Sehemu ya pili....
"Unisamehe bure Twaha kwa kukuponza. Ila ukweli nitabaki kuwa German Machine hata nikifukuzwa na hapa." Alisema maneno yaliyomfanya mwalimu wa nyuma amtie konzi la kichwa na kuwafanya wanafunzi wote wakimbilie madirishani kumtazama kwa nje alivyokuwa anapelekwa ofisini msobe msobe.
Nilistaajabu kwa ujasiri aliouonesha kutetea jina lile hadharani pasipo kuogopa.
Hapo ndipo nilipoijenga shauku na hamu ya kumjua kiundani mwanafunzi huyu ni nani haswa na kwanini anajiita hivyo hata awe radhi kufukuzwa shule lakini si kubadili jina? Ilikuwa ni tukio la ajabu la kwanza kuliona kwake.
Aaaah! German Machine...! ama kweli maneno huumba.
Kilichotokea ofisini hakuna aliyejua pale darasani. Mzozo ukaibuka kila mtu akimzungumzia vile alivyoweza baada ya kituko kile. Binafsi nilikuwa bado naugulia maumivu ya fimbo. Sikutaka kujiunga kwenye vikundi vilivyozua mjadala darasani huku wengine wakicheka na kushangaa. Hadi unafika muda wa kuondoka shule sikumuona hata mstarini siku ile.
Ilikatika wiki nzima hakuja shule. Wiki ya pili asubuhi na mapema tulimuona akiwa ameongozana na mzee mlemavu wa mguu mmoja. Kimtazamo tu ilitosha kumtambua kama alikuwa baba yake kwa jinsi walivyofanana. Nilipita jirani yao na kumsalimu yule mzee huku nikitazamana na German machine ambae alikuwa kavaa sare kuukuu.
"Twaha, huyu ndie baba yangu. Baba huyu ndie yule mwanafunzi niliyekwambia." Utambulisho wake sikuuelewa haraka. Niliwaacha na kuelekea darasani kipindi wao wakielekea ofisini kwa mwalimu mkuu. Ilikuwa tayari kituko chake kilishaenea shule nzima.
"Yule ndie ameandika majina ya kihuni kwenye madaftari, naona amekuja na mzazi wake." Minong'ono ilisikika kwa baadhi ya wanafunzi waliomuona. Laiti vidole vingekuwa risasi basi vingemjeruhi siku hiyo kama si kumuua. Hatukujua nini kiliongeleka huko ofisini lakini baadae tulimshuhudia German Machine akirejea darasani kwa mara nyengine.
"Nisamehe Twaha kwa siku ile." Alinambia wakati akikaa dawatini. Nilimtazama kwa hasira kidogo nikamwambia.
"Kama unataka nikusamehe, simama mbele ya darasa na ututajie jina lako la kweli." Niliitoa kauli kwa sauti ya juu na kila mtu darasani alisikia. Wengi waligeuka kumtazama na wengine wakimcheka na kukazia ataje jina lake la kweli. Alinitazama akiwa mwingi wa tabasamu. Kwa kweli alikuwa na moyo wa kushangaza sana. Ndipo akaenda mbele ya darasa akasimama na kusema.
"Naomba mjue jamani. Jina zuri ni lile utapoitwa likaitikwa ndani ya moyo wako hata usiponyanyua mdomo na kutoa sauti. Si vyema jina likafasiriwa bila utashi wa mtu. Kumbukeni kuwa jina halina uhai ila kupitia uhai wako unaweza kulifanya jina likaishi milele. Jina linaloitikwa na moyo wangu ni German Machine." Baada ya kuongea hayo alitoka pale mbele kurejea dawatini. Wanafunzi walimzomea kwa maneno yake na wengine waliangua vicheko. Binafsi nilizidi kumuona ni mtoto wa ajabu. Muonekano wake na vitendo vyake vilikuwa tofauti sana.
"Twaha naomba urafiki nawe tafadhali wewe ni jirani yangu usiwe kama wengine." Alinambia aliporudi kukaa huku akininyooshea mkono. Nilishindwa kumpa mkono zaidi ya kumtazama tu. Hakujali alikaa na kuanza niongelesha ingawa sikumuonesha ushirikiano.
"Naamini mtu mzuri ni yule anayeonesha hisia zake hadharani. Haijalishi ziwe nzuri ama mbaya. Twaha, tunapaswa kuipambania amani ndani ya nafsi zetu kwanza hata kama itatugharimu vipi. Amani ya nafsi yangu ni kuwa German Machine. Vipi wewe ipi amani ya nafsi yako? Je ushaipata ama unaishi kwa kuhofia wengine?" Aliniuliza lakini sikumjibu kitu zaidi nilimuhama pale alipokaa. Akilini sikumtilia maanani kivile wala sikuwahi weka dhana kama anaweza kuja kuwa mtu muhimu. Kila mtu alimdharau darasani. Hakuwa na rafiki hata mimi niliyekaa naye dawati moja 'nilimchunia'. Lakini hali hiyo haikumfanya anune wala kumkasirikia mtu.
Nakumbuka siku chache mbele tulifanya mtihani wa jaribio la mwezi kabla hatujawapisha shule darasa la saba ambao walikuwa wanajiandaa na mtihani wa taifa. Siku hiyo tena aliingia mwalimu mkuu darasani kwetu akiwa na mwalimu wa darasa sambamba na mwalimu wa nidhamu. Mwalimu mkuu alibeba karatasi tulizofanyia jaribio baada ya kusahishwa. Nakumbuka zilikuwa ni karatasi za mitihani mitatu. Hisabati, Kiingereza na Sayansi.
"Twaha!" Mwalimu wa darasa aliniita pindi walipokuwa wamesimama mbele huku darasa likizizima utulivu.
"Naam mwalimu." Niliitika na kusimama.
"Nenda kakate fimbo nzuri sita za m'biriti ulete hapa haraka." Aliniagiza nami nilitoka nje haraka kwenda timiza wajibu.
"Mh! sijui kina nani leo wanawashwa mboko." Nilijiuliza kipindi hiko nikiwa nje ya darasa tayari nikiuelekea mti mkubwa ulioitwa M'biriti ili niweze kuvunja bakora. Nilirejea na kuzikabidhi. Hapo ndipo tulipoamriwa wote tusimame. Tulitii huku kila mmoja moyo ukimpwita kusubiri kuona kifuatacho.
"Juma Zakaria!"
"Nipo."
"Zuwena Ali"
"Nipo."
"Christina Agustino." Aliita majina mwalimu mkuu kupitia karatasi za mitihani aliyoishika. Kila aliyeenda kupokea mtihani wake aliamriwa akae. Zoezi hilo lilifanyika na kujikuta sote tukikaa chini kasoro mwanafunzi mmoja ambaye alikuwa bado hajapata mitihani yake. Hakuwa mwengine bali yuleyule tuliyemuona kama kituko cha shule. German Machine! alibaki amesimama peke yake. Lakini Mkononi mwalimu alionekana kubakiwa na karatasi tatu pia alikuwa na ile 'dictionary' ya kijerumani.
"Wewe mbona bado umesimama?" Mwalimu wa darasa alimuuliza.
"Sijapata mitihani yangu mwalimu." alijibu.
"Unaitwa nani?" Mwalimu mkuu alidakia huku akimkazia macho. Darasa zima tuligeuza vichwa kumtazama huku tukiyatega masikio.
"German Machine." Alitoa jibu lililotufanya tuachame midomo na kumshangaa mno. Hakika ilikuwa si kawaida kwa mtoto kama yeye kuongea kwa sauti ya kujiamini mbele za walimu tena swali la mwalimu mkuu. Mwalimu mkuu alitikisa kichwa kwa kumsikitikia wakati huo mwalimu wa nidhamu alibaki akimtazama kama hamuoni. "Kuja mbele haraka piga magoti." Aliongea kwa ghadhabu mwalimu wa darasa. Na kweli bila kuhoji alitii agizo, alipiga magoti mbele ya darasa.
"Wenzenu wanaingia kuanza mitihani mwezi ujao. Ninyi ndio darasa la saba kwa sasa. Wale wanakamilisha tu ratiba. Sasa sijajua kwanini mnazembea kwenye mitihani mepese kama hii. Twaha uwezo wako unashuka siku baada ya siku. Bahati nawe bado maji kupwa maji kujaa. La sita mnashangaza sana yaani mtu aliyejitahidi kwenye hii mitihani ni mmoja tu lakini naye amekuwa sifuri. Ameharibu kitu kidogo sana kisicho na faida. Laiti kama angeandika jina lake halisi kwenye mtihani basi ndie alikuwa amewaongoza kwenye jaribio hili. Lakini amerudia yale yale aliyoyafanya wiki chache nyuma. Eti sehemu ya jina la mwanafunzi kajaza GERMAN MACHINE Sasa hali hii inaweza kutokea hata kwenye mitihani ya taifa na kujikuta unafutiwa matokeo. Eti we kijana mdogo una matatizo gani labda tukusaidie maana baba yako hadi chozi lilimtoka ili nikuache usome uhitimu hapa. Sasa kwa tabia hii unataka kuionesha wizara kama shule yetu tunafundisha uhuni? Mbona ripoti zako za uhamisho hakuna sehemu iliyojazwa hili jina la ajabu? eeh! unaweza kutujibu na wenzako wasikie?" Sauti ya mwalimu mkuu ilirindima darasani. Sote tulibaki kimya. Macho na masikio tulimtupia yeye tupate kusikia kwanini anajiita 'German Machine'.
"Mwalimu, naamini msema kweli ni mzuri mbele za Mungu ingawa ukweli wake unaweza kumfanya aonekane m'baya mbele za watu. Kweli German Machine si jina nililopewa siku nazaliwa wala sijaandikishwa shule kwa jina hili. Lakini hili ni jina linalosikiwa vyema na moyo wangu. Jina linasafiri ndani ya ndoto zangu. Naamini naweza kufanya mengi makubwa kwa changamoto ya jina hili. Nimejipa mwenyewe hili jina na moyo wangu hauko tayari kuliacha. Naomba mnisamehe sina chaguo." Aliongea na kumfanya mwalimu mkuu akae juu ya dawati kwa umakini akaendelea kumhoji.
"Sasa kwanini usingejita Tanzania Machine hadi ujiite German. Kwani wewe ni mzungu? na vipi kuhusu hii dikshonary ya kijerumani wapi uliitoa na kwanini?"
"Mwalimu. Tanzania ni nchi yangu kiasili na siwezi badilisha lakini ujerumani ni nchi ya ndoto yangu. Naipenda tu ila sina lugha rasmi ya kuuzungumzia upendo kwakuwa ni kitu maalum sana kinachotokea chenyewe ndani ya moyo. Kuhusu hiyo dikshonary nilipewa na baba."
"Na baba yako? yupi yule mzee uliyekuja naye?"
"Ndio mwalimu. Amefanikiwa kuitunza kwa miaka mingi."
"Mh! sasa sikiliza. Nakupongeza kwa majibu yako ya kujiamini lakini nasikitika kukwambia kuwa bado huna upeo wala weledi wa kuongea maneno ya msingi. Umefanya vizuri kwenye mitihani ila umeshika mkia kwa ujinga uliouandika." Aliongea mwalimu mkuu na kauli yake ilikatizwa na ya mwalimu wa nidhamu.
"Sikiliza niwaambie la sita. Kila mtu anaupendo na kitu fulani ama nchi fulani. Lakini hebu jiulizeni kama kila mtu angeacha asili ya jina lake na kujiita majina ya vile avipendavyo ingekuwaje? Mfano mimi naipenda sana China sababu napenda mazoezi, halafu nijiite China Machine? eeh! haya mwengine anaipenda mfano timu ya mpira kama Simba au Yanga. Kwa hiyo nae ajiite Yanga machine? ha ha ha hiko kitakuwa kituko ambacho huwezi kueleweka popote na utajikuta unakosa vitu vingi vya msingi. Nakusihi nawasihi na wengine wenye kujipa majina ya a.k.a kwamba msiyatumie kama majina rasmi hasa kwenye mambo ya msingi kama haya. Leo hii tumekufutia matokeo japo umefanya vizuri jua huu ni mfano ambao unaweza kukukuta hata kwenye mtihani wa taifa. Utajikuta umeubomoa msingi wa maisha yako kwa sababu ya ujinga tu." Alinyamaza mwalimu wa nidhamu. Nilimshuhudia machozi yakimtoka German Machine akiwa bado amepiga magoti.
Hakika nilijikuta nikimuonea huruma kwa mara ya kwanza. Maneno yake ingawa walimu walisema ni ujinga mtupu lakini nilihisi yamenigusa kwa namna moja. Aaaaah! German Machine!
||******||
Kumbukizi za miaka kumi na mbili zilizidi nitoa machozi. Niliikumbuka sana ile siku ambayo niliamini ndio ingekuwa ya mwisho kulitumia lile jina. Niliumia sana nilipowatazama wale askari wakilieka jeneza lililobeba mwili wa German Machine sehemu maalum iliyoandaliwa. Nilitamani utokee muujiza aamke ama kile kinachoendelea kigeuke ndoto. Aaaah! lakini haikuwezekana. Bwana ametoa na bwana ametwaa. Hatuna budi kulihimidi jina lake.
Nilichukua leso kupunguza machozi yaliyokuwa hayakomi kunichuruza usoni. Ndipo muda ule nilipotazama vizuri eneo la jukwaa la mbele karibu na jukwaa kuu kuna mtu nilimuona. Aaaah! moyo wangu ulifarijika kwa kuwa alikuwa kwenye kumbukizi zangu muda mfupi. Nilijua kiasi gani alijitahidi kulipinga jina la German Machine lakini leo hii naye amekuwa miongoni mwa waombelezaji walioshika bendera za Ujerumani na Tanzania akimlilia mtu ambaye alimjua tokea anaanza kufukuzia ndoto zake. Nilimtazama na kutabasamu nikiwa katikati ya huzuni. Hakuwa mwengine yule mtu bali mwalimu Kisayo. Mwalimu wa kwanza shuleni kumpiga na kumfikisha ofisini baada ya kukuta daftari la somo lake limeandikwa jina GERMAN MACHINE.
....