Kwako Mh.Joshua Nassar ,
Pole kaka yangu kwa changamoto zote ambazo umepitia na hongera kwa kupata mtoto Mungu ampe afya njema na amkuze.
Pia pole kwa kuvuliwa ubunge najua namna unavyojisikia vibaya ,inauma sana .
Ila nimesikia mkutano wako wa vyombo vya habari (Press conference), umeongea vizuri sana hasa ulipojishusha na kuomba Mh.Spika arejee maamuzi yake kwa busara kama mlezi.
Mh.Nassar najua sio muda huu wa kukulaumu ila ni muda wa kuambiana kuwa wapi ulijisahau kidogo na wapi uliteleza kidogo ,kwani kupitia kujua ulipoteleza ndio mwanzo wa kufahamu wapi pakutokea na kujifunza kwa wabunge wengine na kuishi kwa tahadhari.
Ni kweli kabisa ,Mh.Spika Ndugai alipaswa atumie busara kama mzazi na mlezi wa Bunge ,ila na wewe pia Mh.Nassari ulipaswa kuwa na tahadhari kwa kuangalia namna ulivyokuwa vocal critics bungeni ,kwa kuangalia aina ya spika na kalba yake,kwa kujiangalia wewe ni mbunge wa chama gani mpinzani au Chama tawala ,kwa kuangalia pia namna upinzani unavyokumbana na changamoto .Hayo yote yangekupa fahmu ya kujua tahadhari ipi ulipaswa kuchukua.
Mkutano wako na vyombo vya habari uliacha maswali kadhaa ambayo hayakujibika hasa ulipokataa maswali ,labda ni kwa sababu zako muhimu.
Mh.Nassar uongozi au kazi ya kuhudumia wananchi haina maana ya kuacha kuhudumia au kuuguza familia hapana hata kidogo,ila kuna taratibu zake za kufuata ,huku wajibu wa msingi wa kuhudumia au kuuguza familia ukabaki nao na usiathiriwe.
Mh.Nassar ,Spika labda na yeye hakutumia busara ila hata na wewe kuna majukumu fulani uliyaruka ,ukasau kuyafanya aidha kwa mawazo ya kuuguza shemeji yetu au kwa kusahau.
1. Mh.Nassar wewe ofisi yako ni Bunge la jamhuri katika taratibu mlezi na bosi wako ni spika wa bunge ,ulipaswa kuandika barua ukaipeleka au ikapelekwa na mtu kwaniaba yako kwa despatch book ,sababu kutokuhudhuria vikao sio jambo dogo ni swala nyeti ,Mh.Lema angekupelekea bungeni kwa despatch au mbunge yeyote unaye muamini hivyo ungekuwa na ushahidi wa kutosha leo.
Ila Mh.Nassar unasema ulimuomba msaidizi wa spika email ya spika ,Mh.Nassar ni kweli email au barua pepe iko kundi moja na registered mail, DHL, EMS n.k. Kwenye zote hizi, proof ya kupokea ni utumaji. Once sent, it's deemed to have been delivered.
Ila hofu yetu ni kuwa vipi kama aliyekupa email ya spika alitoa email ambayo sio active kwa makusudi ? ,vipi kama Mh.Spika aliona email yako ila akasema hajaona kwa makusudi au hajaiona kweli ? ,vipi kama mh.spika akiikana kwa makusudi email uliyotumia kuwa sio yake na akadai aliyekupa amekudanganya ?.
Turudi kwa hoja ya awali kuwa ulipaswa kupeleka au mtu akakupelekea barua ofisi ya spika kwa despatch book leo ungekuwa unatuonesha saini ya kupokea barua sio texts za whaatsp za msaidizi wa spika.
Pia ulisema Bunge la mwanzo wa January mwaka jana na Novemba mwishoni 2018 ,hukuwepo ,huku ukisema uliandika barua January hii ya 2019 ila hujasema huko nyuma ,kama ulitoa taarifa kwa spika au laa .
2.Mh.Nassar wewe ulikuwa unawakilisha wananchi wa Arumeru mashariki waliokuchagua kwenda bungeni ,hivyo wewe ulikuwa Agent kwao na wao kwako ni principal, hivyo wewe ulikuwa unawajibika kwao, sababu bungeni haukuwa unaenda chukua posho ila kuwawakilisha wao ,ulipaswa kutoa taarifa ya kiofisi (Ofisi ya Mbunge ) kwenda kwa wananchi kuwa hautakuwepo bungeni kutokana na changamoto za kuuguza ,hakika matatizo yameumbiwa binadamu ,wananchi wako wangekuelewa na wangekuwa wanakuombea dua na baraka kwa Mungu.
3.Mh.Nassar ,wewe ulipita kupata uwakilishi kupitia Chama chako ,Bungeni kuna ofisi ya Kiongozi wa kambi rasmi ya upinzani (KUB) ,ofisi ya party whip ambaye kaimu ni Mh.Selasini pia katika chama chako kuna uongozi Katibu au ofisi ya mwenyekiti .Hawa walipaswa kupata barua yako ya kutohudhuria bungeni kutokana na changamoto za afya ya shemeji yetu (Mke wako) na Afya ya shemeji yetu ilikuwa na uzito mkubwa hakuna ambaye angekataa ,ungepata pia baraka za chama chako na viongozi wako ,hata nakala ya barua ambayo ungetuma kwa spika ingetosha tuu kuwatumia na wao.
Leo Kaka yangu Nassar ungekuwa na utetezi kutoka pande zote ,watu wameumia na wanasikitika ila kuna sehemu nyingi uliteleza ukajisahau ndio maana wanashindwa wasimame kutetea namna gani.
Ushauri wangu kwako kaka yangu.
1.kaa pamoja na wanasheria wako uwasilikize kama kuna ushihidi wa kutosha (Evidences ) na (Vithibitisho) exhibits vya msingi ambavyo vitasaidia kama ukifungua kesi kupinga haya maamuzi ,simama imara pinga bila kuvunjika moyo kutafuta haki yako na ya wananchi wako.
2.Ila kama kweli wanasheria wameona hakuna ushahidi na vithibiti vya kutosha ,Nakuomba ujadiliane na viongozi wako kwenda kuongea na ofisi ya spika ,busara yake itumike hapa kama mzazi na mlezi wa wabunge wote .
Aguswe na afya ya shemeji yetu ,aguswe na changamoto ulizopitia na ukiri kuwa kweli ulikosea kutokana na changamoto za kuuguza shemeji yetu (Mke wako ) ,na usiache pia kumuomba Mungu akuvushe katika kipindi hiki kigumu hakika Mungu atakujalia ,na hakika Mungu atampa busara zaidi Mh.Spika katika kuangalia maamuzi yake upya .
Pole sana kaka yangu,Mungu ampe afya njema mdogo wetu na mama huko nyumbani ,awape uvumilivu wa kutosha katika kipindi hiki kigumu.
Abdul Nondo.
abdulnondo10@gmail.come
Sent using
Jamii Forums mobile app