Mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Amos Makalla, amepokea Mabasi 70 ya Mwendokasi kwa ajili ya kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma ya usafiri kwa Wakazi wa Dar es salaam.
Akizungumza wakati wa kupokea Mabasi hayo RC Makalla amesema anafurahishwa kuona mafanikio hayo yamepatikana ndani ya siku 100 za Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan ambapo amesema upatikanaji wa magari hayo utaenda kutatua kero za Wananchi.
RC Makalla amesema Serikali imejipanga kutatua changamoto ya Mafuriko Dar es salaam hususani eneo la Jangwani ambayo imekuwa ikisababisha usumbufu wa kusimama kwa huduma za usafiri nyakati za mvua.
Changamoto nyingine ambazo RC Makalla amezipokea kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa UDART na kuahidi kuzipatia ufumbuzi ni kero ya Bodaboda na magari binafsi kuingia kwenye Barabara za Mwendokasi na Wafanyabiashara kuendesha biashara zao kwenye Barabara za Mwendokasi.