SEHEMU YA KUMI NA TANO
SEHEMU YA KUMI NA TANO
Sikukarahishwa na ile mikojo ya mama lao badala yake fikra zangu ziligandiana maneno ya Jojina ambaye n’do alikuwa shuhuda wa kila kinachoendelea.
Alikuwa amekiri kuwa hatuna ujanja na tumekamatika. Niliisikia na kuiona vyema mikono yangu jinsi ilivyokuwa ikitetemeka, nilijaribu kujiimarisha lakini sikuweza.
“Wewe kaza uso wako nitazame!!!” niliisikia sauti ya askari ikiamrisha, Jojina akazidi kutetemeka, sasa hakuwa akijikojolea tena, bila shaka mikojo ilijiishia katika kibofu!! . .Mimi ndo nilikuwa kwenye mashaka zaidi.
Niliiona miguu ya yule askari ikiwa imesimama imara mbele ya siti ya mwisho kabisa, bila shaka alikuwa akiwakagua akina Jojina.
Niliusikia mkono wa Jojina ulishuka kwa kasi na kuanza kunipapasa, alinishika sikio mara anishike kichwa!! Nikajiuliza kulikoni na bado sikufanya jitihada za kumzuia asinipapase. Sikujua anachokihitaji ni kipi. Mara akanishika pua na hatimaye akapanda juu kidogo akainyofoa miwani katika macho yangu.
Nilistaajabu nisijue kama hii ni hofu inasababisha ama ni kipi kinamsibu mwanamama huyu!! Nilikuwa namwomba Mungu afanye muujiza wowote ule na ile iwe ndoto. Tatizo ni moja tu!
Mungu hapangiwi kazi!! Yeye huombwa tu. Nami nikalazimika kuomba huku nikitarajia majibu ya haraka haraka.
Hatimaye miguu ile ikageukia upande aliokuwa ameketi Jojina. Hofu ikaongezeka maradufu.
“Kwani kuna nini hapa jamani!!!” nniliisikia sauti ya Jojina, sikujua anamuuliza nani.,
“Tiketi yako ipo wapi mwanamke??” sauti kali ya kiaskari ilijibu.
“Tiketi…tiketi yangu mimi….. Joshua, we Joshua….. mpe kondakta tiketi yake.” Jojina alijibu nikabaki kuduwaa kule chini nisijue nini kinaendelea baina yao.
Jojina aliendelea kusema maneno maneno, bila shaka aliyajua mwenyewe mimi nikabaki katika fumbo!!!
Kimya kikatanda, nikamsikia yule askari akisonya na mara akageuza na kuondoka zake.
Nilistaajabishwa sana na muujiza huo.
“Usitoke…vumilia huko huko!!!” alinong’ona Jojina, nami nikajizi kujikaza. Gari likawashwa!! Safari ikaendelea na kile kilichotokea kikabaki kuwa cha kutetwa ndani ya basi.
Baada ya dakika kadhaa Jojina aliniruhusu nitoke kule chini, hii ni baada ya abiria kadhaa kuwa wameuchapa usingizi wasijue kama nilitokea kule chini.
“Jojina umewalaghai kitu gani wewe mwanamke!!” nilimuhoji kwa sauti ya chini.
Akaanza kwa tabasamu kisha akanieleza kitu kilichonifanya niamini kuwa si lazima uende shule ndipo uwe na uwezo mkubwa wa kimaamuzi kama wa mama lao.
“Yaani nilikuwa najua kuwa sitaweza kuchomoka hapa, yaani kitu nilikuwa nimesahau ni kwamba Dulla huwa ana picha zangu tena nyingi tu, na wale jamaa waliniona nikiwanaye na mbaya zaidi aliwatambulisha kwangu. Hivyo ule mzoga kwa namna yoyote ile lazima skendo za kuua ziwe juu yangu. Sasa nikajibweteka kimawazo nikiamini ni wewe wanakusaka. Alikuwa pale hivi siti ya nne nd’o nikaiona picha, wacha nichachawe mtu mzima!! Yaani nikajua tumekwisha. Aliponikaribia zaidi nikaamua kama ni kufaacha nife kishujaa, ndo pale nikakupapasa nikakutoa miwani yako harakaharaka nikaitundika katika uso wangu. Aliponifikia nikaanza kujisemesha, jamaa akaniondoa miwani, aisee kitu nilichofanya najua mwenyewe, nikabenjua macho yangu, hii bolti nyeusi ikapotea ikabaki hii nyeupe, hii michezo naijua sana tangu zamani, wakati nabenjua nilikuwa napapasa huku na kule na mara nimkamate mkono, mara nimshike kifua. Nadhani unajua kilichotokea hapo, wasafiri bila kutumia aki;li wakaanza kukoroma kuwa mimi sina uwezo wa kuona tena wakitumia lile neno kali kabisa, kipofu!! Askari akaishiwa hamu, akanirejeshea miwani yangu machoni, nikayaweka macho yangu sawa na kumwona jinsi alivyokuwa na wasiwasi. Lakini nadhani ile picha nikiwa na kipara na uhalisia huu nikiwa na wigi umemwacha hoi. Kipofu mwenye wigi, wakati picha ni mtu anayeona akiwa na kipara.
Akasonya na kuondoka zake!! Sam siamini hata kidogo kama…….” Akasita kuzungumza, akaniegemea na kunong’ona, “kuna bwege anatuchora….” Aliniambia na kisha akanionya kuwa nisifanye jitihada zozote za kupepesa macho.
“Pita upesai nenda kamwombe kondakta,,, mwambie ninaumwa tumbo….pameharibika Sam hapa nenda haraka.” Akanisihi, upesi nikasimama na kupita nikafanya hima na kumfikia kondakta. Nikamsihi kama nilivyoelekezwa, nikalalamika sana juu ya mgonjwa wangu asiyeweza kuona anaumwa tumbo.
Kondakta akanielewa, nikarejea na kumchukua Jojina katika namna ileile ya kumwongoza mimi mbele yeye nyuma, akiigiza kuwa hana uwezo wa kuona. Wakati huu niliweza kumtilia mashaka yule mtu ambaye Jojina alidai kuwa hana nia nzuri, nilimwona akinong’ona na mwenzake. Nikajifanya sijui lolote linaloendelea.
Tulipoufikia mlango mimi nikiwa mbele kama kawaida mara tukasikia sauti kali ikiamrisha.
“Ninakutilia mashaka wewe mama usiyeweza kuona. Simama hapo hapo ulipo!! Nayaongea haya kwa mamlaka niliyopewa na jeshi la polisi Tanzania.” Niliskia miguu ikiishiwa nguvu, nikaanza kutetemeka. Lakini haikuwa hivyo kwa mama lao.
Ghafla akanisukuma nikatangulia nje.
“Saaaam poteaaaaa!!!” ndo neno pekee alilotoa, akatupa miwani huko, akaikunja sketi yake. Akili ikafanya kazi vyema sikulemaa, mwanamama anakimbia sijapata kuona, kumbe ule unene ni gelesha tu.
Nikaanza kufuata nyuma, huku nyuma zikawa zinasikika kelele za abiria. Yule askari sikuisikia sauti yake. Na niisikie ili iweje tena.
Nikapenya kila alipopita Jojina, mimi nyuma.
“Simama la sivyo nafyatua risasi!!!” ilisikika sauti kwa mbali, almanusura nisimame kama yasingekuwa maneno ya Jojina.
“Sam usisimame hakuna kitu hapo Sam kimbia.” Alinisisitiza pasipo kugeuka nyuma.
Maneno yake yakanitia wazimu wa kukimbia nikakazana zaidi. Hakika hatukujua ni wapi tunakwenda!!
Taratibu nilianza kuchoka, na bado nilisikia vishindo kwa nyuma. Jojina alikuwa ameniacha tayari na vile tulikuwa tukipenya katika majani sikuweza kumwona kabisa. Hofu ikaanza kutanda, dalili za kukata tamaa zikanikumba.
“Jojinaaa…..Jojinaaa..” nilianza kuita lakini sikujibiwa.
“Simama kimburu Kenge, shenzi kabisa simama.” Sauti iliamrisha kwa nyuma. Nilikuwa nimechoka, nikasikia miguu ikigongwa kwa nyuma, nikayumbayumba kisha kama mzigo nikatua chini.
Meno yangu yakauma nyasi!!! Nikajitahidi kugeuka nikakutana na mwanaume akiwa ameshikilia pingu. Alikuwa anahema juu juu, ni yuleyule mwanaume ambaye tulikuwanaye ndani ya gari. Alikuwa ananitazama kwa jicho kali.
“Shetani mkubwa!!!” nikasikia sauti nyingine ikasikika ikitokea katika majani!!! Mimi na yule mwanaume mwenye pingu tukatahamaki, lakini hatukudumu sana mara yule mwanaume akaaguka chini akijishika kichwa, nikaona jiwe kubwa pembeni yake. Na hapo akatokea yule mama aliyejikojolea ndani ya gari.
Jojina kwa mara nyingine!!!
“Mshenzi mkubwa wewe ukipona nenda kamweleze mkuu wako wa kazi kuwa kuna watu wabaya anawafuga huko.” Alikoroma mama lao. Lakini huyo mtu aliyepewa nafasi ya kupona akataka kuleta ujanja, ambao Jojina aliutegemea kumbe, akasimama na kurusha teke, mama lao akaingiza mkono wake katika sketi yake, akatoka na jiwe jingine kazuga kama analirusha yule askari akajificha kwa kutumia mikono miwili huku akiruka kando.
Jojina akatabasamu wakati yule bwana anaitoa kinga yake usoni, hapohapo akalivurumisha lile jiwe.
Nilibahatika kuona meno kadhaa yakitoka katika kinywa cha yule bwana. Kufikia hapo mama lao hakuwa akizuilika.
“Auaye kwa upanga……” alisema huku akitua juu ya mwili wa yule bwana anayevuja damu,
“Atauwawa kwa upange vilevile” akamalizia huku akiishika ile pingu na kuanza kumcharaza nayo yule bwana usoni.
Kila alipoituliza paliumuka kisha damu!!
Akapiga kwenye taya, akapiga paji la uso!! Akapiga kila kona!!!
Kisha mbio zikaendelea. Kidogo nilikuwa nimepumzika. Nikaweza kukimbia zaidi, wakati huu tukiwa sambamba na mama lao Jojina.
“Niliwahi kuwa mwanariadha shule!!” alisema bila kunitazama.
Sikumjibu.
Hapakuwa na mtu anayetufuatilia kwa nyuma!!!
“Hivi unajua tunapoelekea lakini?” Jojina aliniuliza, hapo tukajikuta tunapunguza mwendo taratibu huku kila mmoja akikumbwa na kiwewe.
“Hata sijui ndugu ujanja wangu mimi Morogoro mjini tu Msamvu, Kihonda basi!!” nilimjibu na hatimaye tulikuwa tumesimama.
Jojina akajipekua na kutoka na simu yake katika koba lake ambalo hakuwahi kulitua hata mara moja tangu tuliposhuka garini na kuanza kutimua mbio.
“Simu imezima chaji aisee tungeweza hata kutumia ramani ya simu kama ingeweza kufaa.”
Akasonya kisha akairudisha simu yake mkobani.
Tukaendelea kutembea kuelekea mbele bila kufahamu kama ni salama ama hatari.
“HIFADHI YA TEMBO MIKUMI” Kibao kikatukaribisha baada ya mwendo mrefu.
“Mungu wangu tupo mbugani Sam!! Mbugani Mikumi hapa…” aliweweseka Jojina nami nikapagawa. Hapakuwa na ngojangoja zaidi tukaanza kukimbia kuelekea uelekea mwingine, tukapishana na makundi ya Swala, na kwa mbali kabisa tukaiona barabara. Tukaukaza mwendo zaidi hadi tulipoifikia ile barabara.
Ilikuwa barabara ya vumbi, na ilikuwa bahati yetu tena tukaonana na wanadamu. Tukauliza na kupewa uelekeo wa barabara ya kuelekea Iringa, tukakaza mwendo, miguu yangu ilikuwa hoi sana lakini sikukubali kuonekana lelemama.
“Sam hawa jamaa tunaopambana nao hawa wananikumbusha hekaheka za Tunduma huko.” Jojina akaanzisha maongezi, walau mwendo na maongezi wapunguza uchovu.
“Tunduma? Harakati zipi tena huko.”
“Wakati ule wa uchunaji ngozi bwana!! Yaani kuna mdogo wangu fulani hivi kidogo achunwe ngozi, mwanamama nikaingia ‘front’ kutetea damu aisee, yaani mafunzo ya mgambo niliyopitia yananibeba sana mara kwa mara. Nikamjua jamaa anayewafahamu mabwana waliomteka dogo, aisee akajifanya mbishimbishi, nilimpiga ngumi mbili akalegea huko nikamkamata, nikamuwasha vibao ka’ vinne hivi wacha apagawe!! Nikamzuga kama nampiga teke akasema atanipeleka, nikamshika ile staili inaitwa Tanganyika jeki, yaani nikamkamata suruali yake huku nyuma nikamyanyua akawa anatembelea vidole. Moja kwa moja hadi eneo la tukio, saa nane usiku hiyo mwanamke barabarani. Nimeficha kisu huku kwenye pindo la sketi, tumbili yeyote ajiweke mbele yangu nafyeka korodani zake namtia uhanithi mimi!!, nikafika pale, nikatia mkwara na jamaa akiwasihi, mbona walimtoa ndani, walikuwa nd’o wanajiandaa na safari ya kwenda Zambia wakamchune ngozi….nikaondoka naye mabwege wananishangaa tu!! Chezea mama lao wewe!!!” alimaliza simulizi hii kwa majigambo, nikamkodolea macho wakati huo tukiwa barabarani tayari.
Kichwani nikakiri kuwa huyu Jojina alikuwa na mengi zaidi ya nilivyomtambua.
Baada ya muda tukafanikiwa kuelewana bei na lori la mbao lililokuwa linaelekea Mafinga,
Jojina akawa siti ya mbele mimi nikawa nyuma huku na vijana wengine.
Safari hii haikuwa na mushkeri wowote ule.
Tukafika Iringa mjini majira ya saa nne usiku!!
Tukatembea kwa miguu kuitafuta nyumba ya Jojina.
Tukaifikia nyumba vyema, lakini mazingira haya yalikuwa tofauti kidogo!! Ni kama kuna aidha ukarabati ulikuwa umefanyika ama la yale makazi kuna mtu aliongeza ama kupunguza kitu.
Naam!! Tulipoufikia mlango palikuwa na kufuri!!
Nani amefunga sasa? Wakati sisi tulikuwa tukitumia kitasa cha kawaida!!
Hatukungoja usiku ule upite, tukazunguka kwa nyuma na kuifikia nyumba ya mmiliki wa nyumba zote pamoja na chumba alichokuwa amepanga mama lao!!
Mwenye nyumba alikuwa hajalala, kuna mambo ya faragha alikuwa anashughulika nayo na mkewe na bila shaka ujio wetu ulimshtua sana!!!
“Kulikoni Jojina…” aliuliza kwa sauti tulivu.
“Mimi n’do niulize kulikoni kama ni kodi yako nilimaliza mapema tu vipi tena kufuli jipya mlangoni kwangu!!”
Mwenye nyumba akaduwaa kabla hajauliza.
“Wewe mwanamama wewe mbona mnataka kunivuruga sasa. Si wamekuja kaka zako hapa na dada zako wengine kudai kuwa unahama wewe, tena wamekuja na simu yako wewe kuwa haurudi tena hapa. Tena kizuri zaidi walikuja na mwenyekiti wa mtaa na mjumbe, mimi nikawaruhusu wakachukua mizigo yako kuwa wanakuletea huko ulipo, sijui kwa mume wako wewe!! Mi hayo sijui na hapa wakaacha vitu vichache tu!!!” alijibu kwa kujiamini baba mwenye nyumba.
“Mungu wangu weeeee!! Bahasha!!!” ndicho kitu cha kwanza kabisa kukumbuka kuwa tulikiacha ndani ya chumba kila kabla ya kusafiri!!!
Jojina akalegea na kushuka chini.
Akakaa!!
Nikaungana naye katika fedheheko hili!!!
Bila kithibitisho kile ni wapi zaidi pa kujitetea?
Tumekwisha!!!!
Nilikiri kimoyomoyo!!!