Naomba msome hii ArticleDAWASCO wamkataa Mkurugenzi wao...
2008-03-22 09:41:24
Na Mashaka Mgeta
Wafanyakazi wa Kampuni ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASCO), wamemtaka Mkurugenzi Mtendaji Mkuu wao, Bw. Alex Kaaya, wanayedai kuwa `aliwekwa` madarakani na aliyekuwa Waziri Mkuu, Bw. Edward Lowassa, aachie ngazi kwa kushindwa kuendeleza kampuni.
Pia, wanadai kuwa Bw. Kaaya, aliyeshika wadhifa huo, wakati Bw. Lowassa akiwa Waziri wa Maji, amepandikiza chuki na mgawanyiko miongoni mwao.
Hali hiyo ilijitokeza jana jijini Dar es Salaam, wakati wa mkutano wa wafanyakazi hao, kupitia Chama cha Wafanyakazi wa Viwanda, Biashara, Taasisi za Fedha, Huduma na Ushauri (TUICO).
Wakati wafanyakazi hao wakitoa shutuma hizo, Bw. Kaaya na Katibu Mkuu wa TUICO, Bw. Bonifas Nkakatisi, walikuwepo.
Risala ya wafanyakazi hao, ilisomwa kwa niaba yao na Katibu Msaidizi wa TUICO wa matawi yaliyopo DAWASCO katika mikoa ya Dar es Salaam na Pwani, Bw. Geroge Lugendo.
Bw. Lugendo, alisema tangu aingie madarakani takribani miaka mitatu iliyopita, Bw. Kaaya, ameshindwa kutimiza ahadi za kuboresha mazingira ya kazi, huduma na maslahi ya wafanyakazi.
``Alituahidi kutupatia viwanja kwa kila mfanyakazi, kufanya mikutano kila baada ya miezi mitatu, kutuletea maisha bora ili tumudu kuwasomesha watoto wetu, hajatekeleza hayo yote,`` alisema.
Bw. Lugendo, alisema chini ya uongozi wa Bw. Kaaya, DAWASCO imeibua kundi la wafanyakazi wa zamani ambao wengi wao hawana elimu na wasomi walioajiriwa hivi karibuni.
Alidai kuwa, wafanyakazi wa zamani wanalipwa mishahara duni na kunyanyaswa, wakati wasomi wasiokuwa na ujuzi wanapata uongozi na mishahara mikubwa, hivyo kuwa `vinara` wa unyanyasaji.
Walidai kuwa, mmoja wa Mameneja hao, (wakamtaja jina), aliwahi kutishia kumuua mfanyakazi mwenzake kwa bastola.
Aidha, walimshutumu mkurugenzi wao kwa kuzuia kuunda mabaraza ya wafanyakazi na kutowashirikisha wafanyakazi katika maamuzi na mwenendo wa shughuli za DAWASCO.
``Tunamuomba Waziri wa Maji na Umwagiliaje aje amchukue Dk. Kaaya, sisi hatumtaki huku DAWASCO,`` alisema mmoja wa wafanyakazi aliyechangia risala hiyo.
``Kutokana na shutuma hizo, na uzito wa nafasi yake, apime mwenyewe na kuchukua hatua kama walivyofanya wanasiasa kule bungeni,`` alisema mfanyakazi wa DAWASCO, Bw. Abdallah Jongo.
Hata hivyo, Bw. Kaaya alijaribu kusimama ili ajitetee dhidi ya shutuma hizo, lakini wafanyakazi hao walipiga kelele wakisema ``ondoka, ondoka, ondoka.``
Bw. Kaaya aliendelea kuzungumza, lakini kelele za wafanyakazi hao na wengine zilipozidi akaamua kuacha.
Bw. Shaban Chezo, Bi. Happy Martine na Bw. Said Mfaume, walisema kwa nyakati tofauti kuwa, licha ya shutuma hizo, kuna michango ya SACCOS wanayokatwa wafanyakazi, lakini haifiki inapotakiwa.
Naye Bw. Staha Mrisho, alisema Bw. Kaaya, anaponzwa na utendaji wa mameneja wapya wanaoongoza kundi la wasomi katika kampuni hiyo.
Hata hivyo, Bw. Nkakatisi, aliwataka wafanyakazi hao kufuata sheria, kanuni na taratibu, ili kupata suluhu ya kero zinazowakabili.
Bw. Nkakatisi, aliyekabidhiwa risala ya wafanyakazi hao, alisema hatua yoyote itakayokuwa kinyume cha sheria, kanuni na taratibu zilizopo, itaashiria vurugu na hivyo kuwafanya wasifikie malengo yao.
Kuhusu Bw. Kaaya kuteuliwa na Bw. Lowassa, Katibu Mkuu huyo wa TUICO, alisema hatua hiyo ilitokana na mamlaka ya Uwaziri aliyokuwa nayo (Lowassa) na si vinginevyo.
SOURCE: Nipashe
imetoka kwa Nipashe 22/03/08