[h=1]MAMA YANGU ADUI YANGU - 41-[/h]ILIPOISHIA
Naweza kupata mwanaume mwingine mambo yakawa yaleyale."
"Nakuhakikishia matatizo yaliyotokea hayatatokea tena."
"Kivipi?"
"Tatizo lililokuwepo nimeshalimaliza japokuwa ilikuwa kazi nzito."
"Unaweza kuniambia nani aliyefanya mchezo huu?"
"Wapo wawili, mmoja mke wa huyu mzee na mwingine nina imani naye ameachana na mchezo huu," mama Amina alinificha.
"Nani mama?"
"Hapana."
"Sasa nani?"
"Shida yako kupona au kumjua huyo mtu?"
"Vyote."
"Naomba basi nisikilize, acha kuchimbua vilivyopita. Mshukuru Mungu kukuponya."
Sikutaka kumchimbua sana na kujikuta mawazo yangu nikihamishia kwa mama. Lakini wazo hilo nilipingana nalo kutokana jinsi mama alivyopigania maisha yangu.
SASA ENDELEA...
NILIJIULIZA atakuwa nani au dada mkubwa niliyemchukulia mpenzi wake? Lakini kama dada angekuwa amefanya vile alikuwa ananionea kwani tulikubaliana.
Hata wazo hilo bado sikukubaliana nalo kutokana na matatizo ya awali kunitokea nikiwa ndani ya ndoa yangu. Swali likabakia ni nani aliyenifanyia vile, kwa nini mama Amina hakuniambia kama alivyonieleza ya mke wa mzee Sambi?
Swali lile liliniumiza kichwa, sikutaka kumuuliza sana kwani ningemuudhi na kuonesha sina adabu, kama makosa niliyofanya mwanzo. Wasiwasi wangu ulikuwa ni kutokea tatizo lingine na mama Amina kugoma kunisaidia kwa vile si msikivu.
Mama Amina alinipatia dawa za kuoga na makombe ya kunywa. Baada ya zoezi la mwisho alinieleza nifanye chochote bila tatizo. Nilirudi zangu nyumbani kichwa kikiwa kizito huku nikijiuliza kwa nini mtu huyo hatakiwi kutajwa, ni nani?
Nilipanda gari la Mbande - Tandika na kuteremkia Tandika. Kwa vile kulikuwa na njia ya mkato sikutaka kupanda usafiri wowote, nilikatiza kwenda nyumbani.
Nikiwa navuka Barabara ya Devis Kona, nilisikia jina langu likiitwa.
"Mwaija."
Sikuitika mpaka nilipogeuka na kumuona aliyekuwa akiniita. Alikuwa kaka mmoja tuliyekuwa tukikaa mtaa mmoja siku za nyuma, alikuwa kwenye gari.
"Abee," niliitika na kugeuka kumsikiliza.
"Unatoka wapi?"
"Mbagala."
"Kwema?"
"Kwema."
"Kwa vile naelekea maeneo ya kwenu naomba nikusogeze."
"Acha tu nitafika."
"Hapana Mwaija nafika karibu kabisa na kwenu, ingia twende."
Sikutaka kuwa mbishi, nilifungua mlango wa gari na kuingia. Akaondoa gari, tulipokaribia Transfoma, alianza kunisemesha.
"Leo nina bahati ya kuonana na wewe."
"Bahati ipi Juma?" nilimuuliza huku nikimtazama.
"Kwanza pole."
"Ahsante," nilimjibu kwa mkato.
"Nimekufuatilia muda mrefu."
"Kuhusu nini?" nilimkata kauli.
"Subiri basi."
"Haya endelea."
"Mwaija kama usingeolewa na Beka ningekuoa mimi."
"Kivipi?"
"Nilikupenda muda mrefu, huwezi kuamini kila hatua ya maisha yako niliifuatilia mpaka mlipoachana na Beka. Wakati najiandaa kuja kwenu nilipata safari ya ghafla.
"Niliporudi nilikuta unaumwa sana, bado niliendelea kukufuatilia. Leo hii ninaweza kusema hii ni nafasi yangu."
"Nafasi gani?"
"Ya kutuma maombi ya kukuoa."
"Juma naomba sasa hivi suala la mapenzi tuachane nalo."
"Kwa sababu gani?"
"Nahitaji kupumzika, mapenzi yamesababisha nichungulie kaburi."
"Bila matatizo hayo ungekuwa tayari?"
"Ndiyo kwa vile heshima ya mwanamke ni ndoa."
"Kwa nini usinipe nafasi hiyo?"
"Labda baadaye, lakini sasa hivi nahitaji mapumziko ya muda mrefu, kwa sasa nayachukia mapenzi kuliko kitu chochote."
"Kwa hiyo utakuwa tayari lini?"
"Niache kwanza."
Juma alinifikisha nyumbani na kuniacha huku akiniomba awe sehemu ya mawazo yangu ya kila siku. Nilimkubalia ili aniache nipumzike kwa vile bado mbaya wangu aliendelea kuwa siri iliyonitesa sana.
Baada ya kufika nyumbani, niliendelea kutumia dawa nilizopewa na mama Amina huku ombi la Juma likiwa halipo akilini mwangu.
Lakini kumbe kwa mwenzangu ilikuwa tofauti, aliendelea kunifuatilia kwa karibu. Baada ya wiki mbili kukatika, mama aliniita na kunipa taarifa ya kujitokeza mtu wa kutaka kunioa ambaye ni Juma.
"Mama naomba suala hilo tuachane nalo kwa sasa."
"Hapana mwanangu nakuomba ukubaliane nalo."
"Mama nimechoka, kila siku miye tu."
"Kwa nini unasema hivyo?"
"Mapenzi yamekuwa mateso na kutishia uhai wangu kila siku."
"Sasa hivi hayatatokea tena."
"Kwa nini unasema hivyo?"
"Mimi najua, naomba unisikilize mimi mama yako."
"Mmh! Sawa mama kwa vile nakupenda sana pia umenipigania maisha yangu kwa nguvu zako zote nimekubali."
"Nimefurahi mwanangu kunisikiliza mama yako."
Nilikubaliana na mama kuhusu kuolewa, huku nikishangaa mama yangu kuwa mbele katika kukubali jambo lile tofauti na siku za nyuma.
Majibu yalirudi kuwa nimekubali, mipango ya ndoa ikaanza mara moja. Taarifa ile nilimweleza mama Amina na dada Suzy na wote wakaniunga mkono. Namshukuru Mungu nilipata ushirikiano wa hali na mali kwa familia, muda wote mpaka wakati wa ndoa yangu.
Niliolewa na Juma, mfanyabiashara wa maduka ya nguo na vyombo vya umeme Kariakoo aliyekuwa amejenga Kibamba. Namshukuru Mungu baada ya ndoa nilimuweka wazi mume wangu juu ya maisha yangu niliyopitia na umuhimu na mama Amina kwangu.
Hakuwa na tatizo, alinipa ushirikiano ikiwa ni pamoja na kumualika mama Amina kwetu japokuwa kwenye harusi yangu alihudhuria na kunipa ushirikiano mkubwa sana.
Kuna kitu kimoja kilinifurahisha, mama Amina japo alikuwa mganga wa jadi naye alikuwa wamo! Akiamua kujilipua na pamba huwezi kuamini kama ni yeye anayevaa kaniki wakati wa kutibu.
Siku ya harusi nilimsahau alivyolipuka na ‘migoldi' iliyomchafua kichwani mpaka mikononi. Alikuwa mganga wa kileo anayekwenda na wakati.
Namshukuru Mungu maisha ya ndoa yalikwenda vizuri, baada ya muda nilishika ujauzito. Mama Amina aliufunga ili nisiupoteze tena.
Mungu alijalia nikajifungua salama mtoto wa kike mwenye afya njema. Kwa kweli maisha niliyoishi na mume wangu yalinikumbusha mbali huku nikiwa na wasiwasi juu ya kutokea yaliyotokea mwanzo.
Nilikuwa na furaha na malezi mazuri ya mume wangu, familia yangu kwa jumla ilikuwa karibu nami. Lakini nilipokumbuka maisha ya zamani na misukosuko, moyo ulikosa raha.
Nakumbuka vizuri siku moja nikiwa Kariakoo, karibu na Kituo cha Msimbazi niliguswa bega na mtu. Nilipogeuka nilikutana na mtalaka wangu Beka.
"Mwaija," aliniita akionesha kunishangaa.
"Abee."
Japokuwa nilimpenda kuliko mwanaume yeyote lakini kitendo alichonifanyia sikumchangamkia, nilimuona mtu wa kawaida.
"Za siku?"
"Nzuri."
"Umeolewa?" aliniuliza baada ya kuona pete ya ndoa kidoleni.
"Uliponiacha ulitegemea sitaolewa tena?" nilijikuta nikizungumza huku nimebinua midomo japokuwa sikukipenda kitu kile katika maisha yangu.
"Mwaija bila vile ningebakia jina," Beka alisema kwa sauti ya majonzi.
"Si nilikuuliza nani anataka kukubakiza jina hukuniambia ikabaki siri yako na familia yako huku ukitaka kunigombanisha na mama yangu?"
"Samahani tutafute sehemu nzuri, tuzungumze vizuri."
Je, Beka anataka kumwambia nini? Usikose kufuatilia Jumapili ijayo......