KWAHERI MANCHESTER UNITED. IPO SIKU TUTATIZAMA EPL KWA AKILI
Wakati msimu unaanza wadau wa United walisema hakuna Champions League bila ya Manchester United......Hakuna ushindi kwa Waingereza kwenye Uefa bila Manchester United.
Manchester United ndio timu iliyokuwa inakosekana katika Uefa Champions League.
Ngoja nilitizame kundi na nguvu ya wapinzani.
Wolfsburg ni ya tano kwenye ligi ya nyumbani
Psv ni ya Tatu kwenye ligi ya nyumbani.
Manchester United ni ya nne kwenye ligi ya nyumbani.
CSKA Moscow, ni ya kwanza kwenye ligi ya kwao.
Nahisi inabidi tuhame katika Imani ya kuwa ligi ya Uingereza ni ligi bora kwa kuamini ukali wa vilabu vyao... Lakini ni ligi bora katika nyanja ya ushindani baina ya vilabu vinavyoshiriki.
Ukitaka kujua kuwa hata ligi nyingine si haba, jiulize viungo wangapi wa United Jana walikuwa na uwezo wa kariba ya Max Kruse, Schurlle na Julian Drexler.
Macho ya mashabiki wa Epl yanaona yasichokiamini, na yanakitizama yasichokitaka. Manchester United haina tena Paul Scholes, Ronaldo, Rooney (yule mwenye Upara) inaye Lingard, Fellain na Depay na Rooney mwenye nywele.
Liverpool haitokuwa na Gerrard mwingine kwa siku za karibuni tena, wala Suarez kwa miaka kadhaa ijayo. Sasa hivi Wana Sturridge tu ambaye anakaa ghetto miezi 4, uwanjani miezi 2, miezi 2 mingine kwa specialist Marekani.
Manchester City mpaka wajifunze kucheza vyema nyumbani. Mochengladbach sio Madrid, unamruhusu vipi akutangulie goli 2? Usipoweza kujilinda Etihad, utaweza kuzihimili kelele na nguvu za Camp Nou, Santiago Bernabeu na Allianz Arena?
Chelsea ugonjwa wao bado unatafutiwa utafiti. Maisha ya Jose Mourinho yameuzidi kasi mshale wa saa. Wanaumwa ule ugonjwa wa "Rare Diseases" magonjwa nadra ambayo tiba yake mara nyingi ni kifo. Unaishije kama kundi lako Porto ya mkameruni Aboubacar inakaribiana kiwango na Chelsea ya Diego Costa na Hazard?
Unapojivunia ukali wa ligi kwa sababu Leicester amekaa kileleni, jiulize kwanini Valencia, Atletico na Sevilla hawakai kileleni kule kwao japo wanasumbua Uefa na Europa.
Unapojivunia Origi ndani ya klabu yako na Hat Trick yake, jiulize Dyabala, Mandzukic, Zaza na Morata wanafanya nini kwa pamoja pale Juventus. Historia nasikia inasema hakuna milki au ngome itakayodumu milele, lakini hii ya Uingereza tunaidumisha kwa kelele zetu tu.
Wakati Javi Martinez akiwa anashikilia jezi na viatu Muda mwingi pale Munich kuliko anavyopiga pasi uwanjani, pale Arsenal akikosekana Coquelin amani inatoweka. Martial anayetakiwa kukuzwa bila Mzigo kama alivyofanyiwa Morata au anavyofanyiwa Coman Sasa hivi pale Munchen, amegeuzwa kuwa Ronaldo, Messi, Lewandowski, Neymar, Suarez, Muller au Bale. Bahati mbaya ni kuwa bado hawezi kuamua mchezo kwa walau kiwango cha Morata, sio kwa sababu hana uwezo ila akili yake haijakomaa hivyo ambavyo mashabiki na kocha wetu anataka iwe.
Nipo naandika huku kichwa kimejaa mawazo juu ya namna ambayo Olympiacos na Dinamo Zagreb wanaweza kuiweka Arsenal huko ilipo. Sidhani kama ili lingekuwa uhalisia misimu 3 na kuendelea huko nyuma. Ndoto ya kweli imekuwa maisha halisi lakini imekuja mapema sana.
Bahati kubwa ni kuwa mkataba wa haki za televisheni wa Epl peke yake kwa vilabu, unaweza kumfungulia kila Mtanzania ghala la chakula, pesa ya usajili ya kila klabu katika vile Sita, inavilipa vilabu vyote vya Bundesliga mshahara kwa wakati mmoja na chenji inabaki. Kwanini Aguero asitamani kwenda Barcelona sasa? Kwanini msiendelee kuwalaumu wa Amerika ya Kusini kutokucheza Uingereza. Mpira hakuna, starehe hakuna, na nyota kwenye timu yako ni Depay aloshindwa kufikia tunachotaka wakati Porto Kuna Brahimi.
Siku ambayo macho yatafunguka tutagundua kuwa tofauti kati ya Liverpool na Sevilla ni ndogo sana, tofauti kati ya Manchester City na Bayern Munich ni kubwa sana. Ile tofauti kati ya Manchester United na Barcelona na Madrid haipimiki kwa vipimo vya macho ingawa bajeti za usajili zinakaribiana. Huku Arsenal na Atletico Madrid ni kisu kwa panga. Ni ukweli mchungu uliozibwa na imani, ni bahati mbaya tu kuwa hatujui kuwa Mioyo ndio inadadavua Epl na sio akili.
Leo Nicasius Coutinho Suso nasema, siku ambayo watanzania watagundua kuwa maisha ya Daudi na Goliath yamebaki kwenye vitabu, hapo pekee tutajua ni kwa namna gani Dortmund anaweza kuishi kirahisi ndani ya ligi yetu pendwa. Ila ni mpaka akili ziamue kutizama Epl na sio mioyo.
Ahsanteni.
By Nicasius Coutinho Suso