Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA) imewataka wadau wa sekta ya usafiri wa anga kuimarisha maandalizi na utayari kukabiliana na athari zinazoweza kujitokeza katika msimu wa mvua 2026/2027, kufuatia utabiri wa Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) unaoashiria uwezekano wa kutokea kwa El Nino, mvua kubwa au za wastani, upepo mkali na mafuriko.
Wito huo umetolewa kupitia barua ya TCAA ya Oktoba 6, 2026, iliyosainiwa na Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Dkt. Jabiri K. Bakari.
TCAA imewataka waendeshaji wa ndege na watoa huduma za usafiri wa anga kufanya au kuboresha tathmini za majanga, kuimarisha mipango ya dharura na mwendelezo wa shughuli, pamoja na kuhakikisha viwanja vya ndege, miundombinu, vifaa muhimu na mifumo ya akiba iko tayari.
Mamlaka pia imeelekeza kupewa kipaumbele hali ya maeneo ya kutua na kurukia ndege, mifumo ya mifereji ya maji, mafuriko, ngurumo, upepo unaobadilika ghafla, mifumo ya mawasiliano na huduma za usalama, pamoja na upatikanaji wa taarifa za hali ya hewa na tahadhari kwa wakati.
TCAA imesisitiza umuhimu wa ushirikiano na utoaji wa taarifa kwa wakati miongoni mwa wadau wa sekta ya anga ili kupunguza athari kwa usalama na mwendelezo wa shughuli za usafiri wa anga.
Wadau wote wametakiwa kuwasilisha TCAA tathmini za majanga, mipango ya kukabiliana na dharura na ushahidi wa hatua za maandalizi ifikapo Oktoba 15, 2026. TCAA itafuatilia utekelezaji wa hatua hizo na kufanya uhakiki maalum wakati wa msimu wa mvua.