Mama Yangu Adui Yangu - 49-
ILIPOISHIA;
"Mmh! Yaani baba yenu alipolala ha..ha...ku...amka tena."
Mama alianza kulia kilio cha kwikwi kitu kilichofanya wote tulie kilio cha kimya kwa kutokwa machozi huku tukizidi kumuonea huruma mama yetu.
Ilibidi mama Amina aanze kazi ya kumbembeleza mama aliyekuwa akilia.
Nilipowaangalia dada zangu kila mmoja alikuwa akilia.
Kwa kweli ilikuwa simulizi yenye kuumiza na kupasua mioyo bila ganzi. Baada ya mama kunyamaza aliendelea kuzungumza kwa sauti ya kilio na kuzidi kuniumiza.
"Kwa kweli sikuelewa sababu ya kifo cha baba yenu, nilijiuliza labda dawa niliyompa kunywa na kama ni ile nilikosea sehemu gani. Niliumia mara mbili baada ya kuhangaika kote kumbe nilitafuta kumuua mume wangu."
Kufikia hapo mama akaanza kulia tena.
Nilishindwa kujizuia nilijikuta nikisema kwa sauti bila kujielewa:
"Mama hujamuua baba, ulifanya kwa ajili yetu lakini bahati mbaya yakatokea yaliyotokea."
"Hapana wanangu bila mimi msingekuwa yatima."
SASA ENDELEA...
"Si kweli, wangapi mayatima si kwa tukio kama lako?" nilihoji.
"Lakini bila mimi baba yenu asingekufa."
"Angekufa kwa kitu kingine, mama toka ulipoanza kuzungumza sijaona sehemu uliyochangia kifo cha baba. Mama tunakuomba uondoe wazo hilo," dada mkubwa alisema.
"Basi wanangu baada ya msiba tulifanya kila kitu na kumlaza baba yenu katika nyumba yake ya milele. Nilikonda kwa mawazo, lakini ninyi ndiyo mlionifanya nisimame imara ili kuhakikisha nawasomesha na hamtetereki kimaisha.
"Sijui niseme nini, lakini baada ya kifo cha baba yenu vitu vingi vilijulikana. Alikuwa na gari na nyumba pia malipo yote ya kazini kwake nilipata.
Baada ya kupata vitu vyote hivyo nilimalizia nyumba ya Mwaija na kuipangisha. Naweza kusema nilifanya kosa kukueleza Mwaija baba yako alikuachia nyumba kubwa.
"Hilo naomba nikiri nilifanya kosa, nimekula fedha yako bila kukushirikisha kwa miaka yote hiyo. Lakini leo nitakukabidhi kila kitu.
"Kupitia mali alizoacha baba yenu niliweza kuwasomesha wote ila sikutaka msome sana kwa vile mngeondoka na kuniacha peke yangu. Hapo ndipo nilipoanza kufanya makosa makubwa.
"Baada ya Zamda na Rehema kuolewa niliona nyumba inapwaya na kujikuta nikipata wazo la kuwarudisha nyumbani, hapo ndipo nilipokwenda kwa mtaalamu na kuzisambaratisha ndoa zenu na ninyi kurudi nyumbani bila kujua mimi ndiye mbaya wenu. Niliweza kuwafanya kuzichukia ndoa kitu kilichokuwa furaha yangu.
"Nilifanya hivyo kwa Mwaija ambaye nilikuwa nampenda sana, wewe ndiyo sikutaka kabisa uondoke nyumbani. Yote yaliyokutokea niliyafanya mimi mama yako.
"Wanangu nachukua nafasi hii kuwaombeni radhi kwa yote niliyowafanyia pia namuomba Mwenyezi Mungu anisamehe kwa kila baya nililowafanyia. Sijui bila mama Amina, wanangu wangeendelea kuishi maisha gani.
"Mwanangu najua nimewaumiza bila ya ninyi kujua, naomba mnisamehe nipo chini ya miguu yenu."
Mama alisema huku akinyanyuka kitini ili apige magoti. Tulinyanyuka wote na kumuwahi kabla hajapiga magoti na kumwambia tumemsamehe.
Baada ya zoezi lile, mama Amina alizungumza:
"Nina imani mmemsikia vizuri mama yenu, siku zote mtu akigundua kosa lake na kutubu hata Mungu umsamehe. Mama yenu kagundua makosa yake na leo kayasema yote bila kuacha kitu.
"Kwa vile mmemsamehe nawaomba muishi kama zamani, mpendeni mama yenu. Alifanya vile kwa mapenzi mazito kwa wanaye lakini akawa anaharibu.
"Namshukuru Mungu kwa upande wangu nimemaliza kazi yangu nina imani kila mmoja ameona mabadiliko," mama Amina alituambia.
"Ni kweli," tulijibu kwa pamoja.
"Mimi nafikiri sina cha zaidi, nashukuru tumemaliza salama acha nikimbie," mama Amina alitaka kutuaga.
"Mama Amina tunashukuru kwa kila ulilotufanyia, nina imani si kwa uwezo wetu bali ni Mungu ndiye aliyetuongoza kukujua wewe na kututoa kwenye kiza kizito.
"Kwa upande wa mama bado tunampenda sana tena sana. Alichotueleza hakitapunguza upendo wetu kwake. Tunampenda mama leo, kesho kwa vile kilichofanyika ni funzo si kwake hata sisi tutazaa na kutorudia makosa.
"Mama ondoa unyonge lililopita limepita, tumshukuru Mungu kwa kulifungua mapema kabla hujafa. Inawezekana tukio hili lilikuwa likitukumbusha kumrudia Mungu wetu.
"Namalizia kumshukuru tena mama Amina wewe si mganga tu bali ni sehemu ya familia yetu. Sisi hatuna cha kukulipa bali Mungu ndiye mwenye uwezo huo.
Wadogo zangu hatuna budi kumtunza mama yetu kwa vile amebakia kama jicho letu. Tusimuwekee kinyogo bali tumpende na kumtunza," dada mkubwa alisema kwa hisia kali mpaka machozi yakamtoka.
"Mama nakupenda nitaendelea kukupenda," dada Rehema alisema maneno mafupi.
"Mama nataka kukuambia mapenzi yangu kwako ni makubwa sana, nataka kukueleza chanzo cha matatizo yangu niliyajua muda mrefu toka nikiwa na Beka.
"Lakini bado sikuwa tayari kukuchukia mama yangu, niliamini unatupenda japokuwa sikupenda maisha tuliyokuwa tukiishi, nilijitahidi niwe tofauti na dada zangu.
"Nilikuwa na bahati iliyoishia na matatizo, hata baada ya kugundua sababu ya matatizo yangu bado moyo haukukubali mama unaweza kuwa adui yetu.
"Nimehangaika kuupata ukweli bila mafanikio, na nilipoupata bado niliendelea kukupenda mama yangu, nilitamani kukueleza lakini niliogopa.
"Inawezekana wote hamkujua kikao hiki kimeitishwaje, nataka kuwaeleza, mimi ndiye niliyemfuata mama Amina na kumuomba aitishe kikao hiki ili kuufungua moyo wa mama uliokuwa na mzigo mzito ila sijui kwa dada zangu kwa vile niliyajua haya mapema.
"Mama inawezekana ukaona nimekuvunjia heshima kwa kukulazimisha kuyasema mambo mazito kwetu. Mama naomba unisamehe nilifanya hivyo kwa ajili ya kukuweka huru.
"Nilijua unaumia na kuendelea kuteketea kama mshumaa, huwezi kujua hali uliyokuwa nayo ilitutesa sana wanao kiasi gani. Lakini leo nataka kukuambia toka moyoni kuwa tumezaliwa upya," nami nilimalizia.
"Asanteni wanangu, narudia kusema namshukuru Mungu kunipa watoto wenye mapenzi ya dhati na mama yenu. Nimejifunza kitu nina imani kila kitu ni uweza wa Mungu.
"Mama Amina nashukuru sana mdogo wangu, Mungu atakulipia, narudia wanangu mnisamehe sana."
"Tumekusamehe mama," tulisema kwa pamoja.
***
Kikao kiliisha salama kwa watoto wote kuiswafi mioyo yetu kwa mama. Kwa upande wangu niliutua mzigo mzito ulionielemea moyoni mwangu na kuwa huru huku nikiendelea kumshukuru Mungu.
Furaha ilirudi katika nyumba yetu, dada yangu aliolewa harusi kubwa na mwingine anaendelea na kazi huku akiwa na bwana ambaye alimuahidi kumuoa.
Namalizia kwa kumshukuru mama Amina kwa msaada wake wa hali na mali kuhakikisha anapigania afya yangu mpaka leo hii ninayotoa ushuhuda huu nina afya njema na watoto watatu, wawili wa kike na mmoja wa kiume.
Dada zangu wote wana mtoto mmoja mmoja.
Pia namshukuru sana mwandishi wa mkasa huu kwa kukubali kupoteza muda wake kuandika mkasa mzito kama huu. Mungu atamlipia kwa kazi yake ya kujituma bila kuchoka.
Mwisho kabisa nawashukuru wasomaji wote kwa kupoteza muda wao kufuatilia simulizi yangu mpaka leo ambapo nahitimisha mkasa huu, Mungu atawalipa pia nina imani kuna kitu mmejifunza hasa wazazi nina imani mmeona madhara ya ushirikina.
Wapeni uhuru watoto wenu waishi maisha yao hata kama mnawapenda sana. Naomba kwa leo niishie hapa Mungu awabariki, ahsanteni.
Kwa kunifuatilia hadithi yangu na kuacha shughuli zenu nawapendeni nyote .
MWISHO!