Saa 3 asubuhi ya tarehe 14 Agosti 2005, Boeing 737 ya Helios Airways iliondoka Larnaca ikiwa na lengo la kuwasili Prague. Hakuna aliyejua ndani ya dakika chache baadae, ndege ingebadilika kuwa chumba cha ukimya (ghost room).
Kabla ya kupaa, mhandisi mmoja aliwasha mfumo wa shinikizo la kipupwe ndani (Cabin pressurization) kwenye “manual” kwa majaribio lakini alisahau kurudisha kitufe hicho kwenye “auto”.
Rubani na msaidizi wake walipitwa na kosa hilo. Ndege ilipopanda, mgumo wa hewa ulianza kutoka polepole sababu uliachwa kwenye 'manual' upungufu wa Oksijeni ukatokea kwenye ubongo wa abiria, macho yakaanza kuzimika abiria mmoja baada ya mwingine.
Ingawa Kengele ya onyo ililia, lakini walidhani ni onyo la kawaida.
Ndani ya dakika chache, watu 121 walikuwa wamelala usingizi wa milele.
Ndege ikabaki peke yake. Ilipaa kwa mduara kuzunguka anga ya Athens karibu mara sita kama ndege iliyopotea.
Jeshi la Ugiriki lilituma ndege mbili za F-16. Marubani wa kijeshi walipofika karibu, waliona msaidizi wa rubani amelala juu ya usukani kiti cha nahodha kikiwa tupu, na vinyago vya oksijeni vinining’inia bila mtu.
Ndege nzima ilikuwa na mzimu, hakuna aliyekuwa macho, mhudumu mmoja wa kiume alichelewa kusinzia sababu alivaa kinyago cha hewa ya dharura (Portable Oxygen mask) na kujaribu kutambaa kwenda chumba cha marubani, lakini pia nae hakuweza kuokoa jahazi.
Saa tatu baadaye angani mafuta yalikata kwenye ndege hiyo ya Helios 522 na kwenda kuanguka Grammatiko.
Ilikuwa ni ajali mbaya zaidi katika historia ya Ugiriki.
Ajali hii ilifundisha dunia kuwa kosa dogo la binadamu, kama kusahau kubadilisha kitufe kimoja, linaweza kusababisha janga lisilofikirika mfano wa hii ndege ya Helios 522 iliyopata umaarufu kama ndege ya mizimu (Ghost Plane)
Tangu mwaka huo wa 2005, sekta ya anga imeimarisha mapitio ya uendeshaji zaidi (“checklist discipline”).
Sasa mifumo ya shinikizo la kipupwe lazima ithibitishwe mara mbili kabla ya kupaa, na sauti au kengele za onyo zimebuniwa zitofautiane wazi ili rubani asichanganyikiwe.
Kwa sababu kila kengele ina maana yake, na kutoisikiliza kunaweza kuwa gharama ya maisha.