Tafasiri Unavyoweza: Maarifa Ondoa Sura ya Umaskini
Naandikia nikijua kabisa tafasiri ya umaskini inachanganya, lakini pamoja na kuchanganya kwake bado wengi tunakubaliana kuwa umaskini ni ile hali ya kukosa huduma muhimu za kibinadamu kama chakula, malazi na nguo na baadhi yetu tunaenda mbali zaidi na kusema kukosa hitaji la mapenzi (sex) ni umaskini. Umaskini pamoja na tafasiri mbalimbali bado linabaki kuwa ni tatizo kubwa kwenye jamii yetu na hata siku moja usiuhusishe umaskini na kukosa pesa, ni zaidi ya hapo. Umaskini una sura nyingi, tafasiri unavyoweza.
Maarifa kwa maana ya ufahamu ni hali ya kujua/kutambua na kuwa na ustadi wa jambo au mambo kadhaa. Maarifa huzaliwi nayo, husakwa iwe darasani au kwenye maisha unayoishi na unakuwa tayari kutumia taarifa uliyojifunza kwa kuona au kushiriki kujiletea maendeleo yako (kupambana na umaskini). Hoja yangu kubwa hapa ikiwa ni umuhimu wa taarifa katika kujiletea maarifa ya kupambana na umaskini ambalo si tatizo la mtu mmoja bali la jamii nzima, tajiri mmoja ndani ya maskini wengi ana hasara ya kuwa tajiri.
Unapokosa nafasi ya kujisomea japo kitabu au gazeti au kusoma habari mtandaoni basi una ukaribia umaskini kwa kasi ya kimbunga. Ni hasara kubwa sana na tena ni umaskini unaotopeza kukosa taarifa. Ukikosa taarifa (information) unawapa nafasi manyang'au kukuamulia mambo ukiwa macho na ukiwa umelala. Ndiyo, watawala wengi wanaficha taarifa ili wazidi kukuibia na ndiyo maana nyumba zao zina mageti makubwa ili kukuzuia usijui taarifa unazostahili. Watakusemea na mdomo unao, wataona kwa macho yako, watasimama juu ya kaburi lako kwa sababu umewapa nafasi ya kukutenda watakavyo kwa sababu hujaamuka kusaka maarifa upambane na umaskini.
Tuonane wiki ijayo, weekend njema