Malenga wetu na sakata la Richmond | JamiiForums | The Home of Great Thinkers

Dismiss Notice
You are browsing this site as a guest. It takes 2 minutes to CREATE AN ACCOUNT and less than 1 minute to LOGIN

Malenga wetu na sakata la Richmond

Discussion in 'Habari na Hoja mchanganyiko' started by KIM KARDASH, Dec 6, 2011.

 1. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #1
  Dec 6, 2011
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Nova Kambota

  Kalamu yangu nashika, shairi nakutungia

  Kamanda umeongea, kiwingu umeondoa
  Hukutaka kusinzia,makosa kuyarudia
  Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

  Mwananchi nimesoma, la jana nilinunua
  Machoya yakatuama, dukuduku umetoa
  Uliyosema Dodoma, Kwakweli yanavutia
  Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

  Richmond kupasua, mapema uligundua
  Kikwete ukamwambia, mkataba kuondoa
  Rais akakataa, nini alitegemea?
  Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

  Nape akashikilia, lile asilolijua
  Mikoani kaambaa, uzushi kang'ang'ania
  Jinalo kulichafua, wewe ukavumilia
  Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

  Mapema nilitabiri, falsafa nikapinga
  Magamba sikukariri, kuvuana sikuunga
  Ukweli niliukiri, mantiki iso kunga
  Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa

  Beti sita nakomea, kalamu naweka chini
  Mengi nimeongelea, soma tena kwa makini
  Yatazidi kutokea,kusini kaskazini
  Jibu umetupatia, viva kamanda Lowassa.

  Nkwazi Mhango

  Kambota nakushukuru, kwani umevua gamba,
  Kumbuka umekufuru, matapishi utaramba,
  Siku kweli ikizuru, utajiona mshamba,
  Shairi lako la hovyo, kwani wasifu fisadi.

  Kwa wachumiao tumbo, Lowassa mtu shujaa,
  Wafikirio kwa matumbo, Lowassa tiba ya njaa,
  Watapigana vikumbo, kwenda kwake ganga njaa,
  Shairi lako la hovyo, kwani wasifu fisadi.

  Hebu rudi darasani, jifunze misamiati,
  Udhaifu tabaini, uijue tofauti,
  Kamanda na marhuni, vina kubwa tofauti,
  Shairi lako la hovyo, wamsifia fisadi.

  Kama Lowassa Kamanda, basi ni wa mafisadi,
  Kwa hili sitamponda, kulhali ni fisadi,
  Kwake nilichokipenda, kukubali yu fisadi,
  Kamueleza Kikwete, kuwa sote mafisadi.

  Kambota nakushangaa, sijaona kicho chako,
  Tafuta dawa ya njaa, si kuvua nguo zako,
  Kesho kaka ni balaa, mafisadi si wenzako,
  watakutumia sana, utatupwa ja nepi.

  Kambota umenikuna, kufichua sura yako,
  Ila la maana huna, kwa huo mradi wako,
  Wamtumikia ngwena, kitoweo mwisho wako,
  Uliza waliowini, kihalali si jinai.

  Uchangu kimaadili, umegeuka mradi,
  Wachovu waona dili, kutumiwa na fisadi,
  Watupia senti mbili, kusafisha mafisadi,
  Mwisho wa siku walia, warambapo matapishi.

  Kaditamati kituo, mbele sitaendelea,
  Onyo wapiga chapuo, fisadi kunyenyekea,
  Ipo siku mlo huo, puani utatokea,
  Kambota u mmojawapo,wapi utaficha sura?


  Nova Kambota

  Lowassa Ni Msafi, Hahitaji Kusafishwa ( Jibu)
  Mjengwa naomba tena, jukwaani nirejee
  Niliyoandika jana, napenda niyatetee
  Mkuranga kimanzichana, Lowassa aendelee
  Nkwazi hujaelewa, umefakamia mada

  Mhango kajichanganya, kujibu asichojua
  Kauropoka unyanya, pasipo kulitambua
  Si hasi wala si chanya, Nkwazi kasimamia
  Mhango wajipotosha, kujibu usichojua

  Lowassa ni mtu safi, tegua kitendawili
  Angelikuwa ni ni fisi, mahakama mhimili
  Hojazo ni mufilisi, wewe ndumilakuwili
  Nkwazi rudi shuleni, kaisome CCM

  Mhango wanishangaza, ukweli kutofahamu
  Waonekana kilaza, rejea Dar es salaamu
  Kwa hoja ntakuchakaza, wewe mwana wa Adamu
  CCM huijui, fitina wamezoea

  Lowassa ni kiongozi, hili unalitambua
  Achana na upuuzi, ule walomzushia
  Usijifanye dandizi, kudandia usojua
  Nkwazi mwana Mhango, uliza nakusikia

  Beti sita natuama, nimefikia tamati
  Lowassa mtu wa maana, hodari wa mikakati
  Nkwazi soma kwa sana, tambua hizi nyakati
  Lowassa ni mtu safi, hahitaji kusafishwa.


  Nkwazi Mhango

  Kambota achaujuha, CCM siyo fani,
  Kijana acha mzaha,kunambia sina fani,
  Sema yenyemkutadha, siyo kuleta uhuni,
  Kama kakaumehongwa, tulia kula kizani

  Najua uko kazini,wataka akusikie
  Lowassa ni yakodini, lazima umsifie,
  Ila jua u kizani,ni heri ujililie,
  Kambotaunachekesha, noisome CCM!

  Sikujua tokamwanzo, ninakinzana na zoba,
  Mwenye mgandomawazo, aso kifani mjuba,
  Sikujua hamnazo,nilomvisha kikuba
  Kambota achaujuha, soma maoni ya watu.

  Wasema nirudi Dar,nipambane na mgao!
  Nani amekuhadaa,huyo kakupiga bao
  Lowassa kaka balaa,ndiye chanzo cha mgao,
  Kambota hebukomaa, mambo ya kitoto acha.

  Mie kwako nimwalimu, hilo kaka walijua,
  Kaiulize kaumu,najua wanitambua,
  Nii mwalimu wawalimu, Bongo nzima watambua,
  Kambota shikaadabu, kiatu changu huvai.

  Hata utetee vipi,Lowassa bado fisadi,
  Wenye mawazomafupi, humuona maridadi,
  Awatumia ja chupi,waona wanafaidi,
  Kambota achautani, haramu haishibishi.

  Wino umeniishia,mbele sitaendelea,
  Karima akijalia,hoja itaendelea,
  Muhimu toto sikia,adabu upate tia,
  Lowassa atakuponza,ukweli ukidhihiri.  Nova Kambota  MHANGO ACHA UJUHA

  Mhango acha ujuha, heshima wajishushia
  Wasababisha karaha,kuimba kuitikia
  Wajiletea jeraha,moyoni hutalilia?
  Kwa hili umechemsha, zumbukuku nakuita.

  Lowassa wamtamka, uzushi wamtungia
  Hoja zako za kubaka, maneno unadandia
  Hakika u kibaraka, leo nakupasulia
  Ikulu ya kutumia, Kikwete swahiba wako.

  Huijui Richmond, kwanini unaropoka
  Tena wajifanya fundi, huku unaweweseka
  Punguza wako upimbi, punguza kubwekabweka
  Nkwazi acha ujinga, heshima wajishushia.

  Kanada umetopea, hupakumbuki nyumbani?
  Halafu wajitetea, uhesabiwe kundini
  Tatizo lako sikia, upeo wa kiganjani
  Miaka umenizidi, Kwa hoja usithubutu.

  Wamtukana Lowassa, nini amekukosea?
  Umegeuzwa galasa, uzushi kufakamia
  Kwani kamanda Lowassa, nani alimteua?
  Nkwazi wewe mjinga, fumbo hutaling'amua.

  Hapa mwisho nagotea, tamati nimefikia
  Nkwazi nakushangaa, nini unajivunia?
  Siri zako nafichua, Ikulu yakutumia
  Nkwazi nipe jawabu, unalipwa bei gani?


  Nkwazi Mhango

  Kabota nitakubota, hata kama kiroboto,
  Yote unayolumbata, si chochote ni kokoto,
  Huna mpata na kata, nijuacho u limpyoto,
  Kabota acha unywanywa, naona unatumiwa.

  Lowassa bado fisadi, hata mmpambe vipi,
  Kambota wewe hasidi, watumika kama nepi,
  wajiona wafaidi, kumbe kesho ni makapi,
  Kabota acha unywanywa, Lowassa akutumia.

  Wauliza nalipwaje, Nani huyo anilipe?
  Sijalipwa hata punje, mie mwezio si kupe,
  Shurti nijikunje, niishi si kwa mahepe,
  Kabota acha ushamba, Lowassa atakuponza.

  Naijua Richmond, Richmond ni Lowassa,
  Kikwete ni Richmond, Richmond ni mkasa,
  Kambota nawe ni bundi, Richmond takutesa,
  Japo wachumia tumbo, Kambota acha ujuha.

  Utajaliwa ja ng'oda, Siku yako ikifika
  Ja ng'oda utakonda, Lowassa akikutoka
  Ukuuishie ukuda, ubaki kulalamika
  Fisadi hana rafiki, Jifunze kwake Lowassa

  Mambo yalipombana, Kikwete kaumuumbua,
  Hawa marafiki sana, Itakuwa wewe bua,
  Leo sana wajiona, ujinga wakusumbua,
  Kambota acha ujuha, Lowassa hasafishiki.

  Huna mpaka na nune, Kambota wala jaani,
  Leo wewe ujivune, kumbe wenda majilini,
  Sema sana utukane, itafika arobaini,
  Kambota acha ujuha, Lowassa hasafishiki.

  Kaditamati natua, mbele sitaendelea,
  Kwa hapa naomba dua, wadudi anisikia,
  Ninamuomba mulua, Kambota aone jua,
  Kambota chumia tumbo, hebu tumia ubongo.


  ROYALS
  Ninakuunga mkono, wewe mr kambota
  Tena kwa maandamano, ya Dar hadi Msata
  Ulosema ni manono, kama ya nyama ya bata
  Laigwenan msafi, wao walimchafua.  Nova Kambota

  MHANGO WAJUA NINI?

  Nkwazi nakuuliza, nini kimekuingia?
  Mwenyewe wajishangaza, kubisha usiyojua
  Kwa hoja nakuchakaza, hili unalitambua?
  Mhango wajua nini? Zaidi ya kutumiwa?

  Nakuuliza hasidi, nijibu nikulipue
  Nitoe na ushahidi, watu wote wakujue
  Watumiwa kama pedi, kanusha nikuumbue
  Nyumba unayoringia, mimi ni mjenzi wake.

  Lowassa mchapakazi, Leigwani maridadi
  Tena yu baba mlezi, wa viwango na spidi
  Muda wake hapotezi, Kulumbana nawe kidi
  Nkwazi unachekesha kumtuhumu Lowassa.

  Unalipwa bei gani, kwanini jibu hunipi?
  Nimekutoa manani, wamung'unywa kama pipi
  Unazungumza nini?, msimamo wako upi?
  Nkwazi wanichekesha, kupungukiwa na hoja

  Richmond mali ya mtu, Kikwete namtangaza
  Punguza roho ya kutu, uongo kuutandaza
  Wewe ni kidudu mtu, kwa hoja nakuchakaza
  Mimi naitwa Kambota, "Kabota" waweweseka

  Kwa hoja nakuadhibu, tamati nimefikia
  Nakufundisha adabu, Zinduka umesinzia
  Kwa hoja wewe ni bubu, leo nakupasulia
  Nkwazi wajua nini? zaidi ya kutumiwa?


  JE KUNA MTU ANAWEZA KUINGILIA KATI MALUMBANO HAYA KWA STYLE YA MASHAIRI KAMA HAWA,NA JE NANI ANATUMIWA KATI YA HAWA MALENGA WETU??????????????????????

   
 2. k

  kilolambwani JF-Expert Member

  #2
  Dec 6, 2011
  Joined: Dec 3, 2010
  Messages: 395
  Likes Received: 1
  Trophy Points: 0
  lowasa kukwepa hili hawezi

  kilola mwana wa pwani, ebu nishike kalamu,
  niingie ulingoni, huku nikiwasalimu,
  nami nitoe maoni, kwenye huu udhalimu,
  lowasa hapa hatoki, kukwepa hili hawezi.

  Lowasa tatizo lake, nae alijiingiza,
  yeye kwa kauli zake, wizara aliagiza,
  na vile vimemo vyake, uzito viliongeza,
  lowasa hapa hatoki, kukwepa hili hawezi.

  Alipoona mkulu, ushauri hautaki,
  yeye angetunusuru, na kututendea haki,
  sheria angenukulu, na kanuni kuhakiki,
  lowasa hapa hatoki, kukwepa hili hawezi.

  Lakini akasahau, manunuzi nchi hii,
  hayahitaji nahau, yanahitaji utii,
  sheria kaidharau, kaingiza usanii,
  lowasa hapa hatoki, kukwepa hili hawezi.

  Wangefuata sheria, halisi ya manunuzi,
  isingeleta udhia, na hivyo vigugumizi,
  maana tungetambua, ni taratibu za kazi,
  lowasa hapa hatoki, kukwepa hili hawezi.

  Kufuata mizania, hupunguza matumizi,
  na gharama halisia, sisi tungezimaizi,
  thamani ya kulipia, ingefanana na kazi,
  lowasa hapa hatoki kukwepa hili hawezi.

  Sasa huo ushauri, wa makatibu wakuu,
  mbona kaufanya siri, hakutaka kunukuu,
  angeuweka dhahiri, ingekuwa ni nafuu,
  lowasa hapa hatoki, kukwepa hili hawezi.

  Lowasa mtu mahili, uamuzi atoapo,
  lakini kwa jambo hili, amenasa kama popo,
  lazima alikubali, asikwepe kwa viapo,
  lowasa hapa hatoki, kukwepa hili hawezi.
   
 3. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #3
  Dec 6, 2011
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Ahh mie yangu macho mashairi siyawezi,ngoja tusubiri waje wenye fani,wapi nkwazi,wapi kambota??kazi kwenu,natahakikisha hii kitu inaendelea mpaka tunampata rais mpya 2015 na kuendelea.....
   
 4. Barubaru

  Barubaru JF-Expert Member

  #4
  Dec 6, 2011
  Joined: Apr 6, 2009
  Messages: 7,162
  Likes Received: 26
  Trophy Points: 0
  Nitapita baadae.
   
 5. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #5
  Dec 6, 2011
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Karibu tujumuike kamanda!
   
 6. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #6
  Dec 7, 2011
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  [h=2]Mbona malenga wetu wako kimya siku hizi mbili au mpaka lowassa avunje ukimya?[/h]
   
 7. Mwita Maranya

  Mwita Maranya JF-Expert Member

  #7
  Dec 7, 2011
  Joined: Jul 1, 2008
  Messages: 10,569
  Likes Received: 104
  Trophy Points: 145
  Mashairi yametulia haya. Inanikumbusha kipindi cha malenga wetu miaka ile tukiwa na redio ya taifa pekee.

  Tangu ziingie hizi FM stations hata sijui RTD niliipotezea wapi!
   
 8. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #8
  Dec 7, 2011
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Yah!kweli kabisa,enzi za kina sauti ya kiza ambae alikua akiijiita hivyo kutokana na ulemavu wa macho aliokuwa nao!jamaa alikua kiboko ya njia....
   
 9. Ndahani

  Ndahani JF-Expert Member

  #9
  Dec 7, 2011
  Joined: Jun 3, 2008
  Messages: 14,314
  Likes Received: 1,784
  Trophy Points: 280
  Ooooh I am rejuvinated again...this was my passion when I was in primary school! Mashairi yana radha yake bwana.
   
 10. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #10
  Dec 7, 2011
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Tupe mistari basi kamanda....mbona unabana?
   
 11. bucho

  bucho JF-Expert Member

  #11
  Dec 7, 2011
  Joined: Jul 13, 2010
  Messages: 4,541
  Likes Received: 424
  Trophy Points: 180
  hakyanani mmenikumbusha mbali sana . nilikuwa sipendi hiko kipindi kabisa , nilikuwa nikitoka shule mchana huyo jamaaa alikuwa ananipa kichefu chefu. ilikuwa kila nyumba nayopita namskia huyo jamaaa akisoma mashairi pamoja na harufu ya ugali unaopikwa kila nyumba kweli ilikuwa inanikata stimu sana.
   
 12. G

  Gagnija JF-Expert Member

  #12
  Dec 7, 2011
  Joined: Apr 28, 2006
  Messages: 6,288
  Likes Received: 597
  Trophy Points: 280
  Sofia Simba amewahi kutamka kuwa hakuna mwanaume kama Lowasa. Atawaoa wengi huyu.
   
 13. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #13
  Dec 7, 2011
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Bora wewe wengine unakuta jiko limenuna halafu malenga wetu ndio anaunguruma redioni!
   
 14. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #14
  Dec 7, 2011
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  wapambe wake wanamwita mwanaume wao wa shoka eti!
   
 15. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #15
  Dec 13, 2011
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Yote kwa yote Lowassa hawezi kusafishwa kwa mashairi bali kwa kusimama hadharani mchana kweupe na kutueleza anachokijua na asichokijua kuhusu richmond,tunateseka sana na gharama za umeme hatutamsamehe alieileta richmond.
   
 16. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #16
  Dec 17, 2011
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Malenga wetu mpo?????mbona kimya kimezidi????????????????????
   
 17. K

  KIM KARDASH JF-Expert Member

  #17
  Feb 16, 2012
  Joined: Sep 21, 2011
  Messages: 5,083
  Likes Received: 60
  Trophy Points: 145
  Du watu wanavipaji jamani,wako wapi hawa malenga wetu?
   
Loading...