Mama yangu adui yangu -27-
ILIPOISHIA:
Wakati mzee Sambi akizungumza na mafundi, mama alinivuta pembeni na kuniuliza.
Unasema hii nyumba ni ya nani?
Yangu.
Wewe?
Ndiyo mama, huamini?
Muongo! Unataka kuniambia mzee Sambi ndiye aliyekujengea?
Ndiyo mama, mbona mambo mazuri yanakuja, muda si mrefu nitaacha kazi na kufungua duka langu ambalo lipo katika matengenezo. Mwezi wa kesho litajazwa vitu na kufanyiwa matangazo na mwezi ujao nitalifungua,
Mmh! Wapi?
Maeneo hayahaya ninayokaa.
Hongera.
Asante mama.
Wakati huo mzee Sambi alikuwa amemaliza kuzungumza na mafundi, alikuja tuliposimama na kusema:
Mama si ungezunguka kuliona jengo la mwanao?
SASA ENDELEA...
Nimeliona baba inatosha.
Hapana mama hebu twende ukakague nyumba ya mwanao.
Nilimshika mkono mama na kumzungusha sehemu zote za kiwanja changu na nyuma ya nyumba. Mama aliisifia nyumba yangu na kunifanya nifarijike moyoni.
Baada ya kumuonesha mama nyumba yangu, tulimrudisha mpaka Temeke kisha nilirudi nyumbani kwangu kupumzika. Moyoni nilifurahi mama yangu kuona jumba langu la kifahari, mshtuko aliouonesha nilijua ulitokana na kutoamini macho yake.
***
Pamoja na maisha na malezi mazuri kutoka kwa mpenzi wangu, lakini kuchelewa kupata mtoto kulinikosesha raha. Siku moja nikiwa kazini muda mwingi nilikuwa nimetawaliwa na mawazo kitu kilichomshtua da Suzy.
Mwaija mdogo wangu nakuona haupo sawa, nini kinakusibu?
Ni kweli.
Tatizo nini?
Sikumficha nilimweleza kila kitu kuhusiana na kuchelewa kumzalia mtoto mzee Sambi.
Sasa kama mlionekana hamna tatizo kipi kinachelewesha kupata mtoto?
Hapo ndipo ninapochanganyikiwa.
Mmeshatumia tiba mbadala?
Sasa kama huna tatizo tiba mbadala ya nini?
Mdogo wangu huenda ni chango, ukipata dawa za asili zitakusaidia.
Dada kama lingekuwa chango nisingepata ujauzito.
Mdogo wangu, lazima uangalie na jicho la tatu huenda una chango lisilouma na kusababisha mimba isiingie.
Mmh! Sijawahi kutumia dawa za asili tangu nizaliwe.
Ndiyo unatakiwa ukatumie uone kwani wengi walikuwa na matatizo kama yako leo hii wana watoto.
Hizo dawa nitazipata wapi?
Nitakupeleka kwa mtaalam.
Wapi?
Mbagala Maji Matitu.
Hiyo dawa itanisaidia kweli? niliingiwa na wasiwasi japokuwa nilimuamini sana da Suzy.
Dada nakwambia ndani ya wiki ukitumia kitu hicho.
Shoga nakuahidi nikishika mimba nitakupa milioni moja.
Wee iandae tu, nakuapia mwezi haukatika bila kunasa.
Basi dada naomba unipeleke, nilijikuta nikipata shauku ya kwenda kwa huyo mtaalam ili niweze kumzalia mtoto mzee Sambi.
Hakuna tatizo.
Tulikubaliana mwisho wa wiki anipeleke kwa huyo mganga ili anisaidie kupata mtoto. Maneno ya dada Suzy yalinipa faraja kwa asilimia ndogo.
Mwisho wa wiki nilimpitia dada Suzy na kukodi gari mpaka Mbagala Maji Matitu. Tulipofika tulikwenda moja kwa moja kwa mtaalam aliyekuwa akikaa ndani kidogo kupita kituo kidogo cha polisi cha Maji Matitu. Tulifika kwenye nyumba iliyokuwa imezungushiwa uzio wa makuti. Tuliingia ndani tulikuta watu kama sita wakiwa wamekaa kwenye mkeka na ndani kulikuwa na watu wawili.
Mganga alikuwa akitoka ndani alipotuona alitufuata na kutukaribisha. Alikuwa dada mmoja aliyekuwa na umri wa kawaida, pia hata mavazi yake yalikuwa ya kawaida kuonesha si mganga wa kizamani wa kuvaa kaniki na ngozi.
Alikuwa na umbile fupi na alivaa dela lililompendeza, mikononi mwake alikuwa amevaa pete za rangi ya fedha kila kidole na shingoni alikuwa na mkufu wa rangi ya fedha pia, kichwani alikuwa ameseti nywele, ukimuangalia haraka huwezi kuamini kama ni mganga.
Jamani karibuni, alitukaribisha kwa uchangamfu mkubwa.
Asante dada, tulijibu kwa pamoja.
Samahani jamani, vumilieni kidogo sina kazi kubwa nitawaiteni baada ya muda mfupi.
Hakuna tatizo.
Mganga alituachia na kuelekea ndani tukiwa tumekaa kwenye benchi lililokuwa pembeni ya mkeka.
Baada ya muda alituita ndani, tuliingia chumbani ambako ndiko kwenye kilinge, kulikuwa na vitu vyake vya kiganga na dawa. Baada ya sisi kuketi mganga alikaa mbele yetu kwenye kigoda na kutulia kwa muda kisha alisema:
Ndiyo, karibuni.
Asante, tulijibu kwa pamoja.
Mna tatizo gani?
Mwenzangu anahitaji mtoto.
Anahitaji vipi? aliuliza huku akitutazama kwa zamu.
Amekwenda hospitali na kuonekana hana tatizo lakini mtoto hapati, alisema da Suzy aliyeonekana mzoefu wa sehemu zile.
Na mwenzake naye alikwenda?
Ndiyo wote wapo sawa.
Basi tumuombe Mungu nina imani dawa nitakazompa zitamsaidia.
Halafu tulitaka kujua talaka yake ya mwanzo ilisababishwa na nini? da Suzy aliuliza kwa niaba yangu.
Hakuna tatizo, mganga alisema huku akinyanyuka na kuchukua lubega wa Kimasai na kujifunga kisha alivaa taji la Kimasai na chini alivaa viatu vya matairi na kushikilia mkuki, pembeni yake alilaza sime.
Nilijikuta nikiingiwa na hofu na kujiuliza alikuwa akitaka kufanya nini lakini dada Suzy hakuonesha wasiwasi wowote.
Baada ya kutulia kwenye kigoda chake alimwita mwanaume aliyekuwa nje ambaye alikuja kukaa pembeni yetu.
Jamani nina imani mwalimu atakayepanda kuna maneno yatakushindeni kuyaelewa. Huyu atawasaidia kuwaelewesheni.
Hakuna tatizo.
Baada ya kusema vile alichoma udi na kuuweka pembeni kisha akashika mkuki wake na kuuinamia kwa muda, akatulia kupandisha jini la Kimasai lililokuwa likiitwa Lukuki.
Heloo habari, alisema baada ya kupandisha, nilitulia tuli kuangalia kwani jambo lile kwangu lilikuwa ndiyo siku ya kwanza.
Nzuri, da Suzy aliitikia.
Alianza kwa kutusalimia kwa kutushika mikono na kugusanisha kichwa chake na kila aliyekuwemo mle ndani.
Alianza kuelezea matatizo yangu huku nikibahatisha mawili matatu yaliyonishinda mkalimani alinisaidia kunifafanulia.
Rafiki una matatizo makubwa sana, matatizo yako si ya leo hata najiuliza maswali mengi yaliyokosa majibu, kweli?
Ndiyo, ndiyo nilijibu.
Tatizo lako limeanza baada ya ndoa yako, ikiwa pamoja na kuharibikiwa mimba, mume kuharibikiwa maisha na kukosa kazi. Kuharibikiwa maisha na kila kitu kusimama ni kweli? mganga aliniuliza, yote aliyosema yalikuwa ni ya kweli alikuwa kama mtu anayejua maisha yangu.
Ni kweli, nilikubali.
Mumeo aliondoka na aliporudi alikupa talaka isiyo na maelezo ni kweli?
Ndiyo ila alisema mama anajua.
Tatizo lako nitakutibu wala sitaki kulichimba sana kwa vile nitazalisha visivyotakiwa, kingine unatafuta mtoto bila mafanikio japo huna tatizo lolote, ni kweli?
Kwa nini usinieleze mbaya wangu? nilitaka kujua.
Huna moyo huo wa kusikia vitu vizito vilivyo kuzunguka, ila nakuahidi kukutibu na kukuondoa vifungo ulivyofungwa.
Itaendelea Jumamosi, usikose.