Makapuku Forum

Sehemu ya tatu



Nilichukua leso kupunguza machozi yaliyokuwa hayakomi kunichuruza usoni. Ndipo muda ule nilipotazama vizuri eneo la jukwaa la mbele karibu na jukwaa kuu kuna mtu nilimuona. Aaaah! moyo wangu ulifarijika kwa kuwa alikuwa kwenye kumbukizi zangu muda mfupi. Nilijua kiasi gani alijitahidi kulipinga jina la German Machine lakini leo hii naye amekuwa miongoni mwa waombelezaji walioshika bendera za Ujerumani na Tanzania akimlilia mtu ambaye alimjua tokea anaanza kufukuzia ndoto zake. Nilimtazama na kutabasamu nikiwa katikati ya huzuni. Hakuwa mwengine yule mtu bali mwalimu Kisayo. Mwalimu wa kwanza shuleni kumpiga na kumfikisha ofisini baada ya kukuta daftari la somo lake limeandikwa jina GERMAN MACHINE.
Nilipotupa macho vizuri jukwaa kuu upande ule wa mwalimu Kisayo ndipo nilimuona yule mwalimu wetu mkuu wa shule ya msingi. Nilizidi kufarijika kumuona akiwa mstari wa mbele tayari kutoa heshima zao za mwisho. Ubongo nao haukuacha kunifunulia kumbukumbu za nyuma hasa nilipomtazama mwalimu mkuu. Nilijikuta nasafiri tena kwenye kumbukizi hadi siku ile German Machine akiwa amepiga magoti akilia kwa shinikizo la walimu waliomtaka aachane na hilo jina kwenye mambo ya msingi. Niliamini tukio lile hata mwalimu mkuu muda ule lazima angelifikiria tu. Nakumbuka yeye ndie alikuwa wa kwanza kwa ulimi wake kutengeneza ruksa ya uhuru wa jina la German Machine. Ilikuwa kama utani lakini amejikuta ameingia kwenye historia kubwa leo hii.
* * * *
||MIAKA 12 NYUMA||
"Sasa kipi kikulizacho eeh!" mwalimu mkuu alimuuliza huku akimtazama usoni.
"Anataka fimbo huyo mwalimu." Mwalimu wa darasa alidakia. Lakini mwalimu mkuu alimpa nafasi ya kusema kwanini analia. Ndipo hapo aliunyanyua uso na kuzungumza.
"Mwalimu machozi yanayonitoka usoni hayafanani hata robo ya yale yanayomwagika moyoni mwangu. Nina hakika hata nikikubali kwa mdomo bado nitakuwa nimewadanganya ndani ya moyo wangu. Sina sababu ya kusema uongo walimu naomba mniache niwe German Machine huenda nikafanya kitu kama Johannes Kepler."
Aliposema hayo mwalimu mkuu alisimama kutoka pale dawatini alipokaa. Alimsogelea na kumuuliza.
"Unamfahamu Johannes Kepler?"
"Ndio mwalimu ingawa yeye hakuwahi kunifahamu kabla."
"Ha ha ha haaa una maajabu na vituko sana wewe? Eti wanafunzi mnamfahamu Johannes Kepler" Aliligeukia darasa mwalimu na kutuuliza. Hakika binafsi jina hilo ndio nililisikia pale. Ilikuwa wazi hata walimu wengine hawakulijua labda. Isipokuwa mwalimu mkuu.
"Hapana mwalimu hatujawahi kumsikia." Darasa lilijibu.
"Haya hebu simama uwaambie wenzako huyo Johannes Kepler ndie nani? yuko wapi na wewe unataka kufanya kitu gani kama alichokifanya yeye." Darasa zima tulitulia baada ya mwalimu mkuu kumpa nafasi ile tupate kusikia na kumjua huyo mtu aliyekuwa mgeni masikioni mwetu. Na kweli alisimama na kusema.
"Johannes Kepler ni mwanasayansi bingwa wa hesabu aliyeishi katikati ya karne ya kumi na tano na kumi na sita huko Ujerumani ambaye ndie aliyefichua siri za jua na mizunguko ya sayari. Ninachofikiria kufanya ni kuendeleza kile ambacho dunia imeshindwa kukigundua ambacho Johannes Kepler hakukimalizia baada ya kufa." Maneno yake yalitufanya darasa zima tuangue vicheko na hata walimu wote walimtazama na kucheka.
"Mkuu huyu mtoto sio bure ana matatizo ya akili daaah!" Mwalimu wa darasa aliongea wakati huo mwalimu wa nidhamu aliomba ruksa na kutoka nje baada ya kukaukiwa kwa kicheko. Ilikuwa kama kituko. Shule yetu ilikuwa kijijini tena kwenye nchi masikini kama Tanzania ambayo haikuwahi kufanya lolote kubwa katika upande wa sayansi. Sasa hata alichokuwa anakizungumza na kukiota German Machine sijui hata alitoa wapi tumaini la kutimiza ndoto yake. Katika karne ya 21 tena kutoka kwa mtoto wa fukara kama yeye asiyemudu kununua hata viatu vya shule? leo hii akakifanye ambacho eti wameshindwa kugundua wasomi wa dunia wenye weledi na uwezo? Tena kitu chenyewe kiwe ndani ya muendelezo wa mwanasayansi mkubwa aliyekufa zaidi ya miaka 400 nyuma? Ha ha ha haaa ama kwa hakika hata mimi nilicheka kwa mawazo yake. Lakini ajabu upande wake alikuwa makini. Hacheki zaidi ya kutushangaa tu. Inawezekana Mungu alimpa kitu tofauti ubongoni mwake. Hakika ajabu ya maneno yake ilionekana hata kwenye vitendo ingawa hakuna aliyethubutu kumuamini pale shule kama anaweza kufanya kitu chochote kikubwa.
"Kwa hiyo umesema Johannes Kepler alikuwa bingwa wa hesabu si ndio?" Mwalimu mkuu alimuuliza tena.
"Ndio mwalimu."
"Kwa hiyo vipi wewe unajua hesabu?" Swali hili lilimfanya asijibu kwa sauti zaidi ya kumtazama tu mwalimu mkuu ambae alisema.
"Sasa nataka nikupe swali moja tu. Endapo utalipatia jibu sahihi ndani ya dakika tano, naahidi nitakurudishia dikshonari yako pia nitaruhusu uitwe German Machine. Ila ukishindwa kumaliza nje ya muda basi itakuwa marufuku kwa hilo jina na ukikiuka tutakufukuza shule kabisa." Baada ya mwalimu kusema hayo, German Machine alitabasamu. Mwalimu aliandika swali la hesabu ubaoni ambalo hakika hakuna kati yetu aliyewahi kuliona toka tunaanza shule. Haikuwa hesabu ya shule ya msingi kwa kweli.
Kwa lugha nyengine niligundua mwalimu aliafanya kumkomoa ili iwe ukomo wa lile jina. Baada ya kumaliza alimpa chaki German Machine na kumruhusu aundee ubao alifanye swali husika. Kwa mara ya kwanza alituonesha maajabu. Hakuchukua hata dakika tatu. Aliujaza ubao kwa njia za kukokotoa jibu na mwishowe alilipigilia mstari jibu husika. Si mwalimu mkuu tu, bali hata mwalimu wa darasa alitoa macho.
"Twende ofisini." hiyo ndiyo kauli aliyonena mwalimu mkuu baada ya kurudishiwa chaki ili asahishe kama alipata ama amekosa.
Walimu walitoka darasani na zozo kuingia kwa wanafunzi. Mara wengine walibishana kuhusu ile hesabu kama amepata au amekosa. Wengine walijikuta wanaulizama yule mwanafunzi mgeni imekuaje afaulu kuliko wengine wakati anaonekana akili zake mbovu? Basi kila mtu alimzungumzia kivyake kwa kile alichokionesha mbele za walimu. Nusu saa baadae tulimuona akirejea darasani huku mkononi akiwa na ile 'dictionary' ya kijerumani. Hapo moyo wangu ulipiga PAA. Kila mtu alimkodolea na kubaini lazima atakuwa amepatia swali alilopewa na mwalimu mkuu.
"Jamani makofi kwa Germaaaaaaan Machine kwa kufaulu mtihani wa mwalimu mkuu!" Sauti ya TINA kibonge ilisikika darasani lakini hakuna aliyeshangilia wala kupiga makofi zaidi ya kumtazama tu.
Hapo ndipo niliposimama na kupiga dawati kama mbunge aliyekunwa na hoja huku nikilitamka jina lake kwa kuliimba.
"Geeeerman Machinee! Geeeerman Machinee! Geeerman Machine!"
Ndipo nae Tina akafanya kama mimi. German Machine alizidi kutabasamu akipiga hatua kuja dawatini alipokaa siku zote. Mithili ya uchawi mara tulimroga mmoja baada ya mwengine darasani kupiga dawati na kulitaja jina German Machine kwa pongezi. Mwishowe darasa liligeuka kuwa bunge.
Alipokaa tu nilimpa mkono na kumwambia.
"Hongera sana rafiki yangu." Alitabasamu na kushukuru. Mara wanafunzi wengi walimzonga na kutuzunguka dawatini tulipokaa.
Kila mtu alimuuliza lake huku kubwa likiwa hesabu, uwezo wake wa kuongea na siri ya kujua mengi ambayo shule hayafundishwi. Hakusema kitu kwa siku ile zaidi ya kushukuru na kutabasamu tu. Siku hiyo nakumbuka pia ndiyo ulizaliwa urafiki wetu wa kweli.
Urafiki uliopita undugu. Nilijiweka jirani yake naye alijiweka jirani yangu. Hiyo ndio ikawa siri ya kuanza kujua mengi kuhusu safari yake na ndoto zake. Kama upepo kwa haraka jina lake la ajabu lilianza kuvuma shule nzima na kwa kuongelewa na wanafunzi wakajikuta wanalikuza hadi kijijini. Tulipopata likizo ya kuwapisha darasa la saba waliokuwa wanafanya mtihani ndipo tulipoanza tabia ya kutembeleana majumbani. Kwanza nilianza mimi kufika kwao. Nyumba yao iliyochoka mwana kuchoka ikishikiliwa na miti iliyokandikwa na udongo huku nyasi zikipambwa kwenye paa. Kwao aliishi na baba yake aliyekuwa mlemavu wa mguu.
"Anhaa! mwanangu German huyu si ndieye Twaha?" Aliuliza baada ya kumuamkia babaake ambae nilishangaa na yeye anamwita mwanae German..
"Ndio na leo amekuja kupajua tunapoishi, ili tuwe tunazungumza na kujifunza pamoja."
"Hongereni wanangu. Karibu sana Twaha."
"Asante baba." Niliitika na kuingia kwenye chumba cha German Machine. Kwa mara ya kwanza nilishangazwa na kila nilichokiona kwenye kile chumba kidogo. Picha za michoro ya bendera ya ujerumani zilibandikwa kwenye kuta. Picha za watu ambao sikuwajua hata kidogo nazo zilipamba chumba chake. Nikiwa bado nachunguza ndipo niliiona picha moja kubwa ikiwa imechorwa maduara duara makubwa na madogo kwa mzunguko maalum.
"German, picha hii kachora nani?"nilimuuliza nikimuonesha ile picha yenye maduara.
"Nimechora mimi Twaha." alinijibu na kunishangaza zaidi.
"Sasa ina maana gani?" nilimuuliza huku nikiichunguza kwa umakini mkubwa.
"Hizo ni sayari Twaha. Na huo ni mzunguko wake ambao umegunduliwa na huyu hapa." Aliongea huku akinionesha picha ya kuchorwa ya baba mmoja wa kizungu.
"Huyo ndio nani?" nilimuuliza.
"Huyu anaitwa Johannes Kepler! yule niliyemzungumzia siku ile darasani." Aliponijibu niliikumbuka ile siku na kutabasamu.
"Naye ulimchora wewe?"
"Hapana Twaha, mimi siwezi kuchora watu. Picha zote za watu unazoziona zilichorwa na baba kasoro picha hizi za bendera na ramani ya michoro ya sayari na namba." Alinijibu na kunishangaza.
"Oooh! kumbe baba hodari sana wa kuchora eeh! sasa German hivi umezitoa wapi habari za huyu Johannes? hata kuelewa mambo mengi ya sayari?" Nilimuuliza huku nikiurudia ule mchoro wake.
"Twaha! maishani kuna vitu viwili tu katika hatua ya ufunuo wa kujua mambo. Kimoja kinaitwa HOFU na chengine IMANI. Hivi vitu vyote ni muhimu kuwa navyo lakini usivitumie kama vilivyo bali vitumie kinyume chake. Panapo hofu iweke imani na pengine panapo imani iweke hofu. Hiyo ndio njia ya kujua mambo hata yale ya kale." Alinambia maneno ambayo hakika sijayaelewa na kumuomba ufafanuzi.
"German maneno yako magumu sana hebu nieleweshe una maana gani? nimekuuliza kuhusu Johannes lakini!"
"Ndiyo nakujibu Twaha ili nawe upajue kule ninapojifunza mambo haya. Hofu ni adui anayeweza kukufanya uishi duniani bila kuacha faida wala kupata faida. Lakini ukimtumia kwa kinyume chake adui huyu huwa rafiki anayeweza kukufanya upambane na ufanye vitu ambavyo wasipate ufunuo ulifanyaje. Lakini pia imani ni rafiki anayeweza kukuvusha salama pale ambapo panaonekana hapavukiki. Lakini imani huyuhuyu ni adui mkubwa anayeweza kukuangusha pale panapoonekana rahisi mno kuvuka. Johannes Kepler alitumia mbinu hii ambayo hakuwahi kuiandika wala kuwaambia wengine. Ila Wapo wengi wanaamini ukiwa na hofu huwezi kushinda ila ukiamini ndipo utashinda. Lakini wewe ni rafiki yangu ukiamini hivyo utabaki kwenye kundi zuri lakini hautakuwa maalum. Hautaweza kufanya kitu kikubwa cha kujenga kumbukumbu za vizazi. Ili ufanye hivyo inapaswa kwenye haya mambo mawili uyatumie kwa umakini panapo kinyume."
"Ina maana German una maanisha pale nitapoona panatia hofu nisiiweke hofu ila niweke imani, si ndio?"
"Haswaa, vilevile pale unapoona pamejaa imani basi ili upite vyema iweke hofu hakika itakulinda. Twaha unajua kwanini watu wana imani kuwa Mungu yupo lakini wanatenda dhambi?"
"Hapana sijui." Nilijibu huku nikimtazama German Machine ambaye siku hiyo alinipa kitu ambacho sijawahi kukipata popote.
"Ni kwa sababu hii. Hawafanyi hiki ninachokwambia. Hawaweki hofu palipo imani. Kama ukiamini Mungu yupo na ukamhofia kweli, basi lazima utafaulu na utakuwa mwema kwake." Aaaah! nilijikuta natabasamu mwenyewe na kumuamini.
Ama kwa hakika urafiki tu wa German Machine ulinipa faida kubwa kuliko hata urafiki niliouweka kwa shule. Nilichokivuna kwa German Machine kilikuwa kikubwa kuliko nilichokivuna shule. Hakika ukikaa nae unaweza kufaulu mengi kwenye maisha kuliko aliyesoma. Lakini leo hii ndio hayupo! kwanini German umeenda mapemaa!
||*******||
Kumbukizi zilikatika kilio kikanishika. Sikuweza kujizuia kabisa nikajikuta nanyong'onyea miguu na kushuka chini taratibu. Watu wa huduma ya kwanza waliniwahi.

l....
 

Similar Discussions

Cookies are required to use this site. You must accept them to continue using the site. Learn more…