Kwa abiria wengi, ndege kutua taratibu au kutua laini (Soft landing) au mara nyingine ile hali ya “kutua laini kama siagi” (butter landing) inatoa hisia ya utulivu na ujuzi wa juu na ndiyo maana wengi hupenda.
Lakini ndani ya ulimwengu wa uendeshaji wa ndege, kutua laini sio kila wakati humaanisha ndio bora zaidi.
Kuna wakati rubani anapanga makusudi kutua kwa nguvu kidogo. Sababu yake ni usalama, na si uzuri.
Lengo kuu sio kufurahisha abiria bali ni kuhakikisha ndege inafika mwanzo wa njia ya kutua kwa kasi sahihi, inagusa eneo lililokusudiwa, inabaki kwenye mstari wa kati na inaanza kupunguza mwendo mara moja.
Kwenye njia fupi za kutua, njia zilizolowa na siku zenye upepo mkali, kujaribu sana kutua kwa laini kunaweza kuwa hatari.
Kutua kwa nguvu zaidi kunasaidia magurudumu kugusa haraka, vifaa vya kupunguza mwendo kama 'spoilers' kufunguka kwa wakati na breki kuanza kufanya kazi vizuri. Hapo ndipo udhibiti wa ndege unakuwa bora zaidi.
Watu wengi hudhani kutua laini ndio ishara ya ubora. Lakini mara nyingine marubani huangalia usahihi.
Ni muhimu ndege iguse sehemu sahihi ya njia ya kutua.
Ndege kuelea wakati wa kutua (landing flare) mbali zaidi ya eneo lililotakiwa ni hatari zaidi kuliko kutua kwa nguvu kidogo lakini katika sehemu sahihi.
Kuna sababu kuu tatu zinazofanya marubani kutua kwa nguvu kwa kukusudia.
Kwanza ni urefu wa njia ya kutua.
Njia fupi haiachi nafasi ya kuelea (landing flare).
Pili ni hali ya njia yenyewe
Mvua, theluji au barafu vinahitaji magurudumu kugusa chini haraka ili breki zifanye kazi mapema.
Tatu ni upepo, hasa upepo wa pembeni maarufu kama "Crosswind" wenye nguvu, ambapo udhibiti unakuwa muhimu zaidi kuliko uzuri wa kutua.
Kwa hiyo hisia ya kutua kwa nguvu si ishara ya kosa.
Mara nyingi ni ishara ya urubani wa nidhamu ya usalama wa abiria na chombo.
Ndege ikigusa chini sehemu sahihi (touch down zone) hupata muda wa kutosha wa kusimama kwa usalama.