Mabadiliko makubwa ya uongozi yaja
na mwandishi wetu
Mabadiliko makubwa ya kiuongozi yanatarajiwa ndani ya Serikali mara baada ya uchaguzi wa Chama cha Mapinduzi kukamilika ngazi ya taifa katika uchaguzi unaotarajiwa kufanyika mwanzoni mwa Novemba hii.
Vyanzo vyetu ndani ya serikali na ndani ya chama chenyewe, zinaonyesha kwamba Mwenyekiti wa CCM ambaye pia ni Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania anatarajia kufanya mabadiliko makubwa kwenye safu za uongozi akianzia kwenye sekretarieti ya chama na kuishia serikalini.
Habari kutoka kwa watu walio karibu na uongozi, zinaonyesha kwamba hadi sasa, Rais Kikwete hajaridhishwa na hali halisi ya kiuongozi.
Kuna pengo kubwa kati ya mawazo na matarajio ya mwenyekiti na hali halisi ya kiuongozi ilivyo. Kwa hiyo kuna uwezekano wa mabadiliko tangu kwenye sekretarieti ambayo ndiyo humuwezesha mwenyekiti kufanya kazi zake kwa ufanisi na kisha mabadiliko hayo kusambaa hadi serikalini,chanzo chetu cha habari kilieleza.
Kwa upande wa serikali hasa katika Baraza la Mawaziri, habari hizo zinaeleza kuwa baada ya mambo mengi kutokea na baada ya kujipa muda wa miaka miwili ya kuwapima watendaji wake, Rais Kikwete anatarajiwa kufanya mabadiliko makubwa siyo katika sura tu bali na mwelekeo halisi wa serikali yake.
Kumekuwapo malalamiko ya hapa na pale kuhusu utendaji wa baadhi ya mawaziri, wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya. Hata hivyo, Rais Kikwete amekuwa mkimya kuhusu malalamiko hayo.
Chanzo chetu cha habari kimeliambia Rai kwamba Rais alisubiri kujiimarisha kwenye chama ndipo aweze kuwa na timu ambayo itafanya kazi kwa mujibu wa matarajio yake.
Kwa upande wa chama, kwa sasa mazungumzo yanayotawala kwenye chama hicho ni uteuzi wa Makamu Mwenyekiti; nafasi ambayo kwa sasa inashikiriwa na John Samwel Malecela. Kiongozi huyo hajasema kama angependelea kuendelea na nafasi hiyo au la. Kwa mujibu wa utaratibu wa CCM, baada ya kukamilisha safu za wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, Mwenyekiti hutangaza jina la mtu ambaye angependelea awe makamu wake.
Desturi hizo za uchaguzi zinaonyesha kwamba haijawahi kutokea wajumbe wakalikataa jina la mtu aliyependekezwa na mwenyekiti kuwa makamu wake.
CCM ina makamu wawili. Mwingine ni lazima atoke upande wa Zanzibar ambaye kwa sasa ni Amani Abeid Karume.
Wachunguzi wa mambo ya kisiasa, wanaeleza kwamba kuna uwezekano mkubwa Rais Kikwete akafanya kama alivyofanya mwenzake wa China Hu Jintao ambaye baada ya kuchoshwa na tuhuma za rushwa, aliamua kufanya mabadiliko makubwa ambayo yamesababisha kuondolewa madarakani kwa Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama cha Kikomunisti cha nchi hiyo, Chen Liangyu ambaye anatuhumiwa kwa ubadhilifu katika mpango wa pensheni.
Wachambuzi wa mambo wanasema Kikwete anaweza kabisa kuchukua mfano wa kiongozi wa China ambaye baada ya kuchoshwa na rushwa ndani ya chama, ameamua kufanya kile kilichowashinda waliomtangulia. Katika uchaguzi wa ngazi za wilaya na mikoa, Kikwete aliagiza vyombo vya usalama vya dola kuingia katika kumbi za mikutano za CCM na kuwashughulikia watoa na wapokea rushwa.
Hata hivyo, hatua hiyo ilisababisha malalamiko makubwa kutoka kwa baadhi ya wahafidhina ndani ya chama hicho jambo lililomfanya Kikwete kuitisha mkutano wa dharura wa Kamati Kuu na kusisitiza nia yake ya kupambana na ufisadi kuanzia kwenye chama.
Kikwete aliwahi kukaririwa akisema kuwa huwezi kuwa na chama kinachokumbatia rushwa, ukapambana na rushwa ndani ya serikali. Ni kutokana na mkakati huo wa Kikwete, uchaguzi wa CCM ya mikoa umetoa sura mpya za uongozi.
Pamoja na matarajio ya mabadiliko hasa ndani ya chama, baadhi ya wanachama wa CCM waliozungumza na Rai lakini kwa masharti ya kutotajwa majina, wameeleza kwamba wangehitaji mabadiliko siyo ya sura bali ya kiitikadi.
Mmoja wa waasisi wa chama hicho, Peter Kisumo, alisema matarajio yake kuona siyo mabadiliko ya sura bali mabadiliko katika itikadi. Ni lazima chama kijifikishe mahali ambapo kitakuwa na sauti ya kuzungumza na watu wakakisikiliza, alisema mzee Kisumo. Uchaguzi wa wajumbe 85 wa kukamilisha nafasi za Halmashauri Kuu ya CCM ndiyo utatoa mwanga na mwelekeo wa nani atakuwa nani katika chama hicho.
Kwa sasa kinyanganyiro kinachotupiwa macho mawili ni cha wajumbe 20 kupitia kundi la Bara.
Kundi hilo lenye jumla ya wagombea 59 lina majina mazito katika chama hicho na serikalini na mchuano wao unatarajiwa kuwa mkali.
Kundi hilo lina majina kama vile Waziri Mkuu mstaafu, Fredrick Sumaye, Waziri Mkuu wa sasa, Edward Lowassa, Naibu Katibu Mkuu, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, Katibu Mkuu wa sasa, Yusuph Makamba, Naibu Katibu Mkuu, Jaka Mwambi, Balozi wa Tanzania nchini Afrika Kusini, Emmanuel Mwambulukutu pamoja na orodha ndefu ya mawaziri, naibu mawaziri pamoja na wabunge mashuhuri. Wagombea wanaopitia kundi hilo ni pamoja na Tarimba Abbas, Filbert Bayi, Shy-Rose Bhanji, Enock Chambiri, John Chiligati, Siwajibu Clavery, Dk. David Mathayo, Said Masoud Fundikira, Christopher Ghachuma, Arbogast Godogodo, David Holela, Jared Kadunga, Charles Kagonji, Dk. Deodorus Kamala, Constantine Kanyasu, Prof. Juma Kapuya na Alhaji Said Kilahama.
Wengine katika kundi hilo ni pamoja na Haidah Kilua, Abdulrahman Kinana, Lukas Kisasa, John Komba, Edward Lowassa, William Lukuvi, Pascal Mabiti, Dk. Milton Makongoro Mahanga, Amos Makala, Yusuf Makamba, Novatus Makunga, na Mohamed Yakub Mamoon.
Katika kundi hilo pia wamo Wilson Masilingi, Bernard Membe, Maurus Mhimbira, Mohamed Mkumbwa, Dk. James Msekela, Dk. Ibarhim Msengi, Jackson Msome, Prof. Idrisa Mtulia, Prof David Mwakyusa, Captain Jaka Mwambi, Emmanuel Mwambulukutu, Aggrey Mwanri, Abeid Mwinyimusa, na Job Ndugai.
Wengine ni William Ngereja, Kingunge Ngombale-Mwiru, Brigedia Jenerali Hassan Ngwilizi, Dk. Baanda Salim, Salim Khamis Salim, Abdul Adam Sapi, Isidore Shirima, George Simbachamwene, Amos Siyantemi, Fredrick Sumaye, Dk. Hashim Twaakyondo, Frank Uhaula, Prof. Samwel Wangwe, Stephen Wasira, na Nicholaus Mateso Zacharia.
Source: RAI