Polisi mkoani Songwe limemkamata, Aloyce Nyabwanzo (53), Mkazi wa Kitongoji cha Kikamba, Kijiji cha Kapalala wilayani, Songwe kwa tuhuma za kuwaua wajukuu zake wawili kwa kuwapasua mafuvu ya kichwa na mchi wa kutwangia.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Songwe, Theopista Mallya amesema tukio hilo lilitokea Aprili 30, 2023 majira ya saa 5:00 alfajiri na kwamba jeshi hilo linaendelea na uchunguzi ili kujua sababu za mtuhumiwa huyo kutenda tukio hilo.
Amesema mtuhumiwa aliwashambulia wajukuu zake wakati wanatoka chumbani wakimfuata bibi yao sebleni aliyekuwa anajaribu kuzuia vurugu hizo zilizoanzishwa na babu nyakati hizo za usiku.
Marehemu wamefanyiwa uchunguzi na daktari na kubaini kuwa vifo vyao vimesababishwa na kupasuka kwa mafuvu ya vichwa baada ya kupigwa na kitu kizito hali iliyosababisha kuvuja damu nyingi na ubongo kutoka nje,” amesema Kamanda Mallya.
Amewataja marehemu hao kuwa ni Jackson Chacha (2) na George Chacha (5) wote wakazi wa kitongoji cha Iwindu- Kikamba katika Kijiji cha Kapalala na walikuwa wakilelewa na mtuhumiwa.
Hata hivyo, Kamanda Mallya amesema wakati uchunguzi wa kujua sababu zilizosababisha mtuhumiwa kutenda tukio hilo, watapelekwa hospitali ili kupimwa afya ya akili.