Mada maalum ya ndege toka FB

Mada maalum ya ndege toka FB

Serikali ya Marekani kupitia Wizara yake ya Mambo ya Nje imeidhinisha mpango wa uwezekano wa kuiuzia Saudi Arabia ndege 48 aina ya Lockheed Martin F-35A Lightning II, katika mkataba unaokadiriwa kuwa na thamani ya dola bilioni 24.3 za Marekani.

Mpango huo unafanyika kupitia mfumo wa Foreign Military Sales (FMS), huku kifurushi hicho kikijumuisha pia injini 49 pamoja na vifaa na huduma zinazohusiana na ndege hizo.
Hata hivyo, uuzaji huo bado unahitaji kukamilisha mchakato wa idhini wa Bunge la Marekani kabla ya makubaliano kukamilishwa.

Iwapo utatekelezwa, mpango huo utaifanya Saudi Arabia kuwa miongoni mwa waendeshaji wa ndege za kivita za F-35 katika Mashariki ya Kati.
Kwa sasa, Israel ndiyo nchi pekee katika eneo hilo inayotumia F-35.

F-35A Lightning II ni ndege ya kivita yenye uwezo wa kujificha (stealth) iliyoundwa kwa ajili ya kufanya operesheni mbalimbali za anga, ikiwemo mashambulizi ya ardhini na ulinzi wa anga.

Uamuzi huo wa Marekani unatajwa kuwa sehemu ya kuimarisha ushirikiano wa kiulinzi kati ya Washington na Riyadh, wakati ambapo hali ya usalama katika Mashariki ya Kati ikiendelea kuwa tete.View attachment 3675443
 
Kimbunga Dujuan kimesababisha usumbufu mkubwa wa usafiri wa anga na nchini Japani baada ya kuleta mvua kubwa na upepo mkali kwenye pwani ya mashariki.

Mashirika makuu ya ndege yamelazimika kufuta mamia ya safari katika viwanja vya ndege vya Haneda na Narita jijini Tokyo, hali iliyoathiri maelfu ya abiria.

Mamlaka ya Hali ya Hewa ya Japani imetoa tahadhari kubwa ya mafuriko na maporomoko ya udongo kwa maeneo ya Kanto na Tokai kutokana na kiwango kikubwa cha mvua kilichorekodiwa ambacho kinajaza mito kwa kasi.

Mbali na usafiri wa anga, huduma za treni za mwendokasi na za kawaida zimesimamishwa au kupunguzwa katika maeneo kadhaa karibu na Tokyo ili kulinda usalama wa abiria.

Athari za kimbunga hicho zimeenda mbali zaidi ya sekta ya usafiri, kwani maelfu ya nyumba katika mkoa wa Chiba zimebaki bila umeme baada ya upepo mkali kukata nyaya za nishati hiyo.

Matukio makubwa ya kijamii, ikiwemo siku ya mwisho ya maonyesho makubwa ya michezo ya video ya Tokyo Game Show na matamasha ya nje, yamefutwa kabisa huku wananchi wakishauriwa kusalia majumbani na kufuatilia taarifa mpya za usalama kutoka kwa mamlaka husika.
1790050978132.jpg
 
Chuo cha Usafiri wa Anga Tanzania (CATC) kimeendesha mafunzo ya Utambuzi wa Tabia (Behaviour Detection) yanayodhaminiwa na ICAO, kwa lengo la kuimarisha ujuzi wa wataalamu wa usalama wa anga.

Mafunzo hayo yanafanyika katika Kituo cha Mafunzo ya Usalama wa Anga (ASTC), Dar es Salaam, kuanzia Septemba 21 hadi 25, 2026, yakishirikisha wataalamu 15 kutoka Tanzania, Kenya, Rwanda, Nigeria, Angola, Eswatini na Uswisi.

Akifungua mafunzo hayo, Mkuu wa CATC, Aristid Kanje, amesema programu hiyo ni muhimu katika kuwajengea wataalamu uwezo wa kutambua mienendo inayoweza kuhitaji uangalizi zaidi, huku wakizingatia weledi, haki za binadamu na taratibu za usalama wa anga.

Mafunzo hayo ni sehemu ya juhudi za ICAO na CATC katika kujenga uwezo wa wataalamu na kuimarisha viwango vya usalama wa anga kwa mujibu wa miongozo ya kimataifa.
1790051711164.jpg
 
Airbus Helicopters imezindua jukwaa jipya la helikopta inayojiendesha yenyewe bila rubani inayojulikana kama U145, ambayo imetokana na muundo wa helikopta ya kijeshi ya H145M.

Helikopta hii imeundwa maalum kwa ajili ya kusafirisha mizigo mizito ya vifaa vya kijeshi na kufanya operesheni hatari kwenye mazingira ya adui bila kuweka maisha ya marubani hatarini.

Katika mabadiliko makubwa ya kiteknolojia, Airbus imeondoa mifumo ya kawaida ya usukani na kuweka mifumo ya kisasa ya kielektroniki, huku nafasi ya ndani ya chumba cha rubani ikiondolewa ili kutengeneza sakafu tambarare inayoruhusu uingizaji rahisi wa mizigo kutoka pande zote.

Kulingana na meneja wa mpango huo Constance Pinsdorf, majaribio ya kwanza yataanza mwishoni mwa mwaka huu wa 2026 kwa kutumia teknolojia mseto, yakifuatiwa na majaribio rasmi ya ndege hiyo bila rubani ifikapo mwaka 2028, huku uzalishaji wa jumla ukitarajiwa kuanza mapema miaka ya 2030.
1790079950742.jpg
 
Ndege hii aina ya Short SC.7 Skyvan 3M-100 inayomilikiwa na Jeshi la Polisi la Malawi ikiwa na usajili wa 7Q-YAY ilikumbwa na ajali mnamo tarehe 24 Aprili 1986 nchini Kenya.

Wakati ikikaribia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Moi mjini Mombasa ikitokea Lilongwe, Malawi, ndege hiyo ilipata hitilafu kubwa baada ya injini zote mbili kuzima ghafla kutokana na kuishiwa na mafuta.

Hali hiyo iliwalazimu marubani kufanya kutua kwa dharura nje ya uwanja wa ndege, ambapo walilazimika kuishusha ndege hiyo kando ya barabara takriban kilomita 18 kusini-magharibi mwa uwanja wa Mombasa na kupelekea kugonga miti wakati wa kutua.

Licha ya uharibifu mkubwa uliojitokeza kwenye ndege yenyewe, wafanyakazi wote wawili waliokuwemo ndani walinusurika salama bila kupoteza maisha.
1790195545790.jpg
 
Ndege ya serikali ya Irani aina ya Airbus A340-311 (EP-IGI) iliyobeba ujumbe wa Irani kwenye Mkutano Mkuu wa 81 wa Umoja wa Mataifa, ilianza safari kutoka Tehran, Irani mnamo tarehe 22 Septemba 2026.

Ndege hiyo ilipitia anga ya Uturuki, Ugiriki na Italia, kabla ya kuvuka Bahari ya Mediterania na kutua Algiers, Algeria, kwa ajili ya kusimama kwa muda wa kiufundi.

Baada ya takribani saa mbili, iliendelea kupitia anga ya Hispania na kuvuka Bahari ya Atlantiki ya Kaskazini kuelekea Marekani.

Hatimaye ilitua Uwanja wa Ndege wa John F. Kennedy (JFK), New York, kabla ya kuhamishiwa Baltimore/Washington International Airport (BWI), ambako ndege hiyo itabaki wakati wa shughuli za Mkutano Mkuu wa Umoja wa Mataifa.
1790195758145.jpg
 
Kishindo kikubwa cha ndege mbili za kivita aina ya B-1 Lancer kilitetemesha uwanja wa kijeshi wa Joint Base Andrews, na kutengeneza taswira ya kipekee wakati Rais wa Marekani Donald Trump alipomfanyia mapokezi ya nadra Rais wa China, Xi Jinping.

Ndege hizo za kimkakati zenye mwendokasi (supersonic bombers) zilipita chini kabisa angani juu ya viongozi hao kama sehemu ya onyesho la kijeshi la kukaribisha ujumbe wa China.

Wakati ndege hizo ziliporuka kwa kasi juu ya zulia jekundu, sauti hiyo ya ghafla ilimfanya Rais Trump ashtuke ghafla na kujikunja uso kwa sekunde kadhaa akitazama juu kana kwamba sauti hiyo ilikuwa inamuumiza masikio.

Tofauti na Trump, Rais Xi Jinping alibaki thabiti na kutazama ndege hiyo kwa utulivu bila kushtuka, huku ndege hizo zikiacha mwangwi mzito uwanjani hapo unaoashiria nguvu kubwa ya anga ya jeshi la Marekani.
1790227736390.jpg
 
Helikopter Service ilikuwa kampuni ya Norway iliyoweka historia kwa kutumia helikopta kubwa za kibiashara za Boeing Vertol 234 ambazo ni toleo la kiraia la helikopta maarufu ya kijeshi ya CH-47 Chinook.

Katika miaka ya 1980, kampuni hiyo ilinunua helikopta hizi tatu maalum kwa ajili ya kuhudumia sekta ya mafuta na gesi kwenye bahari ya kaskazini pamoja na kubeba mizigo mizito ya miundombinu maeneo ya milimani kote Ulaya.

Helikopta hizi zilikuwa na uwezo wa kipekee wa kubeba mzigo wa nje wa hadi kilo 11,800 (Tan 11.8) kwa kutumia kamba maalum kwa sababu ya muundo wake wa propela mbili kubwa zinazozunguka pande tofauti na kufanya nguvu zote za injini kutumika kwenye kunyanyua uzito pekee bila kupoteza nguvu kwenye mkia.

Baadaye mnamo mwaka 1995, kampuni hiyo iliuza helikopta hizo kwa kampuni ya Columbia Helicopters ya nchini Marekani ambayo inaendelea kuzitumia hadi sasa kwa kazi za kuzima moto na kubeba mizigo mizito duniani.
1790243271272.jpg
 
Picha hii inaonyesha njia ya ajabu ya ndege iliyorekodiwa kupitia programu maarufu ya kufuatilia safari za anga ya Flightradar24.

Rubani wa ndege ndogo aina ya Cessna Skylane RG yenye namba ya usajili N1810R alitumia saa kadhaa angani kuchora alama kubwa ya kidole (Finger Print) iliyoambatana na ujumbe wa upendo unaosema "YOU are Loved".
Tukio hili lilifanyika angani karibu na mji wa Bentonville, Arkansas nchini Marekani.

Rubani huyo anafahamika mitandaoni kwa jina la "The Pilot Picasso", msanii wa uchoraji anayetumia ramani za GPS kupanga njia zake kwa umakini mkubwa kabla ya kupaa angani ili kueneza jumbe aliyokusudia.
1790267476474.jpg
 
Serikali ya China imeweka chini ya ulinzi vipuri nyeti vya ndege ya kivita ya Marekani ya F-35 baada ya shehena iliyotokea nchini Australia kuelekezwa kimakosa hadi Hong Kong.

Tukio hili limezua hofu kubwa za kiusalama na uchunguzi wa bunge nchini Washington kuhusu uwezekano wa China kufikia teknolojia hiyo ya siri ya kijeshi.

Shehena hiyo iliyokuwa na kifuniko cha chumba cha rubani na mlango wa sehemu ya kuhifadhia silaha kutoka kwenye ndege ya jeshi la anga la Australia, ilisafirishwa mwishoni mwa mwezi Mei 2026.

Lengo lilikuwa ni kuvifikisha vipuri hivyo nchini Marekani kwa ajili ya matengenezo na ukaguzi kupitia kampuni ya usafirishaji ya UPS kwa niaba ya mkandarasi Lockheed Martin.

Hata hivyo, baada ya ndege hiyo kuwasili kituo kisichotarajiwa nchini Korea Kusini, ilielekezwa Hong Kong ambako maofisa wa China walivikamata vipuri hivyo, na mpaka sasa havijarudishwa.

Sehemu zote mbili za vipuli vilizokamatwa zimepakwa mchanganyiko maalum wa rangi za siri zinaofyonza miale ya rada ili kuifanya ndege hiyo isionekane kwa urahisi, jambo linalozidisha wasiwasi wa kiintelijensia kwamba China inaweza kuvifanyia utafiti wa kisayansi ili kunakili teknolojia hiyo.

Wakati maofisa wa usalama wa Marekani wakionyesha wasiwasi mkubwa na kuanzisha uchunguzi wa kina kuhusu udhaifu wa ugavi wa kijeshi, Waziri wa Ulinzi wa Australia, Richard Marles, amepunguza ukubwa wa athari hizo akidai kuwa vipuri hivyo vilikuwa vimeharibika na haviwezi kutumiwa kirahisi kwa madhumuni ya kijeshi.

Kampuni hiyo ya usafirishaji inaripotiwa kuwa hapo awali ilishirikiana na kampuni iliyowekwa kwenye orodha nyeusi kwa kuhusishwa kuwa na mawasilano na jeshi la China.
1790269509341.jpg
 
Rais wa China, Xi Jinping, amewasili nchini Marekani kwa ndege yake aina ya Boeing 747, iliyotua katika Kambi ya Pamoja ya Andrews.

Katika maandalizi ya mapokezi na ulinzi wa hafla hiyo, ndege za kijeshi aina ya F-16 na F-22 Raptor zilipangwa na kuegeshwa uwanjani, huku ndege mbili za aina ya B-1 zikifanya safari ya maonyesho angani.

Uwepo wa ndege hizo za kijeshi uliongeza taswira ya kijeshi katika hafla hiyo.

Aidha, mizinga ilipigwa kwa heshima, huku vikosi vya kijeshi vikiwa katika mpangilio rasmi wa mapokezi.

Bendera za China na Marekani ziliwekwa katika eneo hilo, zikionyesha hadhi ya tukio hilo la kidiplomasia.

Kivutio kingine kilikuwa zulia jekundu lenye urefu wa takribani mita 100, lililowekwa kutoka kwenye ndege ya Rais Xi Jinping hadi eneo la mapokezi.

Mchanganyiko wa heshima za kijeshi, ndege za kivita, saluti za mizinga, bendera za mataifa hayo mawili uliifanya safari hiyo kuwa na taswira ya kipekee na isiyo kawaida katika historia ya Marekani kwa zaidi ya miaka 50.
1790270845463.jpg
 
 
 
Huduma za wasafiri wanaotumia ya jengo la watu mashuhuri la "Uhuru VIP Terminal" katika Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA) zimeendelea kupewa msisitizo kupitia matumizi ya magari maalum ya huduma za VIP yanayowaunganisha abiria moja kwa moja kati ya ndege na kituo hicho.

Kwa mujibu wa taarifa iliyochapishwa na Miracle Concierge, huduma hiyo inahusisha usafiri wa abiria kwa magari ya kifahari zikiwemo Mercedez Benz, ndani ya eneo la airside, pamoja na huduma binafsi za kuwahudumia wageni na kusaidia kuratibu mizigo katika hatua mbalimbali za safari.

Kwa abiria wanaowasili, wageni hupokelewa mara baada ya kushuka kwenye ndege na kusafirishwa kwa magari hayo kutoka kwenye ndege hadi Uhuru VIP Terminal.
Kwa upande wa wanaoondoka, abiria husindikizwa kutoka kituoni hadi kwenye ndege kwa kutumia magari hayo maalum wakati wa kujiandaa kupanda ndege.

Huduma hiyo inalenga kuhakikisha mchakato wa abiria kutoka terminal kwenda kwenye ndege au kutoka kwenye ndege kwenda jengo (terminal) unafanyika kwa urahisi, faragha na kwa uratibu maalum, ikiwa ni sehemu ya kuongeza kiwango cha huduma za wasafiri wanaotumia huduma za VIP katika KIA.
1790306521507.jpg
 
Kampuni ya Bell imeanza uzalishaji wa helikopta za mashambulizi aina ya AH-1Z Viper kwa ajili ya Jeshi la Anga la Nigeria (NAF), kupitia mpango wa Marekani wa Foreign Military Sales (FMS).

Ujumbe wa Nigeria ulitembelea kiwanda cha Bell jijini Amarillo, Texas, ambako ulipewa nafasi ya kutembelea eneo la uzalishaji na kutia saini kwenye fremu ya helikopta ya kwanza inayotengenezwa kwa ajili ya Nigeria.

Kwa mujibu wa msemaji wa NAF, Air Commodore Ehimen Ejodame, Nigeria inatarajia kutumia AH-1Z Viper kama moja ya majukwaa muhimu katika uwezo wake wa helikopta za mashambulizi, huku ikisisitiza uwezo wake wa kisasa na utangamano na mifumo mingine ya kijeshi.
1790307959227.jpg
 
Jeshi la Anga la Misri limepokea helikopta zake tano za kwanza aina ya Boeing CH-47F Chinook, ikiwa ni sehemu ya oda ya helikopta 12 zenye thamani ya takribani dola milioni 426 za Marekani.

Helikopta hizo zilikabidhiwa rasmi wakati wa El Alamein International Airshow uliofanyika nchini Misri mwezi huu. Helikopta saba zilizobaki zinatarajiwa kukabidhiwa kulingana na ratiba ya mkataba inayotarajiwa kukamilika mwaka huu 2026.

CH-47F mpya zitatumika kuchukua nafasi ya kundi la zamani la CH-47D Chinook linalotumiwa na Jeshi la Anga la Misri.
1790322700347.jpg
 
Back
Top Bottom