Mambo ya Kuzingatia ili Kutoa Huduma Nzuri kwa Wateja

Miss Zomboko

JF-Expert Member
May 18, 2014
4,502
9,282

1. Elewa hitaji la mteja​

Kamwe huwezi kumhudumia mteja vizuri bila kufahamu hitaji lake. Mara mteja anapofika katika biashara yako hakikisha unafahamu na kuelewa vyema anahitaji nini kabla ya kumhudumia.

2. Jitosheleze kihuduma​

Kabla ya kuamua kutoa huduma yoyote kwa mteja hakikisha unajitosheleza katika kutoa huduma . Hakikisha vitendea kazi vyote kama vile bidhaa, mifumo, chenji na maarifa na ujuzi wa kutoa huduma husika unavyo vya kutosha ili uweze kutoa huduma nzuri kwa mteja.

Si jambo sahihi mteja kuja kwenye biashara yako kisha unaanza kumwambia kauli kama vile: Ngoja nikakubadilishie hii bidhaa pale, ngoja nikaombe chenji pale, ngoja nikaulize bei ya hiki kitu kwa jirani, ngoja nimpigie bosi anieleze jinsi ya kutoa huduma hii n.k.

3. Mthamini mteja kuliko pesa​

Mara kadhaa nimekuwa nikisisitiza kuwa pesa ni ujira anaopewa mtu baada ya kutatua tatizo la mteja.

Hata hivyo, jambo la kusikitisha ni kuwa wafanyabiashara wengi hutazama zaidi kupata pesa kuliko kumridhisha mteja kwa huduma nzuri kwanza.

Hii ndiyo sababu wafanya biashara hupanga bei hovyohovyo au hata kwa kuiga bila kumfikiria mteja zaidi. Wafanya biashara wanaothamini zaidi pesa wao hufanya jitihada sana kuhakikisha mteja analipia bidhaa au huduma hata kama atafanya hivyo kwa shingo upande au akilalamika.

Ukitazama kwa makini pia utabaini kuwa hii ni moja ya sababu inayofanya baadhi ya wafanya biashara kuuza bidhaa bandia au kwa njia ya ujanja ujanja ili tu wapate pesa.

4. Jifunze lugha nzuri kwa mteja​

Suala la lugha duni kwa mteja ni tatizo kubwa sana katika biashara nyigi za sasa.

Kwenye biashara nyingi wateja hujibiwa kwa mkato, mkato au hata kukejeliwa na watoa huduma kwani wanaonekana hawana thamani bali wenye thamani ni wafanya biashara/watoa huduma.

Ikiwa unataka kufanikiwa kwenye biashara yako ni lazima uhakikishe umetoa kauli nzuri kwa mteja. Hakikisha mambo yafuatayo katika suala hili,

i. Mkaribishe mteja kwa heshima na uso wa furaha.

ii. Sikiliza na muulize mteja kuhusu hitaji lake kwa lugha ya staha

iii. Kuwa na utulivu unapozungumza na mteja siyo unashika hiki, unaongea na yule n.k.

iv. Mpe mteja nafasi ya kuuliza na kupata ufafanuzi au taarifa anayoitaka.

v. Mshukuru na mkaribishe mteja kuja wakati mwingine. Unaweza pia kumjulisha kuhusu huduma nyingine zilizopo ili atakapozihitaji wakati mwingine afahamu atakapozipata.

Pasipo shaka ukizingatia mambo tajwa hapo juu utatumia mbinu ya kauli nzuri kwa mteja ili kufanikisha utoaji wa huduma bora.

5. Kuwa mwaminifu​

Kuna msemo usemao “uaminifu ni mtaji” Ndio uaminifu ni mtaji muhimu sana katika kufanikisha suala la kutoa huduma nzuri kwa mteja hasa katika dunia na kipindi hiki ambacho watu wengi siyo waaminifu.

Wewe kama mfanya biashara au mtoa huduma hakikisha unazingatia mambo yafuatayo katika kutoa huduma kwa uaminifu:

i. Uza bidhaa bora na stahiki kwa mteja, usiuze bidhaa feki au duni.

ii. Uza bidhaa kwa bei halali.

iii. Usitumie mbinu yoyote kumlaghai au kumrubuni mteja.

iv. Kuwa mwaminifu juu ya mali na fedha za mteja. Iwapo mteja atasahau au atazidisha fedha hakikisha unamrejeshea fedha au mali yake.

v. Unapobaini mteja amepata tatizo kama vile kupata huduma au bidhaa yenye dosari, hakikisha unatafuta njia ya kumsaidia na si kujitetea kuwa mali ikishauzwa hairudishwi au kubadilishwa.

vi. Hakikisha unatoa huduma na bidhaa unazotozitangaza na kuzielezea kuwa zipo kwenye biashara yako. Kwa mfano siyo sawa kusema unauza mchele safi lakini ukauza mchele uliojaa chuya au mawe. Au kujinasibisha Kuwa unatoa huduma 10 kumbe zinazopatikana ni mbili tu.

Pasipo shaka ukizingatia haya utatumia mbinu ya uaminifu katika kuhakikisha unatoa huduma nzuri kwa wateja wako.

6. Jali muda wa mteja​

Kwa hakika hakuna mteja anayependa kupoteza muda wake wakati wa kutafuta huduma au bidhaa.

Uwapo katika biashara hakikisha unatengeneza mfumo mzuri wa utoaji huduma ambao hautompotezea mteja muda.

Ikiwa biashara yako inahudumia wateja kwa wingi andaa utaratibu wa kuajiri watoa huduma zaidi ili kupunguza foleni kwa wateja.

Hakikisha pia umeweka mpangilio mzuri wa utoaji huduma ambao hautawachelewesha wateja.

7. Pokea maoni na mrejesho​

Biashara nyingi hazifahamu umuhimu wa kupokea maoni au mrejesho kutoka kwa wateja, na hii ndiyo sababu si jambo la kawaida kuona biashara nyingi za kiafrika zikipokea mrejesho kutoka kwa wateja.

Unapojijengea utaratibu wa kupokea maoni na mrejesho kutoka kwa wateja utabaini changamoto zinazowakabili wateja ili uziboreshe pamoja na kufahamu wateja wanapendekeza au wanahitaji ufanye maboresho gani. Kupitia maoni na mrejesho kutoka kwa wateja utaweza kubaini ikiwa mipango na mbinu zako za mauzo na utoaji huduma kama zina ufanisi au la.

8. Tumia nafasi ya teknolojia​

Ulimwengu umebadilika kwa kiasi kikubwa vivyo hivyo pia ulimwengu wa biashara.

Kufanya biashara katika ulimwengu huu wa sasa bila kuzingatia nafasi ya teknolojia ni sawa na kufanya kazi gizani. Hakikisha unatumia teknolojia kurahisisha utoaji wa huduma kwa wateja pamoja na utunzaji wa taarifa zako muhimu za biashara ili biashara iwe na ufanisi.

Matumizi stahiki ya teknolojia yatakuwezesha kutoa huduma nzuri kwa wateja ambayo wataifurahia na kuona thamani halisi ya pesa yao.

9. Tumia nafasi ya fidia na kuomba msamaha​

Siyo kila mara mambo yote yataenda sawa kwa wateja. Ukiwa kama mfanyabiashara anayejali suala la kutoa huduma bora kwa wateja ni lazima uweke utaratibu wa fidia na kuomba radhi pale ambapo jambo fulani halikwenda sawa kwa mteja.

Moja kati ya jambo linalo tangaza biashara kama inatoa huduma bora kwa wateja ni namna inavyofanya kazi changamoto zinazokabili wateja wake. Unaweza kufanya yafuatayo:

i. Tenga fedha kwa ajili ya fidia au kumudu hasara

ii. Tengeneza utaratibu wa kupokea na kutatua changamoto za wateja wanaohitaji fidia au matengenezo.

iii. Ondoa/Boresha bidhaa na huduma zinazoleta changamoto au zinazohitaji fidia na matengenezo kwa wateja.

10. Jifunze kila siku​

Kujifunza ni msingi muhimu wa kufanikiwa kwenye jambo lolote unalolifanya. Kila mara jifunze kutoka kwenye kampuni na biashara zilizofanikiwa jinsi zinavyotumia mbinu na mikakati mbalimbali katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja.

Zipo kampuni mbalimbali za kitaifa na kimataifa kama vile Google, Amazon au hata Apple ambazo zimejijengea mfumo madhubuti katika kuhakikisha wanatoa huduma bora kwa wateja.
 
Hayo mambo ya kizamani sana, siku hizi unafanya biashara wala nteja huonani nae,
Mtandaoniiiiiiiiii,
So hayo yote hayahitajiki,
Lakini pia yakihitajika uwaambie na wateja nao wawe na heshima kwani wengine viburi sana kisa anatoa hela
Wengine kwao mteja ni fala tu
 
Ahsante kwa muongozo...

Tatizo binadamu wa siku hizi ni wabishi sana...
 
Back
Top Bottom