DAR ES SALAAM - Mwanamuziki nyota wa Bongo Flava, Diamond Platnumz, amesema alidhurumiwa kiasi cha Shilingi Bilioni 4 alicholipia kwa ajili ya kununua ndege yake binafsi aina ya Bombardier Challenger 603.
Akizungumza katika mahojiano na Wasafi Media yaliyorushwa kupitia YouTube na majukwaa mengine ya Wasafi, Diamond alieleza kuwa ndoto yake ya kumiliki ndege binafsi pamoja na helikopta ilipata pigo baada ya wakala aliyemtegemea kutoweka na fedha hizo.
Kulingana na Diamond, ndege hiyo binafsi "Private Jet" na Helikopta hiyo hazikuwa za matumizi yake binafsi tu, bali zlikuwa ni sehemu ya uwekezaji ambao ungetumika kukodiwa na kumwingizia mapato.
Hata hivyo, baada ya kukamilisha malipo ya awali, aligundua kuwa wakala husika hakuwa mwaminifu. Alitoweka na fedha bila kuwasilisha chombo hicho cha usafiri kama walivyokubaliana.
Kutokana na changamoto hiyo, msanii huyo amesema bado anategemea kukodi ndege kutoka Kenya kila anapofanya ziara kubwa za kimataifa barani Afrika. Hii inagharimu mamilioni ya fedha kwa kila safari.
Alitoa mfano kuwa safari moja ya kukodi Private Jet kutoka Tanzania kwenda Nigeria inagharimu takriban dola laki 150, ambayo ni karibu na shilingi milioni 400.
Diamond alisema kama angekuwa na ndege yake binafsi, basi hata waandaaji wa matamasha wangelazimika kuikodi kutoka kwake. Pia alisisitiza kuwa hawezi kwenda kufanya show yoyote barani Afrika bila kutumia private jet.
Akifafanua kuhusu ukimya wake tangu tukio litokee, Diamond alisema alifuata ushauri wa kisheria. Alibainisha kuwa mamlaka husika zinaendelea na uchunguzi wa kina ili kuona uwezekano wa kurejesha fedha zake na kupata haki yake, badala ya kujadili suala hilo hadharani.