Katika mwaka mmoja uliopita tangu Donald Trump kurejea Ikulu ya White House, sera ya Marekani kwa Afrika imeanza kubadilika kimya kimya. Barua ya ndani ya mkuu wa Idara inayoshughulikia mambo ya Afrika katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Marekani Nick Checker, iliyovuja hivi karibuni, ilifichua wazi mwelekeo huu mpya: misaada haionekani tena kama jukumu la kimaadili, bali kama chombo cha kusukuma mbele maslahi ya kimkakati ya Marekani. Kwenye barua hiyo, Bw. Cheker alisema, “Si aibu kuwasisitizia watu wa Afrika mchango wa misaada ya Marekani, na cha muhimu ni kutumia ipasavyo misaada hiyo ili kuhudumia maslahi ya kisiasa ya Marekani. ”
Takwimu za Umoja wa Mataifa zinaonyesha kuwa mwaka 2025 mchango wa Marekani katika misaada ya kibinadamu duniani umepungua kwa zaidi ya asilimia 75. Wakati huo huo, mfumo wa misaada ya nje wa Marekani umefanyiwa marekebisho makubwa: shirika la USAID limefungwa, na miradi mingi kwenye sekta za afya, chakula na maendeleo katika nchi za Afrika imesitishwa au kufutwa, jambo lililosababisha athari kubwa kwa jamii zilizo tayari kuwa dhaifu barani humo.
Mabadiliko muhimu zaidi si kupungua kwa fedha, bali ni kufafanuliwa upya kwa madhumuni ya misaada. Chini ya mfumo mpya, miradi ya afya, hali ya hewa na maendeleo inalazimika kutumikia malengo ya kimkakati ya Marekani, na kuunganishwa na masuala kama madini muhimu na misimamo ya kidiplomasia. Misaada imegeuka kuwa chombo cha mazungumzo, si tena suluhisho la matatizo ya kijamii.
Mwelekeo huu unaendana na Mkakati mpya wa Usalama wa Taifa wa Marekani, ambapo Afrika inatajwa kwa kifupi tu, hasa kwa umuhimu wake katika upatikanaji wa madini, ushindani dhidi ya China, na udhibiti wa hatari za usalama. Maendeleo ya Afrika hayachukuliwi kama lengo la muda mrefu, bali kama sehemu ya ushindani wa nchi kubwa.
Kwa nchi za Afrika, hili si tatizo la mradi mmoja bali changamoto ya kimuundo. Ndiyo maana umuhimu wa muungano wa kikanda, kama Umoja wa Afrika na Eneo la Biashara Huria la Afrika, unaongezeka. Kwa pamoja, Afrika inaweza kuongeza nguvu ya majadiliano na kupunguza utegemezi kwa nje. Wakati huo huo, ushirikiano na nchi za Dunia ya Kusini, ikiwemo China, unaendelea kutoa njia mbadala inayozingatia maendeleo ya muda mrefu, bila masharti ya kisiasa, na kutoa nafasi zaidi ya kimkakati kwa Afrika katika mazingira ya kimataifa yenye utata.