Mafisadi wapanga
'mapinduzi' CCM
- Lengo ni kuzuia kufukuzwa kwao kwenye chama
- Mbinu zasukwa kumwengua JK kama mwenyekiti wa CCM
- Mabilioni ya shilingi yatengwa kukiteka chama
MWANDISHI WETU
Dar es Salaam
KUNDI hatari la wanachama waandamizi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM)
ambalo linajumuisha watuhumiwa wakubwa wa ufisadi nchini sasa
linapambana usiku kucha ili kujaribu kuzuia chama hicho kuwatosa katika
kikao kijacho cha Halmashauri Kuu ya chama tawala (NEC) wiki ijayo,
KULIKONI limeelezwa.
Mkakati wa kuwaengua watuhumiwa wa ufisadi umeelezwa kuwa ni sehemu ya
utekelezaji wa kauli ya Mwenyekiti wa CCM, Rais Jakaya Kikwete, ambaye
alisema ili kukabiliana na upinzani chama hicho tawala ni lazima
kiwatose wanachama wake ambao ni mzigo kwao.
Katika hotuba yake ya hivi karibuni, Rais Kikwete, alitumia msemo wa
kuiga nyoka wanaojivua gamba na kwamba ikibidi ni lazima CCM nayo
kujivua gamba na kubaki chama kisafi kisicho na doa.
Habari zinaeleza kwamba, baada ya kauli hiyo ya Kikwete, baadhi ya watu
ndani ya chama hicho walianza kujipanga kupendekeza kutoswa kwa
watuhumiwa wa ufisadi walio ndani ya uongozi wa chama hicho ili
kukiepusha chama hicho na tuhuma zilizoelekezwa kwao.
Tuhuma ambazo zimetajwa wazi wazi katika vikao vyama chama hicho,
ikiwamo vile vya Umoja wa Vijana wa chama hicho (UVCCM), ni pamoja na
kashfa ya mradi wa umeme wa dharura uliokabidhiwa kampuni ya Richmond
na baadae mrithi wake Dowans.
Pia vigogo wa CCM waliohusishwa na tuhuma ya ufisadi wa rada nao ni
miongoni mwa 'magamba' ambayo makada wa chama tawala wanataka
kuondokana nayo.
"Unajua kuna kundi moja hatari sana CCM ambalo ni mtandao unaojumuisha
vigogo wenye tuhuma kubwa za ufisadi ikiwemo kashfa ya Richmond, rada,
Kagoda, Meremeta na tuhuma nyingine chafu," alisema kada mmoja wa CCM.
"Kundi hili limetenga mabilioni ya shilingi ili kinara wake ndiye awe
Rais ajaye licha ya kuchafuka sana kwa tuhuma nyingi za ufisadi na
kujilimbikizia mali ndani na nje ya nchi."
Tuhuma hizo zimeelezwa kuwa chanzo kikubwa cha kushuka kwa umaarufu wa
chama hicho na mjumbe mmoja kutoka mkoa wa Arusha, Mrisho Gamba,
alikiambia kikao cha Baraza Kuu la UVCCM, mjini Dodoma hivi karibuni
kwamba hakuna sababu ya kuuma maneno kuhusu hilo.
Kauli hiyo ya Gambo ambayo imeelezwa kuungwa mkono na vijana wengi na
hata baadhi ya wazee kutoka bara na visiwani, imeelezwa kujikita katika
vichwa vya baadhi ya wajumbe wakiwamo viongozi wastaafu.
Utashangaa kuona kwamba hiyo ajenda inaungwa mkono na wazee ambao
huwezi kuamini, japo nao wanapingana na baadhi ya hoja zilizotolewa na
UVCCM, lakini hilo la kutoswa mafisadi halina mjadala, alisema
kiongozi mmoja wa UVCCM.
Habari zinaeleza kwamba Rais Kikwete amekuwa makini katika kukubaliana
na mkakati huo wa kujivua gamba kutokana na sababu za kisiasa na
kiusalama kuepuka mpango huo kutumika vibaya kumjengea maadui ama
kuwaingiza watu ambao hawahusiki na kashfa zozote bali wamekuwa
wakiisaidia CCM ionekane nayo si chama cha mafisadi.
Rais anakwepa watu wasioitakia CCM mema kutumia nafasi ya kujivua
gamba kuwahujumu viongozi ambao wamekuwa mstari wa mbele katika
kupambana na ufisadi na hivyo kukifanya chama chetu kujitenga na
watuhumiwa wa ufisadi walio ndani ya chama chetu, anasema mjumbe wa
NEC kutoka Zanzibar.
Imeelezwa kwamba wajumbe wa Zanzibar wataweka wazi kuhusu kuutaka
uongozi wa juu wa CCM kuchukua hatua dhidi ya watu ambao wamesababisha
chama hicho kupoteza baadhi ya majimbo na hata kupungua kura za mgombea
urais wa CCM.
Kuna watu ambao wamesababisha wapinzani na hasa CHADEMA kupata ajenda.
Walisababisha Mwenyekiti wetu akasirikiwe na watu kwa kuwanadi. Watu
kama hao si wa kuachwa, ni lazima watoswe, anasema mjumbe huyo wa
Zanzibar kwa sharti la kutotajwa.
Mbali ya kushughulikia watuhumiwa wa ufisadi, imeelezwa kwamba vijana
ndani ya UVCCM ambao wameelezwa kupingana na dhana ya kujivua gamba nao
watashughulikiwa kwa maelezo kwamba itakua ni hatari kwa vijana kuanza
kutumika.
Kundi hilo la mafisadi ndani ya CCM sasa linadaiwa kufadhili mapinduzi
baridi yenye lengo la kumwengua Kikwete kama Mwenyekiti wa Taifa wa
CCM.
"Mtandao huu wa mafisadi unataka kugeuza kauli ya Rais Kikwete
mwenyewe ya kuleta mabadiliko kwenye chama kwa kumuengua kama kiongozi
wa chama," alisema mjume mmoja wa NEC ya CCM.
"Wajumbe kadhaa wamepangwa kuleta hoja kwenye vikao vya Kamati Kuu na
NEC kuwa ni bora Rais Kikwete aachie nafasi yake ya Mwenyekiti wa
Taifa wa CCM ili aweze kupata muda mwingi zaidi kushughulikia matatizo
ya taifa kama Rais."
Inadaiwa kuwa kundi hilo la mafisadi linatembeza pesa nyingi kwa
wajumbe wa NEC, Kamati Kuu na Mkutano Kuu wa chama ili kufanikisha
mapinduzi hayo.
"Pia baadhi ya wazee maarufu wa chama wako kwenye listi ya watu
watakaopewa rushwa ili kuunga mkono mapinguzi haya baridi," alisema
kada mmoja wa CCM.
"Ni mkakati mpana sana umepangwa. Watadai kuwa mabadiliko hayo ni kwa
nia njema ili Rais apumzike na majukumu ya chama na badala yake
ateuliwe kiongozi waliompanga ili awe mwenyekiti wa CCM na hivyo basi
Rais wa 2015."
Vyanzo vyetu ndani ya CCM vinasema kuwa wanachama wengi wanapendelea
kuwa Katibu Mkuu wa chama tawala, Yusuf Makamba, ang'atuke ili
apatikane kiongozi mwingine atakayeleta ufanisi zaidi.
Taarifa zinadai kuwa kuna baadhi ya makada wa siku nyingi wa CCM
tayari wamemshauri Makamba kusoma alama za nyakati na kujiuzulu yeye
mwenyewe.
Wajumbe kadhaa wa UVCCM wameweka bayana kuwa ni lazima mafisadi
watimuliwe kwenye chama na Makamba astaafu ili kuleta uhai mpya kwenye
chama kuelekea 2015.
(Source: KULIKONI, Aprili 8, 2011)