Ili kulinda ukuaji uchumi na kuepuka athari za kupanda kwa gharama za maisha, Tanzania imejadiliana na Benki ya Dunia juu ya namna itakavyosaidiwa kukabiliana na athari za upungufu wa Dola ya Marekani katika mzunguko wa fedha.
Majadiliano hayo yanakuja, katikati ya wimbi la kupungua kwa sarafu hiyo duniani kunakotajwa kuchagiza ongezeko la bei ya baadhi ya bidhaa muhimu yakiwemo mafuta.
Tayari uhaba wa sarafu hiyo, umeacha makovu katika bei ya mafuta kulingana na taarifa ya jana ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (Ewura).
Taarifa hiyo, imeeleza katika Jiji la Dar es Salaam bei ya Petroli imepanda kwa Sh14 huku dizeli ikipanda kwa Sh324.
Pamoja na majadiliano ya kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na benki hiyo, msaada wa kukabiliana na kupanda kwa sarafu hiyo ni jambo lingine lililojadiliwa.
Majadiliano hayo yamefanyika jijini Dar es Salaam leo, Septemba 6, 2023 ujumbe wa Tanzania ukiongozwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigumu Nchemba, huku Benki ya Dunia ikiwakilishwa na Mkurugenzi wake anayesimamia kanda ya mashariki na Kusini mwa Afrika, Hassan Zaman.
Katika majadiliano hayo ameiomba benki hiyo, kuharakisha upatikanaji wa zaidi ya dola za Marekani 500 milioni ifikapo Novemba mwaka huu.
Ameeleza fedha hizo zitaisaidia nchi kukabiliana na changamoto ya upatikanaji wa sarafu hiyo katika mzunguko wa fedha nchini hali inayochangia mfumuko wa bei na kukwamisha uagizaji wa bidhaa muhimu kutoka nje ya nchi yakiwemo mafuta.
Pia, alitumia fursa hiyo, kuishukuru Benki ya Dunia kwa kuidhinisha upatikanaji wa fedha kwenye miradi nane yenye thamani ya zaidi ya Dola za Marekani 2.16 bilioni.
Akizungumza katika majadiliano hayo, Zaman amepongeza hatua za Serikali za kukuza uchumi licha ya uwepo wa janga la Uviko-19.