MAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI
YAH: HUJUMA ZA BARAZA LA MITIHANI DHIDI YA WAISLAM Kila sifa njema anastahiki Allah, ambaye rehema zake zimeenea katika kila kitu katika ulimwengu bila ya kujali utii ama uasi wa kitu hicho katika amri na sharia zake. Rehema na amani zimuendee kipenzi chetu mtume Muhammad (S.A.W) kwa kuwa kiigizo chema na rehema kwa walimwengu wote. Ndugu waandishi kwa muda mrefu waislam wamekuwa wakiilalamikia suala zima la utendaji wa serikali kuwa umekuwa wakibaguzi kwa kuwapendelea wakirsto kwa kuwapa nafasi mbalimbali muhimu serikalini na katika taasisi zake. Ndugu waandishi na Waislam mnamo tarehe 01/ 05/2012 Baraza la mitihani la Tanzania lilitangaza matokeo ya kidato cha Sita, matokeo hayo yaliwashtua sana wanafunzi waislam waliofanya mtihani wa elimu ya dini ya kiislam (Islamic Knowledge). Takriban asilimia 70 walifeli kwa kupata daraja F, na asilimia 30 ndio waliofaulu tu. Katika hao waliofaulu walipata alama za juu kabisa nchi nzima ni wanafunzi saba tu ambao wamepata daraja D, kwa matokeo haya somo hili likawa somo la mwisho kwa ufaulu nchi nzima (rejea kitabu cha takwimu cha Baraza la mitihani Tanzania April 2012.
Matokeo haya yaliwashtua wazazi na walimu wa somo hili, baadhi ya wanafunzi waliamua kukata rufaa ya kutokubaliana na matokeo hayo.
Waislam kupitia Taasisi mbali mbali za kiislam walimuandikia katibu mkuu wa wizara ya elimu na mafunzo ya ufundi kumuomba aunde tume huru kuchunguza matokeo ya somo husika.
Kufuatia malalamiko hayo ya baadhi ya taasisi za dini, baraza la mitihani liliyatazama matokeo hayo na kugundua pia walikosea na hivyo Baraza la mitihani likaidhinisha kutolewa matokeo mapya kwa somo hilo.
Mabadiliko hayo ya matokeo ufaulu kwa wanafunzi wale wale ambao awali walifeli kwa asilimia 70, sasa yakabadilika na ufaulu ukaongezeka kwa zaidi ya asilimia 70.
Kwa namna yoyote ile itakavyokuwa dosari kubwa kama hii ni kashfa kubwa kwa Baraza la mitihani Tanzania na Serikali kwa ujumla. Na kwa kutilia maanani muundo na historia ya utendaji wa wa baraza la mitihani la Tanzania kama nilivyoanza kuelezea, Waisla wanayokila sababu ya kuamini kwamba matokeo haya ni uthibitisho tosha wa hujuma ambazo wanafunzi wa kiislam walikuwa wakifanyiwa kwa muda mrefu. Na hii inatupa picha kwamba dosari hizi zilizotokea kwenye somo la maarifa ya kiislam, haziishii kwenye somo hili, bali uchunguzi ukifanyika kwa masomo yote waliofanya wanafunzi wa kiislam itadhihirika kwamba hila na dhulma kama hizi zinafanyika katika masomo mengine.
Kimsingi kwa dhulma hii waliyoifanya baraza la mitihani dhini ya wanafunzi wa kiislam, Bakwata na waislam wote kwa ujumla wamepoteza imani na baraza la mitihani la Tanzania na hasa katibu mtendaji wake . Bakwata, linawapongeza na kuwaunga mkono Taasisi zote za kiislam nchini kwa jitihada ya kuligundua hili na hatua walizozichukuwa dhidi ya baraza la mitihani na kuhufahamisha umma wa kiislam juu ya kadhia hii.
Tunarudia baraza tunawapongeza taasisi zote za kiislam na tunasema katika hili Bakwata tuko nyuma yao kwani kauli yao ndio kauli yetu.
Bakwata, inamshangaa Katibu mtendaji wa Baraza la mitihani (Necta) Dk. Joyce Ndalichako, kwa kauli yake aliyoitoa kupitia vyombo mbali mbali vya habari vya jana tarehe 5/06/2012, akisema hakuna hujuma na mitihani inasahihishwa na walimu wenye sifa,wanachaguliwa na na wakuu wa shule zao, walimu wenye uzoofu na kuna mfumo wa usahihishaji aliohuita "Conveyor Belt".
Bakwata inasema hapa tatizo la msingi sio mitihani kusahihishwa na walimu wenye sifa,na nani anawachagua walimu hao wenye sifa au huo mfumo wa usahihishaji,
tatizo la msingi hapa ni kufelishwa kwa makusudi kwa wanafunzi wetu wa kiislam katika somo husika, wakati nakala za mitihani yao (Scripts) zinaonyesha wamefaulu.
Bakwata, tunahoji kwanini tatizo hili la huo mfumo (Conveyor Belt) litokee mwaka huu, mbona matokeo ya mwaka jana waislam hawakulalamika na kulikuwa hakuna dosari kama za mwaka huu iweje itokee mwaka huu, wakati mfumo ni ule ule?
Bakwata, tunaamini waislam katika hili tumehujumiwa na waislam hawajaridhishwa na majibu ya Dk. Ndalichako, aliyoyatoa kupitia vyombo vya habari vya hapa nchini.
Hiyo mifumo ya usahihishaji sio maneno matakatifu kwamba haiwezi kuchezewa kutokana hila za binadamu ni mifumo iliyowekwa na binadamu, na binadamu huyohuyo anaweza kuibadilishabadilisha vyovyote anavyotaka. Sisi kama Bakwata,tunaamini ili kurudisha imani ya waislam dhidi ya Baraza la mitihani tunataka mambo yafuatayo yafanyike,
· Tume huru iundwe la kuchunguza Baraza la mitihani la Tanzania na utendaji wake wa kazi kwa kipindi cha miaka kumi iliyopita.
· Katibu mkuu wa baraza la mitihani (Necta) ajiuzulu mara moja ili kulinda heshima ya serikali ya jamuhuri ya muungano wa Tanzania na Baraza la Mitihani.
· Watendaji wakuu wa kitengo cha mitihani na wanaohusika na mfumo wa kompyuta ya Baraza la mitihani nao wawajibishwe mara moja.
· Hatua za kisheria na kinidhamu zichukuliwe dhidi ya watumishi wa baraza la mitihani watakaothibitika kuhusika na kashfa hii.