`Mapokezi ya Chenge aibu`
2008-05-10 11:37:18
Na Pendo Fundisha,PST, Mbeya
Baadhi ya wakazi wa Mbeya na viongozi wa vyama mbalimbali vya siasa, wamelaani mapokezi ya Mbunge wa Bariadi Magharibi, Bw. Andrew Chenge (CCM) na wanachama wake kwa madai kuwa yanakidhalilisha chama hicho na kumdhalilisha Rais Jakaya Kikwete.
Walisema hakuna sababu za msingi za kuwafanyia mapokezi makubwa watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi, kwa kuwa kwa kufanya hivyo wanazorotesha juhudi za chama hicho na serikali katika vita yake dhidi ya ufisadi.
Mapokezi ya aina hiyo ni ya pili kufanyika baada ya aliyekuwa Waziri Mkuu Bw. Edward Lowassa kujiuzulu wadhifa wake baada ya kuhusishwa katika kashfa ya kampuni ya kufua umeme ya Richmond iliyodaiwa kupata zabuni kwa njia ya utata.
Baada ya kujiuzulu kwake Februari mwaka huu, Bw. Lowassa alifanyiwa mapokezi makubwa jimboni kwake Monduli, mkoani Arusha.
Bw. Chenge alijiuzulu wadhifa wa Waziri wa Miundombinu mapema mwezi uliopita, baada ya kufichuliwa kwa habari kwamba anamiliki zaidi ya Sh. Bilioni 1.2 ambazo zimehifadhiwa katika akaunti moja nje ya nchi. Fedha hizo zinadhaniwa kuwa zilipatikana kifisadi katika \'dili\' la ununuzi wa rada ghali ambayo kimsingi Tanzania ilikuwa haiihitaji.
Baada ya kujiuzulu Bw. Chenge wiki hii alikwenda jimboni kwake na kupokelewa na msafara mkubwa wa magari na wapiga kura wake wakiwemo makada wa vyama.
Wakizungumza juzi jioni walipokuwa wakiangalia taarifa za habari katika televisheni mbalimbali zilizokuwa zikionyesha mapokezi hayo yaliyohudhuriwa na baadhi ya makada wa CCM wakiwa katika makundi, walidai huo ni udhalilishaji wa chama hicho na viongozi wake.
Wakiongea na PST baadhi ya viongozi hao walidai kuwa imekuwa ni kejeli kwa serikali pale viongozi wa ngazi za juu waliokumbwa na tuhuma za ufisadi na kujiuzulu na kukimbilia katika majimbo yao kujisafisha.
``Kwa kweli wananchi, hususan wanachama wa CCM mnapaswa sasa kugeuka na kuangalia ni nini kinachofanywa na viongozi wa ngazi za juu, na si tu kujipanga katika barabara na ofisi za chama kwa ajili ya mapokezi ya watu wanaotuhumiwa kwa ufisadi.
Mnajidhalilisha kwa kunufaisha mafisadi na nyinyi wananchi wenye maisha duni mkizidi kupandishiwa gharama za maisha,`` alisema kiongozi mmoja.
Walisema wananchi walikuwa wakisubiri kauli ya serikali kupitia kwa Rais Kikwete dhidi ya hatua za makusudi zinazochukuliwa dhidi yao, lakini kila kukicha wanawasikia watuhumiwa wakikimbilia majimboni kwao na vyama vyao vikiwataka wananchi kujitokeza kwa wingi katika mapokezi na kwenye mikutano ya hadhara.
Naye mwananchama wa CUF, mkazi wa kitongoji cha Majengo, Bw. Augustino Amani, alisema serikali ilipaswa kufumbua macho na kuwaeleza wananchi hatma inayochukuliwa dhidi ya watu wanaotuhumiwa na ufisadi.
Alisema kwa sasa serikali inapaswa kuwa wazi kwa wananchi na si kuwanyonya kwa kuwapandishia gharama za maisha kutokana na gharama za bidhaa hususan, mafuta, mazao ya chakula kama mahindi na kumfanya mwananchi mwenye kipato cha chini kushindwa kumudu kupanda kwa gharama hizo.