Kampuni ya Airbus Helicopters ilipiga hatua zaidi kwa kufanya mradi wa kubadilisha kabisa taswira ya usafiri wa anga kwa kuunda Helikopta aina ya Airbus RACER.
Huu ni mradi wa kimapinduzi wa Helikopta chotara unaochanganya uwezo wa Helikopta wa kupaa ma kutua wima (rotary wing) na kasi kubwa kama ya ndege za kawaida (Fixed wing)
Mradi huu unafadhiliwa chini ya mpango wa Ulaya wa Clean Sky 2, ukiwa na lengo la kutoa usafiri wa haraka, wenye gharama nafuu na unaolinda mazingira.
Helikopta hii inatofautiana kabisa na helikopta zilizozoeleka kutokana na muundo wake wa kipekee.
Helikopta hiyo inatumia panga ya juu (Rotor) kwa ajili ya kupaa na kutua, lakini ina mabawa maalumu ya pembeni yenye pangaboi zinazofanya kazi ya kama ndege ya kawaida ikiwa angani.
Kasi yake kubwa inatokana na pangaboi mbili zilizowekwa kwenye ncha za mabawa zinazoisukuma helikopta mbele.
Muundo huu unaondoa hitaji la panga la kawaida la mkiani na kuifanya helikopta kuwa na uthabiti mkubwa sana wakati wa kukata kona kali bila kuinama mbele.
Katika majaribio ya hivi karibuni yaliyovutia wengi kwenye maonyesho ya anga ya ILA Berlin Air Show, RACER imethibitisha kuwa chombo cha kipekee kwani ilifikia kasi ya rekodi ya kilomita 444 kwa saa na kuonyesha uwezo mkubwa wa kupaa kwenda juu kwa futi 10,000 ndani ya dakika mbili na sekunde 44 tu.
Zaidi ya hayo, helikopta hii inatumia mfumo wa kisasa wa Eco-Mode unaomruhusu rubani kuzima injini moja ikiwa angani ili kupunguza matumizi ya mafuta na uzalishaji wa kaboni kwa asilimia 20 hadi 25, huku injini hiyo ikiwa na uwezo wa kuwaka tena kwa sekunde chache ikihitajika.
Teknolojia hii ya hali ya juu inatarajiwa kuleta mapinduzi makubwa katika nyanja za usafiri wa dharura.
Kasi na uwezo wake wa kipekee unafanya RACER kuwa chombo bora kwa ajili ya operesheni za uokoaji, huduma za matibabu ya dharura, usimamizi wa majanga, na usafirishaji wa kijeshi ambapo kuwahi mapema ndio nguzo kuu ya kuokoa maisha ya watu.