Watu watatu wamefariki nchini Ujerumani kufuatia mlipuko wa malaria uliobainika katika eneo la Uwanja wa Ndege wa Frankfurt, huku idadi ya visa vilivyothibitishwa ikifikia vinane.
Awali, mamlaka za afya zilikuwa zimeripoti vifo vya watu wawili, kabla ya kifo cha tatu kuthibitishwa katika taarifa ya hivi karibuni. Wagonjwa wengine watano waliogundulika kuwa na malaria wanaendelea kupata matibabu.
Wakati huo huo, visa viwili vipya vimebainika nje ya uwanja huo wa ndege, kwa wagonjwa wanaoishi eneo la Schwanheim, karibu na uwanja huo. Mamlaka zimesema wagonjwa hao si wafanyakazi wa uwanja wa ndege na hawana historia ya kusafiri katika maeneo yanayojulikana kuwa na malaria.
Mamlaka za afya kwa kushirikiana na Taasisi ya Robert Koch zinaendelea na uchunguzi wa kubaini chanzo cha mlipuko huo. Moja ya nadharia zinazochunguzwa ni uwezekano wa mbu aina ya Anopheles kuingia nchini Ujerumani kupitia ndege za kimataifa na kusababisha maambukizi katika eneo hilo.
Kwa upande wake, Fraport, kampuni inayosimamia Uwanja wa Ndege wa Frankfurt, imeweka mitego maalum ya mbu katika maeneo mbalimbali ya uwanja huo. Mbu watakaonaswa watafanyiwa uchunguzi wa vinasaba ili kubaini iwapo wana vimelea vya malaria na kufuatilia chanzo chao.
Hata hivyo, wataalamu wa afya wamesema hatari ya malaria kuenea kwa kiwango kikubwa miongoni mwa umma bado ni ndogo. Malaria haiambukizwi moja kwa moja kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine, bali huenea pale mtu anapong'atwa na mbu aliyeambukizwa vimelea vya ugonjwa huo.