cha miaka mitano iliyopita. Maeneo ya makumbusho ya mauaji ya halaiki, masoko, vituo vya mabasi na mateksi vimekuwa vikilengwa mjini Kigali na eneo la Ruhengeri. Shambulizi la hivi majuzi la gurunedi lilitokea Juni 2017 kwenye wilaya ya Rusizi ambapo mtu mmoja aliuawa.