Macho ya Bundi-7
BASI tumpe nafasi Salome mwenye mume, unasemaje shemeji? aliuliza Kalikalanje.
Unaniuliza miye kwani mimba nimetia mimi? Nilimjibu huku nikimtupia jicho baya Pili nikiwa na hasira huku nikitamani kumrukia kwa kula vyangu.
SONGA NAYO...
Shemeji yangu Kalikalanje alimuuliza mzee Chinchi kama anahusika na ujauzito wa binti huyo, mtoto wa rafiki wa mkewe.
Sina haja ya kukataa, ujauzito huu ni wangu, alisema huku akifikicha macho kwa kitambaa.
Nini? Niliuliza.
Shemeji Salome acha hasira.
Unataka niache hasira nishangilie siyo.
Siyo hivyo shemeji.
Sasa nakusihi Mei. Kwa kuwa jambo hili ni la ghafla na bwana Chinchi hajapinga, amekubali kuwa anahusika na mzigo huu, nendeni nyumbani na sisi tubaki tukijadili, tuone nini cha kufanya.
Tuondoke mjadili, mtajadili na nani kama siyo sisi? Mimi ndiye mzazi wa huyu binti ambaye kwanza amemkatisha masomo yake, pili anaweza kuwa ni mbakaji kwa sababu binti yangu ana miaka kumi na sita tu, nadhani mnajua sheria za siku hizi, alisema Mei huku akiniangalia.
Hakika dakika kadhaa tulikuwa tumeshakuwa maadui kati yangu na rafiki yangu Mei. Nilishangaa kabisa kuona amebadilika kana kwamba tulikuwa hatujuani.
Sawa, wewe ni mzazi wa Pili binti anayetajwa hapa kuwa amepewa mimba na mume wa rafiki yako Salome. Nakuomba chonde, nenda nyumbani nijadili na hawa wenyeji wako.
Nakushangaa. Kwa nini sisi tusishirikishwe huo mjadala? aliuliza Mei.
Utashirikishwa baada ya kujadiliana hawa wahusika wawili si unajua kuwa hawa ni wana ndoa?
Unaona begi lile pale. Mimi Pili aliponiambia kuwa ana mimba ya bwana Chinchi nilikasirika sana na nikaamua akusanye nguo zake tuje huku kwake tena nilimpa taarifa hizi jana.
Baada ya Mei kusema hivyo nikakumbuka kuwa kumbe ndiyo maana jana Chinchi aliporudi kutoka huko alikokuwa amekwenda alishindwa kula chakula na kusingizia alikuwa anaumwa.
Nakumbuka nilimgusa shavu lake na kuona likiwa baridi kuonyesha kuwa hakuwa na homa yoyote. Shaka ilinijaa.
Sasa Mei, wewe unasemaje? Maana nimekuomba sana muende kwenu kisha kesho nitakuita tujadili haya mwenzangu unaonekana hauko tayari, hutaki kabisa.
Kweli sitaki mzungumze peke yenu, mimi na mwanangu ni lazima tuwepo.
Lakini mimi nimekuambia kuwa tuwaache wana ndoa hawa wajadiliane kuhusu hili kwa sababu siyo kitu kidogo hiki, shemeji yangu Kalikalanje alizidi kumuomba.
Najua sana kwamba hiki siyo kitu kidogo lakini napenda kukuhakikishia kwamba sisi pia tumeona kuwa hili ni jambo zito ndiyo maana tukaja hapa, tena na nguo zetu.
Ni sawa, lakini kwa nini unaupuuza ushauri wangu? Tuambie tutazungumzaje bila wana ndoa kukaa na kukubaliana?
Mhusika amekubali kuwa mimba hii ni yake, wajadili nini tena?
Sawa amekubali kuwa hii mimba ni yake, je ungekuwa wewe ni Salome, usingependa kuafikiana na mumeo na kuona nini cha kufanya?
Maswali yako ni mengi sana na unanihoji kana kwamba mimi ndiye mkosaji. Mimi sijakosea kumzaa mtoto wa kike. Alikuwa na tabia njema sana najua mia kwa mia kuwa mwenye makosa ni huyu bwana.
Kwa nini unasema hivyo?
Nasema hivyo kwa sababu nina uhakika kuwa alitumia uwezo wake wa kifedha kumshawishi mwanangu kufanyanaye mapenzi.
Mei alitulia kidogo akameza mate kisha akaendelea.
Ushahidi wote mimi ninao na kuna hata baadhi ya akina mama majirani wa huyu mzee walikuja nyumbani kwangu juzi kuniambia, wakati najiandaa nimuulize binti akanifahamisha kuwa yeye ni mjamzito.
Itaendelea leo jioni..............