Tanzania inatarajiwa kuingia katika orodha ya nchi 10 zinazoongoza kwa uzalishaji wa uranium duniani ifikapo mwaka 2029, kupitia mradi wa Mantra Tanzania Limited unaotarajiwa kuzalisha tani 3,000 za madini hayo kwa mwaka na kutoa ajira zaidi ya 4,000.
Meneja wa Uendelevu wa Mantra Tanzania Limited, Majani Wambura, amesema hayo katika kikao cha Mining Breakfast Briefing (MBB) kilichoandaliwa kwa ushirikiano wa Wizara ya Madini na Chemba ya Migodi Tanzania (TCM).
Amesema utafiti uliofanyika umebaini hifadhi ya takribani tani 58,500 za uranium, huku mradi ukitarajiwa kuwa na maisha ya zaidi ya miaka 20 na tafiti zaidi zikiendelea kubaini uwepo wa rasilimali nyingine.
Wambura amesema utekelezaji wa mradi huo utaongeza shughuli za kiuchumi, ajira na mapato ya Serikali, sambamba na kuiweka Tanzania katika nafasi ya ushindani kwenye soko la kimataifa la madini ya uranium kutokana na matumizi makubwa ya madini hayo katika uzalishaji wa nishati ya umeme pamoja na sekta ya afya.
Akizungumza katika kikao hicho, Waziri wa Madini, Anthony Mavunde amesema Serikali itaendelea kushirikiana na wadau wa sekta ya madini kupitia majukwaa ya majadiliano ili kujenga sekta yenye ushindani, inayovutia uwekezaji na kuchangia zaidi ukuaji wa uchumi wa Taifa.
Amesema Serikali itaendelea kuboresha mazingira ya uwekezaji na kutatua changamoto zinazojitokeza ili kuongeza uzalishaji, ajira na mapato.