Ujue utaratibu wa Kuchagua Papa.
Baada ya Kifo cha Papa shughuli zote za Kanisa Katoliki huwa chini ya Baraza la Makardinali.
Hawa wanasimamia shughuli za kila siku za Kanisa na kutoa maamuzi juu ya mambo ya dharura tu. Baraza la Makardinali ndio linajukumu pekee la kuchagua Papa mwingine.
Baraza hili ndio hutangaza rasmi tarehe ya kuzikwa Papa na tarehe ya kufanya uchunguzi wa Papa mwingine.
Tayari Baraza la Makardinali limekwisha tangaza kwamba, Papa Francis atazikwa siku ya Jumamosi, huko Roma. Bado tarehe ya kufanya uchaguzi wa Papa mwingine bado haijatangazwa
Kwa kawaida, utaratibu unataka ibada na maomboleze ya Kifo cha Papa yafanyike kwa muda wa siku 9 mfululizo.
Katika siku hizo 9, kama hakuna kipingamizi kingine mazishi yanapaswa kufanyika kuanzia siku ya 4 na si zaidi ya siku ya 6.
Baada ya Papa kuzikwa, Kanisa litaendelea kuomboleza hadi siku 9 zitimie. Kisha uchaguzi wa Papa utafuata.
Siku ya kwanza, Makardinali wote ambao wana sifa ya kupiga kura watafanya ibada. Mchana wa siku hiyo wataandama kwenda kwenye chumba maalumu kilichoandaliwa.
Siku hiyo watakulipa kiapo cha uaminifu. Katika kipindi chote hicho, Makardinali hawaruhusuwi kuwasiliana kwa njia yoyote ile wala kusoma magazeti mpaka atakapopatikana Papa Mpya.
Siku zinazofuata uchaguzi utafanyika. Kura zipigwa kwa kura ya siri. Kardinali atakayepata theluthi mbili ya kura zote ndie atatangazwa kuwa Papa.
Iwapo baada ya siku 3 mfululizo za kupiga kura kutakuwa hakuna Papa aliyepatikana, Makardinali watapewa siku 1 ya kupumzika na kutafakari.
Kisha watarudi tena kuendelea kupiga kura hadi Papa achaguliwe. Iwapo kura zitapigwa mara 7 na hakuna aliyechaguliwa, Makardinali watapumzika tena siku 1.
Iwapo kura zimetosha, Kardinali aliyechaguliwa ataitwa mbele ya Baraza la Makardinali na kuulizwa, "Je, unakubali kuchaguliwa kwako kuwa Papa?" Iwapo atakubali ataulizwa tena " Je Unataka kuitwa jina gani?" Baada ya Papa Mteule kutoa jina, mashahidi wawili wanaohusika na sherehe za kipapa wataandaa kiapo na Jina la Papa.
Kuanzia muda huu, Kardinali aliyeshinda anakuwa na Mamlaka kama Papa. Kisha Makardinali hula kiapo cha uaminifu. Baada ya hapo dunia itatangaziwa kupatikana kwa Papa Mpya.