Maoni ya washairi juu ya mauaji wa mwanafunzi Aquilina

Idd Ninga

JF-Expert Member
Nov 18, 2012
5,136
4,298
27972265_2004720506209444_6686189691669949683_n.jpg





MOLA AKULAZE PEMA.

kwanza naanza na pole,nawapoza majirani.
Kisha nije vile vile,kuwauza ikhwani..
Yarabi toba salale,ilikuaje wandani?
Mola amlaze pema,peponi palipo wema!

Pili nasonga kivyele,WA TANZANIA jamani
Kifo chake dada yule,kimetapaza uzuni....
Ila ninawapa pole,subira ziwe nyoyoni..
Mola amlaze pema,peponi palipo wema!

Tatu nasonga mi swale,mzorah wa msambweni.
Gatuzi la kwetu kwale,tulipatwa ni huzuni..
Lakini nawapa pole,ndugu zetu majirani..
Mola amlaze pema,peponi palipo wema!

Sichi kuyanena yale,mauwaji yakihuni....
Mauwaji ya kilele,mama wallai yakini..
Walicho kitenda kile,kitendo cha hayawani
Mola amlaze pema,peponi palipo wema!

Natazama huku kule,waja wanaenga dini..
Nyoyo zimejaa ndwele,wallai sio utani...
Vipi mwenzako umle,mchana pa'h hadharani.
Mola amlaze pema,peponi palipo wema!

Aonekana mpole,sijui alifanyani....?
Hadi wao wamkule,tena risasi mwilini..
Bado nazidi na pole,wa TANZANIA poleni.
Mola amlaze pema,peponi palipo wema!

Familia pia pole,ninasema hadharani....
Walio yafanya yale,yarabi mola walani..
Ni unyama vile vile,ila nasema poleni...
Mola amlaze pema,peponi palipo wema!

Ni yule yule //mwana mtulivu.
Mzorah Swalehe wa Gatuzi la KWALE!

HEBU RUDI AKWILINA.

Huku nikihuzunika, kalamu yangu yatona,
Mwanangu umenitoka, kwa kifo kibaya sana,
Aula ungengojeka, si ghafula Akwilina.

Ulitoka u mzima, ila umerudi jina,
Pumzi zako zimekoma, uhai hunao tena,
Wauma wangu mtima, sikuoni Akwilina.

Sijiwezi wako mama, nina kwingi kusonona,
Vigumu pia kusema, hata ningalikazana,
Nabaki kushika tama, nakuwaza Akwilina.

Ninakuomba mwanangu, jaribu japo kunena,
Niage mtoto wangu, kwaheri ya kuonana,
Aga nipoze uchungu, mwana wangu Akwilina.

Nimeufunga mkaja, kama nimezaa jana,
Na jina nikikutaja, kama vile nakuona,
Usambe ninaleleja, hebu rudi Akwilina.

Rudi sasa nakuomba, tupate kusemezana,
Unambe lilokukumba, hata ukauka mwana,
Lirudie lako gimba, nikuone Akwilina.

Imekupiga risasi, japo hukuandamana,
Kama wapo waloasi, nao hukuchangamana,
Kanama kifo rahisi, umekwenda Akwilina.

Mwanangu hawa polisi, fanya uje kuwaona,
Uone hoja nyepesi, risasi kukata kona,
Lau si kama Rais, lingezimwa Akwilina.

Hapa kikomo natia, la kusema tena sina,
Haya yamenizidia, siyawezi wako nina,
Si punde nitajifia, nikufate Akwilina.

20 February 2018 Jumanne 08:14am

Jina la Mtunzi Dotto Rangimoto
Jina la Utunzi Jini Kinyonga
Simu
260e.png
☎ +255762845394
Morogoro Tanzania.



Nalilia Akwilina
Nalia na Akwilina, umeuliwa mjini,
Hata jambo wewe huna, lakukuponza kifoni,
Umeuliwa mchana, nawe ukiwa garini,
Chozi langu limoyoni, nalilia Akwilina.

Umepigwa kosa huna, guruneti ya kichwani,
Hasila nao hauna, yaniumiza moyoni,
Ukowapi Akwilina, umeuliwa kwanini,
Chozi langu limoyoni, nalilia Akwilina.

Ungeumwa ungepona, ama ngeinamachini,
Kifo chako Akwilina, chatupa teso nyoyoni,
Chakuwafanya hatuna, wauaji hawaneni,
Chozi langu limoyoni, nalilia Akwilina.

Wazaziwo hawatena, sononeko link ndani,
Wapendwa tukiwaona, hawana la kuamini,
Umekwenda hukupona, tukuone na wodini,
Chozi langu limoyoni, nalilia Akwilina.

Siasa hakuna tena, hata haifungani,
Uhuru umeungana, na hali ya ukoroni,
Usalama gani tena, kujitupa kaburini,
Chozi langu limoyoni, nalilia Akwilina.

Mwisho unashindwa kuona, usalama hapandani,
Nachoka na kujikana, vifo vyawa burudani,
Twaua na kuzikana, imekuwa tamaduni,
Chozi langu limoyoni, nalilia Akwilina.

Mtunzi
Alpius Mwageni(mgomela)
0655/0753 640506


MACHOZI YA BUBUJIKA.

Nyoyo zimepigwa shindo, umma umetikisika
Hamadi kwenye kibindo, machozi ya bubujika
Roho zimepigwa nyundo, roho zinaungulika
Siku yako imefika, tangulia kwa upendo.

Mwili nyama sio nondo, risasi zimefyatuka
Zina kasi ya kimondo, nyama zinagawanyika
Kila lilo na mgando, kuna siku huganduka
Siku yako imefika, tangulia kwa upendo.

Wamekwanyua matendo, ya ndoto ulizoweka
Ulipanga kwa mitindo, Tanzania kuishika
Usohatia u kando, mahaini wanacheka
Siku yako imefika, tangulia kwa upendo.

Mungu ajuae kondo, mbele yake ukifika
Mwambie kuna msondo, chozi la tububujika
Kila tukipiga tindo, jumba linaimarika
Siku yako imefika, tangulia kwa upendo.

Baba na mama kwa lindo, leo wamefadhaika
Hayajaiva matondo, mtondo umekatika
Mungu muombeni tendo, la nyoyo kusafishika
Siku yake imefika, akalale kwa upendo.

Kijana mwenye upendo, wa Mungu alotukuka
Nenda ukalale kando, nasi twaja kadhalika
Waliokutia pondo, nao wataadhirika
Siku yako imefika, tangulia kwa upendo.

Mwambe Mungu asofundo, damu imekua zaka
Waja leo wako jando, wanafunzwa kutamka
Uluwa ndio mkondo, wanazidi miminika
Siku yako imefika, tangulia kwa upendo.

Hapa nalitia fundo, kwa amani pumzika
Sura zimefanya pindo, twalia na kuanguka
Twakuaga tuko rundo, sana tutakukumbuka
Siku yako imefika, tangulia kwa upendo.

Mtunzi: Jumaa H Heshima
(Tarishi Wa Malenga)
Chuo Kikuu cha Dar es Salaam



MAUAJI YA AQUILINA
1)Swali tunajiuliza,ni nani kama si yeye ?
Kwanza alitueleza tusimjaribu yeye
Leo wametekeleza,alioyasema yeye
Alomua Aquilina,kifo kitamuumbua.

2)Risasi alofyatua,alikusudia yeye
Cheo watampatia,ndicho apendacho yeye
Huko anafurahia kuona yeye ndo yeye
Alomua Aquilina,kifo kitamuumbua.

3)Risasi za nchi yake,ndizo zimemua yeye
Hilo ndo taifa lake,lilomwangamiza yeye
Ya wapi makosa yake,wakamuhukumu yeye
Alomua Aquilina,kifo kitamuumbua.

4)Walotenda wanajua,amri aliwapa yeye
Wafanya aloamua,wasije muudhi yeye
Aquilina kapotea,kisa ajieshinda yeye
Alomua Aquilina,kifo kitamuumbua.

5)Waloandamana wengi,vipi wamuue yeye
Twabomoa hatujengi,vipi kumlinda yeye
Mipango hatuipangi,vipi hatutishe yeye
Alomua Aquilina,kifo kitamuumbua.


6)Watu hawana silaha,vipi kawalenga yeye
Wengi wana majereha,wanalia kisa yeye
Kum Alomua Aquilina,kifo kitamuumbua.
Alomua Aquilina,kifo kitamuumbua.

7)Yote nguvu ya nini,ama alitaka yeye
Watu waanguka chini,pekee abaki yeye
Nchi yangu masikini,yapotea kisa yeye
Alomua Aquilina,kifo kitamuumbua.

8)Jahazi sasa lazama,alotoboa ni yeye
Azisubiri lawama,zitamshukia yeye
Dongo likianza hema,chanzo atakua yeye
Alomua Aquilina,kifo kitamuumbua.

SHAIRI -MAUAJI YA AQUILINA
MTUNZI-Idd Ninga wa Tengeru Arusha
iddyallyninga@gmail.com
+255624010160

AKWELINA KIPENZI.

Sote tunapita ndia, mauti stendi ya mwisho,
Ila ilivyo kujia, moyoni nahaha jasho,
Sili kutwa ninalia, kipenzi sioni kesho,
Wahubani Akwelina, hujafa kwangu moyoni.

Upepo nafukuzia, nafurukuta silali,
Tonge jaza la sinia, hamu naikosa sili,
Siye ulikusudia, lango uliibatili,
Wahubani AKWELINA, hujafa kwangu moyoni.

Haina raha dunia, ilivyo kama kichomi,
Aliyekuua dia, kuzimu hakumtemi,
Tama itawafikia, hata wakafyata ndimi,
Wahubani AKWELINA, hujafa kwangu moyoni.

Ua uliyechanua, ukapendeza mibani,
Lisilo la kununua, lilikuzwa mchangani,
Jani lililovotia, limedondoka mtini,
Wahubani AKWELINA, hujafa kwangu moyoni.

Iwe kesi ya jinai, kwaye aliyedhubutu,
MAKONDA baba sikia, kaadhibu hao watu,
KAMANDA SIRO fyatua, wafe nao kwa mtutu,
Wahubani AKWELINA, hujafa kwangu moyoni.

Sana walioumia, ndugu na jamaa zako,
Zaidi kanyong'onyea, huruma kwake mamako,
Kiwete ungeniwia, nikufichie mbeleko,
Wahubani AKWELINA, hujafa kwangu moyoni.

Akuhifadhi jalia, kuliko roho za wafu,
Kusema naongopea, sijaona yako kifu,
Mwenyezi kakuumbia, moyo wako mkunjufu,
Wahubani AKWELINA, hujafa kwangu moyoni.

Uledi Bryan.
Kinda Mtunga Nudhuma.
Kedowa_Kericho_Kenya.
Simu +254724845351.
bryanrop8@gmail.com.





MKUSANYAJI-Idd Ninga wa Tengeru Arusha
iddyallyninga@gmail.com
+255624010160
WATUNZI-MZORA SWALEHE
DOTTO RANGIMOTO
ALPIUS MWAGENI
JUMA H HESHIMA
IDD NINGA
BRIYAN MADDIE


Nimeamua jua na njia nyingine ya kutembelea jukwaa hili badala ya kupost katika jukwaa la lugha kwa sababu hata tukio lolote lilisababishwa na siasa.
 
MAUAJI YA AQUILINA
1)Swali tunajiuliza,ni nani kama si yeye ?
Kwanza alitueleza tusimjaribu yeye
Leo wametekeleza,alioyasema yeye
Alomua Aquilina,kifo kitamuumbua.

Hivi ni nani alisema hajaribiwi?
 

Similar Discussions

Back
Top Bottom