Rais Jakaya Kikwete, amewataka wafanyakazi nchini, kukataa kutumika katika miradi ya mafisadi na vigogo wa rushwa ili kuwafanya vigogo hao washindwe kutimiza malengo yao.
Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Ikulu jijini Dar es Salaam, Mkurugenzi wa Mawasiliano wa Ikulu, Bw. Salva Rweyemamu alisema badala yake Rais amewataka wafanyakazi kuwa mstari wa mbele katika kuwafichua vigogo hao bila woga.
Alisema iwapo wafanyakazi watagoma kutumikishwa katika `madili` ya kifisadi na rushwa, itakuwa vigumu kwa vinara wa mambo hayo kufanikisha matendo hayo maovu.
Katika kuwapa moyo wafanyakazi hasa wakati huu wanapojiandaa kusherehekea SikuKuu yao ya Mei Mosi, Bw. Rweyemamu alisema Rais Kikwete amefurahishwa mno na kauli mbiu ya mwaka huu inayosema ``Maisha bora kwa kila Mtanzania yanawezekana Mafisadi wakitokomezwa``.
Kutokana na hilo, amesema Rais amewataka wafanyakazi wawe mstari wa mbele katika mapambano ya kutokomeza rushwa na ufisadi.
``Rais anawaomba wafanyakazi, viongozi na wananchi kwa ujumla washirikiane na Serikali katika mapambano haya,``alisema.
Alionya kuwa wafanyakazi hawana budi kutambua kwamba wakikubali kutumiwa na vigogo katika `madili` yao wataonekana watu rahisi na hivyo kudharauliwa.
Alisema Mafanikio juu ya mapambano hayo yanategemea sana ushiriki wa wafanyakazi.
``Rais anawaomba wafanyakazi wasaidie kwa kutoa taarifa za vitendo vyovyote vya rushwa ili zifanyiwe kazi na wahusika wabanwe,``alisema.
Hata hivyo, alisema kwa vile Rais hatakuwepo kwenye sherehe hizo, atakutana na viongozi wa wafanyakazi akirejea safari.
Alipoulizwa ni kwanini mafisadi wanaojiuluzu hawachukuliwi hatua, Mkurugenzi huyo alisema si kazi ya Rais kuwachukulia hatua watuhumiwa hao, bali kuna vyombo husika.
Alisema mtu akishajiuzulu baada ya kutuhumiwa, kuna vyombo vinafanya kazi ya uchunguzi kwanza.
Bw. Rweyemamu alikumbusha kwamba Tanzania inaongozwa na utawala bora unaojali sheria.
Mmoja wa waandishi alimtaka Bw. Rweyemamu atoe ufafanuzi kuwa mawaziri wanaojiuzulu wanafanya hivyo kwa ridhaa yao au wanashinikizwa na Ikulu, hasa ikizingatiwa kwamba wanapotuhumiwa huapa kwamba hawataachia ngazi, lakini baadaye hutangaza kujiuzulu.
Akifafanua, Bw. Rweyemamu alisema mawaziri hao hujiuzulu kwa ridhaa yao. Alisema japokuwa awali huapa kwamba hawatajiuzulu, lakini hufanya hivyo baada ya muda mfupi kwa vile binadamu hugeuza mawazo.
Alikiri kwamba `madongo` ya vyombo vya habari yamechangia sana watu walioapa kutojiuzulu, kubadilisha mawazo.
Wakati huo huo, Rais Kikwete anaondoka nchini kesho kuelekea Addis Ababa kutimiza majukumu yake ya Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika AU.
Mbali na kuwa mgeni rasmi katika makabidhiano ya madaraka kati ya Mwenyekiti wa kamisheni ya Afrika anayemaliza muda wake Bw. Alpha Omar Konare, anayemwachia Bw. Jean Ping, Rais Kikwete pia atakuwa na mazungumzo na wafanyakazi wa Makao Makuu ya AU.
Pia katika ziara hiyo Rais anatarajiwa kuongoza kikao cha Baraza la Usalama na Amani la AU na kupewa taarifa juu ya shughuli za baraza hilo.
Bw. Rweyemamu alisema tarehe 30 Rais atakuwa nchini Uganda kwa mwaliko wa Rais Yoweri Museven, kwa ajili ya kutafuta ufumbuzi wa matatizo yaliyoanza kujitokeza nchini Burundi.