Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) kimetoa taarifa kikieleza kuwa April 15, 2026, Mwenyekiti wake, Tundu Lissu, amewasilisha mapendekezo muhimu kwa Rais wa zamani wa Jamhuri ya Malawi, Lazarus Chakwera, akiwa mahabusu katika Gereza la Ukonga jijini Dar es salaam, wakati Lissu alipopata fursa ya kukutana na Kiongozi huyo.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano na Uenezi wa CHADEMA, Brenda Rupia, Lissu amewasilisha hoja kadhaa zinazolenga mustakabali wa demokrasia na utawala wa sheria Nchini Tanzania, miongoni mwa hoja hizo ni pamoja na kueleza kuwa kesi ya uhaini inayomkabili inatokana na msimamo wake wa “No Reforms, No Election,” akisisitiza kufutwa kwa kesi zote zinazomkabili yeye na chama, pamoja na utayari wake kushiriki mazungumzo akiwa huru.
Taarifa hiyo inaeleza kuwa Lissu pia amependekeza kufanyika kwa uchunguzi huru wa kimataifa kuhusu matukio ya Oktoba 2025 kupitia Taasisi za Kikanda kama SADC, pamoja na kuwepo kwa mazingira wezeshi yatakayowezesha mazungumzo ya kweli na utekelezaji wake.
Aidha, amesisitiza umuhimu wa uwajibikaji wa taasisi mbalimbali za umma ikiwemo Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (INEC) na Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), akirejea pia mapendekezo ya ripoti za Jaji Nyalali (1992) na Jaji Chande (2023), kuhusu mageuzi ya kisiasa na kiutawala.
Katika hatua nyingine, Lissu ameeleza umuhimu wa kufanyika kwa mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, ikiwa ni pamoja na kuundwa kwa chombo huru cha kusimamia uchaguzi, kwa kuzingatia ripoti za waangalizi wa uchaguzi kuanzia mwaka 1995 hadi 2025, pamoja na mapendekezo ya Tume za Jaji Warioba na Nyalali.
Wakati huo huo, CHADEMA imesema Lissu amepatiwa nakala ya uamuzi wa Mahakama ya Rufani uliotolewa Aprili 15, 2026 unaoruhusu chama kuendelea na shughuli zake, ambapo baada ya kuupitia uamuzi huo, ametoa wito kwa Wanachama na Watanzania kwa ujumla kujiandaa kwa hatua zinazofuata za kisiasa, hususan maandalizi ya mikutano ya hadhara.
.