Ushirikiano wa kihistoria kati ya Urusi na China katika kuunda ndege kubwa ya abiria ya CR929 ulisambaratika rasmi kutokana na mgongano mkubwa wa kimkakati, vikwazo vya kimataifa, na kutosimama upande mmoja kimaslahi.
Mradi huo uliolenga kutoa ushindani dhidi ya kampuni kubwa za Boeing na Airbus ulianza kuingia doa kufuatia vita vya Ukraine mwaka 2022, vilivyosababisha Urusi kuwekewa vikwazo vikali vya kiuchumi.
China, kupitia kampuni yake ya COMAC, ilihofia kuwa kuendelea kushirikiana karibu na Urusi kungeweka rehani uwezekano wa ndege hiyo kukubalika kimataifa na kupata vipuri muhimu kutoka nchi za Magharibi.
Tofauti kubwa ya kifikra ilijitokeza kwenye uteuzi wa teknolojia, ambapo China ilitaka kutumia injini na mifumo ya kisasa kutoka kampuni za Kimagharibi kama General Electric ili kurahisisha mauzo ya nje, wakati Urusi ilishikilia msimamo wa kutumia teknolojia zao za ndani ili kujikinga na shinikizo za kisiasa.
Mbali na hayo, nchi hizi mbili zilishindwa kukubaliana kiwango cha ugawaji wa faida na masoko, huku kukiwa na mzozo wa chini kwa chini wa kutoaminiana kiufundi ambapo Urusi ilisita kukabidhi siri zake kuu za kihandisi na muundo wa ndege kwa China.
Hatimaye, ushirikiano huo ulivunjika na kuifanya China kuondoa herufi "R" iliyowakilisha Urusi na kuupa mradi huo jina jipya la C929 (Awali C-929) ikiendelea nayo peke yake, huku Urusi ikijitenga na kuelekeza nguvu zake zote katika kufanya marekebisho ya ndani kwenye mradi wake wa ndege ya MC-21 kwa kutumia injini na vifaa vya asilimia mia moja vya nyumbani.