John John Mnyika ama "JJ" kama wengi wanavyopenda kumwita, alizaliwa Dar es salaam Agosti 21 mwaka 1980 akiwa ni mtoto wa tatu katika familia ya Bwana John Dalali na Bi Lucia Mduma. Alipata malezi bora chini ya familia hii ya kikatoliki yaliyomjenga kiakili na kimsimamo huku mama yake akiwa ni chachu ya yeye kujiamini, kujitahidi, kuwa na moyo wa upendo kwa kila mtu na kuheshimu watu wenye mitazamo na imani mbalimbali.
Alianza safari yake ya kielimu katika shule ya msingi ya Chang'ombe mazoezi na kumalizia katika shule ya msingi Mbuyuni katika jiji la Dar es salaam. Alishika nafasi ya kwanza katika mtihani wa kuhitimu elimu ya msingi na kuchaguliwa kujiunga na shule ya vijana wenye vipaji maalum ya Ilboru iliyoko mkoani Arusha. Hata hivyo wito wa kuwa padre ulimsukuma kijiunga seminari ya Maua iliyoko Moshi mkoani Kilimanjaro.
Akiwa seminari alijifunza kuishi maisha ya kujinyima, uadilifu na unyenyekevu kama alivyokuwa mtakatifu Fransisko wa Asizi na watawa wakikapuchini kwa ujumla. Aidha maisha ya seminari yalijenga zaidi ari yake ya kufanya kazi kwa bidii hususani katika kilimo na shughuli mbalimbali za uzalishaji mali. Alihitimu kidato cha nne mwaka 1998 kupata daraja la kwanza nukta saba yaani "division one-points seven" huku akiwa na alama A katika masomo tisa.
Pengine kipindi kilicholeta mabadiliko ya kimtazamo na kujenga dira ya maisha yake ni kile alichokuwa akisubiri kujiunga kidato cha tano baada ya kuwa ameshahitimu kidato cha nne. Katika kipindi hiki aling'amua adha ya ukosefu wa ajira kwa vijana na fursa finyu kwa vijana katika kujikwamua kimaisha na hasa kutokuwepo mipango ya makusudi ya kuwaendeleza vijana nchini licha ya wingi wao, nguvu zao na vipaji vyao kuwa tunu kwa mustakabali wa taifa. Kwa hivyo alijiingiza kwenye harakati za kumkomboa kijana kupitia asasi ya National Youth Forum (NYF). Aliomba kwa mafanikio kujiunga na shule ya sekondari Tambaza ili kubaki Dar es salaam kuendeleza harakati alizokwisha zianza.
Akiwa Tambaza aliendelea na harakati za vijana kupitia NYF na akawa pia mwenyekiti wa mkoa wa chama cha wanafunzi wakatoliki "Tanzania Youth Catholics Students", TYCS ambapo alifanya mengi ya kukumbukwa ikiwa ni pamoja na kubuni kampeni ya matumaini katika TYCS na akajifunza kwa vitendo kuwa uongozi ni utumishi.
Ni katika kipindi hiki - mwaka 2000, ambapo yeye na vijana wenzake wengi wao wakiwa ni wanafunzi wa sekondari walipoanzisha Taasisi ya Dira ya Vijana Tanzania "Tanzania Youth Vision Association" almaarufu kama TYVA na yeye kuchaguliwa kuwa katibu mkuu wa kwanza wa Taasisi hii.
Baada ya kumaliza kidato cha sita mwaka 2001,alijiunga na chuo cha diplomasia cha jijini Dar es salaam katika kozi ya itifaki na mahusiano ya jamii. Baadaye aliajiriwa na Redio Tanzania Dar es salaam (RTD) katika kitengo cha PRT na kufanya kazi ya utangazaji kwa mwaka mmoja. Akiwa RTD bado aliendelea na harakati za vijana kupitia NYF mpaka taasisi hiyo ilipofutwa na serikali. Aliendelea pia na harakati za utetezi wa wanafunzi kupitia mtandao wa wanafunzi Tanzania 'TSNP'ambayo yeye ni mmoja wa waanzilishi wake.
Alijiunga na chuo kikuu cha Dar es salaam (UDSM) mwaka 2002 kusoma shahada ya kwanza ya utawala wa biashara (BBA) katika programu ya jioni. Sambamba na masomo ya jioni katika chuo kikuu cha Dar es salaam, ameendelea kuwa muajiriwa wa United Nations Association (UNA) kama mratibu msaidizi wa mradi wa ushiriki wa vijana unaotekelezwa na kitengo chake cha vijana (YUNA) katika wilaya kumi nchini Tanzania.
Pia pamoja na ajira na masomo, ameendelea kushika nafasi kadhaa za uongozi na kufanya shughuli mbalimbali. Mwaka 2003 alibuni na kuratibu programu ya maboresho na marekebisho ya TYVA ambayo yamesaidia asasi hiyo kupata uongozi thabiti, ofisi, miradi, mipango ya muda mrefu na uwezo wa kiundeshaji. Aliongoza kama mwenyekiti wa Taifa wa Taasisi hii mpaka alipoamua kujiuzulu mwezi januari 2005 ili kuweza kuingia kwenye siasa. Amejiunga na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na kuteuliwa kuwa mkurugenzi wa Taifa wa vijana wa chama hicho.
Pamoja na wadhifa huo, bado anaendelea kuwa mjumbe wa bodi na mjumbe wa kamati mbalimbali za kitaifa na za kimataifa za asasi na taasisi kadhaa zinazohusika na masuala ya vijana.
Ameandika na kuwasilisha tafiti na mada kadhaa kuhusu masuala mbalimbali zikiwemo za ukosefu wa ajira kwa vijana, ukuzaji wa vipaji vya vijana na mfumo mwafaka wa elimu Tanzania ambayo aliiwasilisha kwenye mkutano wa wabunge wa jamhuri ya muungano Tanzania.
Amefanya kazi pia kama mnukuzi wa warsha za kuwajengea uwezo wabunge wa jamhuri ya muungano wa Tanzania, nafasi ambayo imempa fursa ya kujifunza masuala mbalimbali ya Bunge ikiwemo uchambuzi wa bajeti, utendaji wa Bunge na usimamizi wa mahesabu.
Ameshiriki warsha mbalimbali za ndani ya nchi na mikutano katika nchi sita. Alichaguliwa kuwasilisha hotuba ya vijana katika mkutano wa fungamano la asasi za Umoja wa mataifa uliofanyika Hispania.
Lengo lake la muda mfupi ni kuchangia katika kuongeza ushiriki na ustawi wa vijana Tanzania na lengo lake la muda mrefu ni kuchangia katika kuleta maendeleo ya jamii kupitia kipawa chake cha uongozi.