Usiku wa Julai 1, 2002, mfululizo wa makosa madogo ambayo yalionekana hayana maana yalisababisha moja ya ajali mbaya zaidi katika historia ya usafiri wa anga
Juu ya mji mdogo wa Überlingen nchini Ujerumani, ndege mbili zilikutana kwenye njia moja angani kwa urefu wa karibu futi 35,000.
Ndege ya Bashkirian Airlines Flight 2937, Tupolev Tu-154M iliyokuwa na watu 69, na ndege ya mizigo ya DHL Flight 611, Boeing 757-200F iliyokuwa na marubani wawili.
Kwa sekunde chache, watu wote 71 waliopanda ndege hizo waliaga dunia, wakiwemo watoto 52 waliokuwa wakisafiri kutoka Urusi kwenda Hispania kwa likizo ya kiangazi.
Tupolev ilikuwa ikitoka Moscow kuelekea Barcelona, wakati ndege ya DHL ilikuwa ikiruka kutoka Bahrain kuelekea Brussels ikiwa na kituo Bergamo, Italia.
Wakati huo zoezi la uongozaji ndege eneo hilo ulikuwa chini ya mnara wa uongozaji ndege wa Zurich, ambapo wafanyakazi walikuwa wamepunguzwa usiku.
Mifumo muhimu ya onyo la rada na mawasiliano ilikuwa imezimwa kwa ajili ya matengenezo, hivyo muongozaji mmoja wa ndege alibaki kusimamia ndege nyingi kwa wakati mmoja.
Wakati ndege hizo zilipokaribiana, muongozaji alitambua hatari na kumwagiza rubani wa Tupolev kushuka mara moja.
Lakini wakati ule ule, ndege zote mbili zilitoa amri tofauti na muongozaji ndege kutoka kwenye mifumo ya ndani ya kuzuia ndege kugongano (TCAS).
TCAS iliamuru Tupolev ipande juu, huku Boeing 757 ikiamriwa ishuke chini.
Marubani wa DHL walifuata amri ya TCAS mara moja kama ilivyoundwa kufanya.
Lakini ndani ya chumba cha marubani wa Tupolev, walichagua kufuata amri ya muongozaji ndege ya kushuka badala ya amri ya TCAS.
Wakati huo sheria za anga hazikuwa wazi ni amri ipi inapaswa kutangulizwa, jambo lililoleta mkanganyiko mbaya.
Saa 5:35 usiku kwa saa za eneo hilo, ndege ziligongana kwa pembe karibu ya nyuzi 90 ambapo mkia wa wima wa Boeing 757 ulikata sehemu ya mbele ya mbawa za Tupolev, kuivunja ndege hiyo na kuifanya kuanguka kuelekea chini hapo hapo.
Boeing yenyewe iliyoumia vibaya na kukosa sehemu kubwa ya mkia wake ilibaki hewani kwa dakika mbili zaidi kabla ya kuanguka msituni kilomita chache kutoka hapo. Hakukuwa mtu aliyenusurika.
Uchunguzi rasmi ulihitimisha kuwa ajali hiyo haikusababishwa na kosa moja, bali na mlolongo wa udhaifu wa kimfumo, upungufu wa wafanyakazi, kuzimwa kwa mifumo ya usalama, mapungufu ya mawasiliano, na utata wa taratibu kuhusu ni amri ipi ifuatwe kati ya TCAS na muongozaji wa ndege.
Ajali hiyo ilibadilisha kabisa usalama wa anga duniani.
Mashirika ya kimataifa kama ICAO yalibainisha wazi kuwa marubani lazima wafuatie amri za TCAS hata kama zinapingana na maagizo ya muongoza ndege.
Mabadiliko hayo bado ni miongoni mwa hatua muhimu zaidi zilizoboresha usalama wa anga ya kibiashara na zimezuia majanga kama hayo kutokea tena.