Makapuku Forum

Chama cha Wahariri Mashariki mwa Afrika kimemchagua Mwenyekiti wa Chama Cha Wahariri Uganda, Daniel Kalinaki kuwa Rais wa Chama hicho kwa kipindi cha miezi 12 ijayo.

Kalinaki amechaguliwa katika mkutano mkuu wa mwaka wa jamii hiyo uliofanyika jijini Lusaka nchini Zambia na wawakilishi wa majukwaa na vyama mbalimbali vya wahariri kutoka Kenya, Tanzania na Ethiopia.

Baada ya Kalinaki kumaliza muda wake hapo mwakani, nafasi hiyo itaongozwa na Deodatus Balile ambaye ni Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF).

Kalinaki ambaye pia ni kiongozi wa uratibu katika vyombo vya habari vinavyomilikiwa na Kampuni ya Nation Media Group nchini Uganda ana uzoefu wa zaidi ya miaka 25 katika tasnia ya habari.
 
Mchezo wa Ligi Kuu Bara kati ya Simba dhidi ya Ruvu Shooting umemalizika kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi huku Ruvu Shooting ikishuka daraja rasmi leo.

Katika mchezo huo Simba ilipata bao dakika ya 30 kupitia kwa kiungo wake, Clatous Chama na dakika ya 72 na 90 mabao yalifungwa na Pape Sakho

Simba ipo nafasi ya pili na alama 67 huku Ruvu shooting ikishika mkia na alama 20 na kubakiza mechi mbili mkononi ambazo hata akishinda bado itashuka daraja.
 
Wakili Harold Sungusia amechaguliwa kuwa Rais wa Chama cha Mawakili wa Tanganyika (TLS) katika uchaguzi uliofanyika leo Ijumaa Mei 12, 2023.

Sungusia ambaye mwaka jana pia aligombea nafasi hiyo na kushindwa na Rais aliyemaliza muda wake Profesa Edward Hosea ametangazwa kushinda baada ya kupata kura 748.

Mpinzani wake Wakili Reginald Shirima alipata kura 77 licha ya kuibuka katika uchaguzi huo na sera ya kuifanya TLS kuendelea kuwa Chama cha kitaaluma na sio chama Cha kiharakati.

Akitangaza matokeo hayo mwenyekiti wa kamati ya uchaguzi TLS, Wakili Mwandamizi Charles Rwechungura amesema kura zilizopigwa katika uchaguzi huo zilikuwa 825 na hakuna ambayo imeharibika.
 
Rais wa Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan leo Ijumaa Mei 12, 2023 amemteua Mkurugenzi wa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC), Mussa Mohamed Makame kuwa Mwenyekiti wa Bodi ya Ushauri na Uwekezaji wa Mfuko na Gesi.

Aidha, Rais Samia amewatua wajumbe wengine wanne wa bodi hiyo akiwemo Dk Suleiman Missango, meneja msaidizi kurugenzi ya utafiti na sera, Benki Kuu ya Tanzania (BoT).

Pia, amemteua Safiel Msovu ambaye ni afisa fedha mwandamizi wa TPDC na Shogholo Msangi ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya Express Microfinance Company Limited.

Aidha, Rais Samia amemteua Mwanaidi Mtanda kuwa mjumbe wa bodi hiyo ambaye aliwahi kuwa mhasibu mkuu wa Serikali.

 
Makamu mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lisu amesema Tanzania inakuwa masikini kwa sababu ya katiba mbovu iliyotugwa mwaka 1977.

Hayo ameyasema leo wakati akihutubia wananchi wa wilaya ya Kahama mkoani Shinyanga ambapo amesema wananchi wasidanganywe kwamba katiba mpya haina maslahi kwasababu viongozi waliopo madarakani hawataki kuruhusu mabadiliko kwa sababu itawabana.

"Katiba iliyopo ni ya kukandamiza wananchi, kwani ukiangali mchele,mafuta, Sukari, mafuta ya kupikia, ya taa na vitu vingine havikamatiki kwa sababu ya utitiri wa kodi nyingi, tozo na ushuru kwani ukiongeza bei kwenye mafuta na ukichukua ushuru wa mpunga kabla haujakobolewa bei ya bidhaa inaongezeka, hivyo sehemu kubwa ya bei ni kodi ambayo inatokana na katiba iliyopo inawaumiza wananchi,amesema Lissu.

 
Daktari binafsi wa Benard Membe, Profesa Harun Nyagori amesema kifo cha mwanasiasa huyo kimechagizwa na ugonjwa wa maambukizi ya mfumo wa mapafu hewa.

Taarifa hiyo ya daktari inakuja kipindi ambacho kumekuwepo na taarifa mbalimbali katika mitandao ya kijamii kuhusu chanzo cha kifo chake.

Membe amefariki dunia leo, Ijumaa ya Mei 12, 2023 katika Hospitali ya Hubert Kairuki jijini Dar es Salaam.

Akizungumza nyumbani kwa marehemu, Profesa Harun amesema ugonjwa huo unasababisha mgando wa damu na kuzuia mapafu kupeleka hewa ya oksijeni.

"Hali hii inaweza kumkuta mtu yeyote mara tu anapopata maambukizi haya kwa njia ya hewa hata kwa wagonjwa wanaopata pneumonia pia inaweza kuwakuta.

"Kinachozungumzwa huko mtaani kwamba mzee ameuawa amepewa sumu sijui nini, hiyo iondoke, ukweli ni kwamba amefariki kwa maradhi ya kawaida," amesema Profesa Nyagori ambaye pia ni Mtaalamu wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI).
 
Maziko ya waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Benard Membe yanatarajiwa kufanyika Mei 16, mwaka huu kijijini kwao, Londo mkoani Lindi.

Membe amefariki dunia, leo Ijumaa ya Mei 12, 2023 katika hospitali ya Hubert Kairuki jijini Dar es Salaam alikokuwa akipatiwa matibabu baada ya kuugua ghafla.

Akizungumzia taarifa ya mazishi nyumbani kwa marehemu, Mikocheni jijini hapa, Msemaji wa familia, Jaji Mustafa Ismail amesema taarifa zaidi zitatolewa baadaye.
 
Baadhi ya waombolezaji na waliojitokeza kwenye maandalizi ya mazishi ya Waziri wa zamani wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Bernard Membe nyumbani kwake, Mikocheni jijini Dar es Salaam.

Membe amefariki dunia leo asubuhi Ijumaa Mei 12, 2023 akiwa katika Hospitali ya Kairuki Dar es Salaam wakati akiendelea kupatiwa matibabu.
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…