Mfanyabiashara Tajiri zaidi Barani Afrika, Aliko Dangote, ameonyesha dhamira ya kuwekeza na kuongoza ujenzi wa Kiwanda kikubwa cha kuchakata mafuta kwa Ukanda wa Afrika Mashariki, hatua inayotajwa kuwa inaweza kubadili mwelekeo wa Sekta ya Nishati katika eneo la Afrika Mashariki,
Dangote amesema yuko tayari kutumia uzoefu na Teknolojia ya kisasa aliyoitumia kujenga Kiwanda chake kikubwa Nchini Nigeria chenye uwezo wa kuchakata mapipa 650,000 kwa siku.
Akizungumza katika mkutano wa Ufadhili wa Miundombinu uliofanyika Jijini Nairobi, Rais wa Kenya, William Ruto, amesema Nchi za Afrika Mashariki zimeanza majadiliano ya pamoja kuhusu uanzishwaji wa kiwanda hicho, ambacho kinatarajiwa kujengwa katika bandari ya Tanga Nchini Tanzania, ambapo ameeleza kuwa mradi huo una thamani ya kimkakati kwa Ukanda huo, hasa katika kuimarisha uhakika wa upatikanaji wa Nishati na kupunguza utegemezi wa nje.
Aidha, Ruto amesisitiza kuwa Kiwanda hicho kimepangwa kunufaisha Nchi kadhaa ikiwemo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Kenya, Sudan Kusini na Uganda, kwa kutumia mafuta ghafi yanayozalishwa ndani ya Ukanda huo badala ya kuyasafirisha nje bila kuyachakata.
Kwa sasa, Nchi nyingi za Afrika Mashariki zimeendelea kutegemea uagizaji wa mafuta yaliyosafishwa kutoka Mashariki ya Kati, hali ambayo imeziweka katika hatari ya kuyumba kwa bei na usambazaji, hasa wakati wa migogoro ya kimataifa hususan unaoendelea huko Mashariki ya Kati, changamoto ambayo imekuwa ikiongeza gharama za maisha na kuathiri uchumi wa Nchi hizo kwa kiwango kikubwa.
.
View attachment 3578460