Macho ya Bundi-18-
Wewe unaingilia yanakuhusu?... Yanakuhusu? Badala ya kurudi nyumbani kwako, unangangania katika nyumba za watu na kuziharibu. Umechangia sana kutugombanisha wewe, nilimjibu.
Mume wangu alikuwa amesimama katikati ya sebule huku akitokwa na jasho jingi usoni kana kwamba alikuwa anafanya mazoezi ya judo. SONGA NAYO...
BADALA ya kusikiliza upuuzi aliokuwa akiusema Pili na mama yake, nilikwenda chumbani kwangu na kumuacha mume wangu akiwa amesimama akiwaangalia.
Lakini mara tu baada ya mimi kufika chumbani nilimuona mume wangu akinifuata na kuja kuingia chumbani nilipokuwa mimi.
Mume wangu, hawa watu wahamishe. Niliwakaribisha kwa kuamini kuwa tutaishi kama ndugu lakini kwa kuwa wananiona mimi sizai wananinyanyasa na kujifanya wao ndiyo wenye nyumba hii, nilinyamaza kidogo kupisha neno litoke kwa mume wangu.
Sikiliza Salome. Kuwahamisha siwahamishi isipokuwa cha kufanya ni kumtimua Mei kwani ndiye anayemharibu Pili.
Tulijadiliana mambo mengi sana kuhusu Pili na mama yake Mei na kuafikiana kwamba mama wa Pili ahame kwa kuwa yeye ndiye chanzo cha ugomvi unaoibuka mara kwa mara katika nyumba yetu.
Mume wangu aliamua kutoka chumbani na kumuita Pili sebuleni kwani sisi tulipoingia chumbani yeye na mama yake wakaingia kwenye chumba wanacholala.
Pili sikiliza. Wewe ndiye mke wangu na ndiye unastahili kukaa hapa kwangu. Mama yako alikuja kwa ajili ya kukusaidia wakati una ujauzito. Sasa umejifungua tena salama nitaomba umuambie mama yako kuwa arudi kwake.Sawa?
Pili badala ya kujibu swali hilo alinyanyuka na kwenda chumbani kwa mama yake. Alikaa huko ndani kwa dakika kumi na tano au ishirini hivi kisha.
Huyo atakuwa anamuambia mama yake haya maagizo niliyompa. Hafai yule mama kukaa hapa, kwanza mshirikina, alisema mume wangu.
Umeonaee. Nafurahi umeliona hilo wewe mwenyewe.
Wakati tunaendelea kuzungumza na mume wangu tulishitukia Pili na mama yake pamoja na mtoto mchanga wakitoka chumbani kwao huku wakiwa na mabegi ya nguo.
Moyoni nilidhani ni nguo za mama yake Pili, yaani rafiki yangu Mei kwamba sasa anakwenda kwake.
Wewe umesemaje? lilikuwa swali la Mei akilielekeza kwa mume wangu.
Lazima uwe na adabu, huwezi kuniuliza hivyo. Mimi mkweo lakini pia nimekuzidi umri, alifoka mume wangu.
Nakuambia nikiondoka hapa naondoka na mwanangu Pili na mjukuu wangu, siwezi kuwaacha hapa.
Huwezi kuondoka na mke wangu pamoja na mwanangu. Nimemuambia Pili uondoke wewe haraka sana. Huwezi kunivunjia heshima mimi na mke wangu.
Nitafutie gari niondoke. Usinitishe mimi mtoto wa mjini babu wee!
Nikutafutie gari? Ingiza mizigo yako kwenye gari langu, nitakupeleka mimi huko kwako.
Unipeleke wewe wakati umenifukuza kwako? Sikubali. Niletee gari hapa niondoke.
Mume wangu alimuagiza mlinzi akatafute taksi na punde si punde ikawa imefika.
Dereva kutoka hapa mpaka Mkuti bei gani? Nataka umpeleke huyu mama.
Shilingi elfu tano na mia tano.
Nakuambia simuachi mwanangu ngo, mwanamke wako asiyezaa asije kumuua mjukuu wangu.
Unasemaje? nilisema nikamvamia na kumkaba koo akawa anahema kwa shida. Mume wangu alijitahidi kutuachanisha lakini mikono yangu ilikuwa kama ina sumaku.
Je nini kiliendelea? Fuatilia baadae..................