Tafasiri Unavyoweza: Afisa wa Polisi na Askari
Hakuna ubishi kuwa asilimia 99 ya polisi wetu hapa nchini wanafanya kazi kwenye mazingira yasiyo rafiki kabisa. Hili linajulikana na halina ubishi. Vitendea kazi vyao vingi bado ni duni na vichache sana, inafikia hadi si ajabu kumuona afisa wa polisi akiwa kavaa raba mtoni kazini. Nini nataka kuandika leo kuhusu afisa wa polisi na askari, subiri. Ninataka kuonesha kuwa kuna tofauti kubwa sana kati ya afisa wa jeshi la polisi na askari. Mmoja ni yule anayehakikisha usalama wa raia na mali zao unazingatiwa na askari ni yule ambaye anahakikisha hata kama una haki ya kitu fulani hukipati na ukibisha anakuchoma kisu unakufa. Tafasiri unavyoweza.
Unajua kabisa Ijumaa huwa siandiki mambo magumu mamgumu maana hakuna haja ya kuumiza sana kichwa mwisho wa wiki, ni muda wa kujipa mapumziko ila nilipokuwa napekua baadhi ya makabrasha yangu nikaona tafasiri ya neno askari, na nikavutiwa na hii inayomuonesha kama mtu mnyanyasaji, anayetetea kundi la wakandamizaji, wezi na siku zote yuko upande wa wenye nguvu, anawalinda wenye nguvu kwa hali na sheria huku akiwakandamiza wale anaopenda kuwaita 'raia'.
Afisa wa polisi yeye ni tofauti, huyu hujipambanua kwa kuhakikisha hakuna unyanyasaji dhidi ya mtu na mtu, barabarani kuko salama na usiku unalala na kuota ndoto zako huku ukiwa na uhakika afisa wa polisi anakulinda wewe na mali zako. Akikusimamisha kwa kosa anakusalimia, anajitambulisha anakueleza kosa lako na kukutaka uambatane naye kituonni inapobidi, hakufungi pingu kama hujakaidi. Anategemea umwambie ukweli maana hatokusingizia makosa usyiyoyajua.
Nikutakia Ijumaa njema na mapumziko mazuri ya wikend. Tukutane wiki ijayo.