MAMA YANGU ADUI YANGU - 21-
ILIPOISHIA
Mwaija.
Abee.
Mzee Sambi.
Naam.
Majibu yenu yametoka, sasa sijui niyatoe kwa kila mmoja au kwa wote?
Kwa wote, sababu ya kuja pamoja kila mtu anataka kujua afya ya mwenzake.
Vizuri, je, mpo tayari kupokea majibu yenu?
Daktari acha mbwembwe we tupe jibu tujue tunasuka au tunanyoa, mzee Sambi ilibidi amweleze daktari aliyeonekana jambo dogo anataka kulikuza kitu ambacho humuongezea mtu hofu moyoni.
SASA ENDELEA...
Sawa nimekuelewa mzee, majibu yenu yapo kama ifuatavyo wote wawili kwa vipimo vya awali vinaonesha mpo sawa.
Una maanisha? nilimsikia lakini sikumuelewa.
Damu yenu wote inaonesha ipo safi.
Ooh! Alhamdulilah, japokuwa nilikuwa na uhakika na afya yangu lakini nilimshukuru Mungu kwa vile sikuwa na uhakika wa uaminifu kwa mtalaka mwenzangu kwa asilimia mia moja.
Lakini upande wa mzee Sambi yeye alikuwa yupo katika hali ya kawaida zaidi ya kutabasamu na kuninyanyua na kunikumbatia kwa furaha.
Hongera mpenzi wangu.
Asante.
Jamani kama nilivyosema vipimo vya awali ndivyo vinavyoonesha mpo salama.
Ina maana kuna majibu mengine? nilijikuta nikiuliza kwa sauti huku nikijitoa kifuani kwa mzee Sambi.
Hapana ila mnatakiwa msikutane bila kinga mpaka mchukue vipimo vya pili ambavyo ni baada ya miezi mitatu.
Kwa upande wangu sihitaji kurudia kwani nina zaidi ya miaka miwili, simjui mwanaume.
Mmh! Hongera.
Hata mimi nilikuwa najijua nipo salama, lakini ili kuzidi kumtoa hofu nitafikisha miezi mitatu nitapima tena ndipo tuanze uhusiano rasmi, mzee Sambi alinitoa hofu.
Basi mi niwapeni hongera kwa kutunza afya zenu, majibu yasiwape kiburi bali yaongeze uaminifu katika uhusiano wenu, daktari alituasa.
Asante daktari.
Baada ya kuchukua majibu na kupata nasaha za daktari tuliondoka kurudi nyumbani. Njiani moyo wangu ulijikuta ukijaa furaha na kuanza kumuamini mzee Sambi ambaye tokea mwanzo alionesha nia njema kwangu.
***
Mzee Sambi aliendelea kunipeleka na kunirudisha nyumbani kwa mtindo wa kuniacha njiani na kunipa fedha ya teksi. Wiki mbili baadaye alinijulisha kiwanja kimepatikana na mwisho wa wiki alinipeleka kwenda kukiona.
Kiwanja kilikuwa kizuri sana kilichokuwa maeneo ya Boko, hakikuwa mbali na Barabara ya Bagamoyo. Kilikuwa kikubwa cha kutosha kujenga nyumba kubwa na kubakia eneo la kupumzikia.
Kwa kweli siku ile kwa mara ya kwanza nilifurahi sana na kumkumbatia mzee Sambi kwa furaha ya kweli toka moyoni.
Asante mpenzi wangu.
Huu ni mwanzo tu, nataka uamini sipo na wewe kukupotezea muda wako bali kuhakikisha nayabadili maisha yako.
Asante mpenzi naanza kuamini.
Utaamini siku moja, najuta kuchelewa kukufahamu mapema.
Hayo achana nayo tugange yaliyopo nayajayo.
Basi mpenzi tukirudi kwenye gari nitakuonesha ramani ya nyumba yako inatakiwa kuwa vipi?
Ramani yake ipo wapi? nilijikuta nimepata kimuhemuhe mtoto wa kike.
Ipo kwenye gari.
Twende nikaione, mtoto wa kike shauku ikanipanda.
Utaiona tu wala usiwe na wasi.
Lakini mpenzi huku mbali sana na mji?
Si utakuwa na usafiri wako ili kukurahisishia kwenda popote bila tatizo.
Mmh! Hapo sawa.
Baada ya kuzunguka eneo la uwanja wangu tulirudi kwenye gari. Kabla ya kuondoka alinionesha ramani ya nyumba yangu pia picha ya nyumba iliyokuwa imeishajengwa ambayo ilionekana nzuri pembeni kukiwa na gari la kifahari na bustani nzuri.
Basi nyumba yako ikiisha itakuwa kama hivi.
Muongo! nilishtuka kuambiwa nyumba kama ile nzuri itakuwa yangu.
Ikiwa tofauti na hii picha ikatae.
Na hili gari la kifahari lililopo pembeni ya nyumba nitakuwa nalo?
Lazima kila kitu kiwe kama kinavyoonekana kwenye picha.
Wawooo! Jamani asante mpenzi wangu.
Hizi ni rasharasha tu, mambo mazuri yanakuja.
Tulitoka kwenye kiwanja changu na kunirudisha nyumbani, kama kawaida aliniteremshia mbali na nyumbani. Nilipofika nilijikuta kila dakika nikitabasamu baada ya kukumbuka picha ya jumba la kifahari nililooneshwa na mpenzi wangu na kunihakikishia nyumba yangu ndivyo itakavyokuwa.
Nilijikuta nikiyaona maisha yangu yakibadilika na kunifanya niwe mtu mbele za watu. Nilikumbuka baadhi ya wanawake waliokuwa wakija kazini na kuwatetemekea kwa vile walikuwa na magari au wake wa watu wenye fedha nami nilijua tayari nimewafikia. Moyo uliniuma baada ya kujua sina haki ya asilimia mia moja hata nikiwa naye. Nilijiuliza kwa upendo alionionesha angekuwa wangu peke yangu sijui ingekuwaje! Naamini ningekuwa juu zaidi ya mawingu.
Siku iliyofuata ilikuwa Jumatatu, nilikwenda kazini kama kawaida. Da Suzy aliniuliza mchakato wangu na mzee Sambi. Nilimweleza yote sikumficha hata moja.
Unaona mdogo wangu ulitaka kuupiga teke mfuko wa fedha!
Lakini kumbuka si wangu wa kufa na kuzikana, Lakini ndiyo hivyo cha kuazima hakisitiri ------.
Mdogo wangu usifikirie visivyo kuhusu, ridhika na unachokipata. Amekuahidi mambo mengi na moja ameanza kulitekeleza. Ningekuwa ndiyo mimi mbona ningemzalia mtoto kwa vile mmepima na kuzijua afya zenu.
Mmh! Sawa, huwezi kuamini nimeanza kumpenda hata bila kujijua.
Chezea faranga wewe? Dada Suzy alitania.
Walaa, si kwa ajili hiyo bali ameonesha upendo wa dhati kwangu, ni mtu mwenye huruma, mkweli pia mwenye nia njema kwangu.
Basi mdogo wangu usiipoteze nafasi hiyo.
Dada sasa hivi mimi na mzee Sambi kama chanda na pete.
Hongera mdogo wangu, la muhimu mzalie mtoto ndicho kilio chake.
Atampata tu muda si mrefu tukianza kujirusha.
Ina maana hujampa? Dada Suzy alishtuka kusikia siku zote hizo sikuwa nimempa mwili wangu mzee Sambi.
Dada sikutaka kuwa naye kibiashara bali kujua hatima ya maisha yangu.
Kweli mdogo wangu una msimamo.
Tuliendelea na kazi, jioni kama kawaida mpenzi wangu alinipitia na kunirudisha nyumbani. Gari lilipofika makutano ya Barabara ya Changombe na Nyerere nilishangaa kuona likinyooka kufuata Barabara ya Nyerere badala ya kukata kushoto.
Sikutaka kumuuliza kwa kujua labda ameamua kupitia Barabara ya Mandela na kuingilia barabara ya kuelekea maghorofa ya Tazara. Lakini tulipofika njia panda ya Nyerere na Mandela alikata kulia badala ya kushoto kitu kilichonishtua.
Vilevile sikuhoji nilitaka nione mwisho wake utakuwa vipi. Gari lilielekea Buguruni, lakini tuliongoza hadi Tabata Dampo. Tulipinda kulia kufuata barabara ya kuelekea Tabata.
Tulipofika Bima alikata kulia kuelekea Tabata Kimanga nami nilikuwa kimya nimetulia nione ananipeleka wapi. Tulipofika Savana alikata kulia na kusimamisha gari nje ya nyumba moja yenye geti, akateremka na kufungua geti.
Aliporudi kwenye gari nilimuuliza.
Mpenzi wewe si una mke?
Mzee Sambi atajibu nini? Pale alipompeleka ni wapi? Kuyajua yote tukutane Jumamosi ijayo...