Msanii
Platinum Member
- Jul 4, 2007
- 25,252
- 36,532
WAZIRI Mkuu aliyejiuzulu kutokana na kashfa ya mradi wa umeme wa Richmond, Edward Lowassa, sasa anaelezwa kufanya mambo ambayo ni dhahiri yanamchimba Rais wake, Jakaya Mrisho Kikwete, kwa kushindwa kumtetea katika janga lililomkuta.
Habari za uhakika zinaeleza kwamba pamoja na mkakati maalumu aliouanzisha yeye na wafuasi wake kujisafisha, Lowassa kwa makusudi kabisa ametajwa kutamka waziwazi kwamba Kikwete hakumsaidia ama alihusika katika kuanguka kwake kisiasa. Kwa mujibu wa habari hizo ambazo tayari zimekwisha kumfikia Kikwete mwenyewe, katika moja ya vikao visivyo rasmi na watu walio karibu naye Lowassa ametamka waziwazi kuhusu kutoswa kwake na mtu anayeamini alichangia kwa kiasi kikubwa kumpandisha chati .
Katika matamko hayo ambayo anatajwa kuyatoa wiki iliyopita katika maeneo mbalimbali ikiwa ni pamoja na katika hoteli moja maarufu katikati ya Dar es Salaam, Lowassa anaapa kupambana kwa nguvu zake zote kuhakisha anarejea katika siasa kwa nguvu zote na hata ikibidi kwa kumshughulikia Kikwete. Vyanzo vya habari vinaeleza kwamba hata kampeni za dhahiri na mikakati ya siri ilizoanza kwa nguvu kubwa wiki hii ni sehemu ya mpango huo kamambe ambao unaelezwa kupewa jina la Agenda 21 ikiwa na malengo kadhaa ya kisiasa.
Kwa mujibu wa vyanzo hivyo, Agenda 21 ina mambo makuu matatu ikiwamo kumsafisha Lowassa na kundi lake kwa gharama zozote kazi ambayo tayari imeanza kwa utaratibu maalumu ikiwa ni pamoja na kutumia vyombo vya habari na mikutato ya hadhara kazi ambayo inafanywa kwa gharama kubwa na usimamizi makini.
Mpango mwingine unaelezwa ni kuhakikisha Kikwete anaanza kuchafuliwa kwa namna tofauti kazi ambayo itaanza wiki hii kwa kutumia kila aina ya mbinu kwa kuanzia na vyombo vya habari na propaganda za kisiasa na hatimaye kutumia Bunge kuwasilisha hoja ya kuundwa kwa Kamati Teule kuchunguza jambo litakalomgusa Rais ama Ikulu.
Wameandaa mkakati ambao hatimaye itaundwa Kamati ya Bunge ambayo itakayoundwa kwa nguvu ya kundi hilo (la Lowassa) ili lipewe Uenyekiti wa Kamati hiyo lakini wanajipanga jinsi ya kumuingia Spika wa Bunge, Samuel Sitta, ili waweze kupenyeza wajumbe wao ama wawanunue watakaoingizwa lakini hilo kwa sasa linawaumiza vichwa kutokana na msimamo na historia ya Spika dhidi ya Lowassa na wafuasi wake, kinaeleza chanzo cha habari ndani ya serikali.
Sehemu ya tatu ambayo nayo inaelezwa kwenda sambamba na ile ya kujisafisha, kundi la Lowassa limepanga kama si kuanza kuwachimba na kuwafuatilia kwa karibu wale wote inaoamini kwamba wamehusika kwa namna moja au nyingine katika kile kilichotokea bungeni wakiwamo wabunge, waandishi wa habari na watu wengine katika jamii.
Wataanza kwa kujaribu kuwavuta upande wao kwa kutumia mbinu na hata fedha wale wanaoamini kwamba walishiriki kwa namna moja au nyingine katika kuanguka kwa Lowassa na wakishindwa ndipo sasa watabadili mbinu na kuwashughulikia kwa mbinu chafu ili kulipiza kisasi na pia kupunguza nguvu ya adui, anaeleza mtoa habari huyo. Inaelezwa kwa uwazi kabisa kwamba hatua zote zinazochukuliwa sasa na Lowassa na wafuasi wake zinalenga kurudisha hadhi yake kwa haraka sana ili kuweza kujiandaa kuchukua madaraka ya juu kabisa ya nchi baada ya Kikwete na ikibidi utekelezaji wake uwe hata kabla ya mwaka 2015 ambao ndio Kikwete atakua anamaliza miaka kumi.
Wanajipanga na wanaweka bayana kwamba kama Kikwete hatamuunga mkono Lowassa basi wataingia katika uchaguzi hata mwaka 2010 kwa namna yoyote ile hata ikibidi kupitia chama kingine badala ya CCM, lakini uamuzi huo ni hatua ya mwisho ikiwa wataona wanakwamishwa katika malengo yao ya baadaye, anasema mtoa habari huyo ambayo yuko karibu na wanasiasa wote wawili (Kikwete na Lowassa).
Tayari Lowassa amekwishatamka hadharani kupitia Televisheni ya Taifa (TVT) na katika mkutano wa hadhara jimboni kwake Monduli kwamba ameonewa huku akifuatiwa na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi na hatiaye Mkurugenzi wa Kituo cha Uwekezaji (TIC), Emanuel Ole Naiko, ambaye ametoa kali kwa kusema kwamba watu wanaotoka Monduli akiwamo yeye wanaonewa.
Karamagi na Ole Naiko walipata nafasi ya kuhojiwa na Kamati Teule ya Bunge iliyochunguza sakata la umeme wa dharura wa Richmond na wote wawili wameonyesha kutoridhishwa na ripoti ya Kamati hiyo iliyoongozwa na Mbunge wa Kyela, kupitia CCM, Dk. Harison Mwakyembe. Kwa upande wake, aliyekua Waziri wa Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Dk. Ibrahim Msabaha, yeye hajatoa kauli yoyote hadharani baada ya ile aliyoitoa bungeni kujitetea na hatimaye kujiuzulu baada ya kutajwa kwake kuhusika akiwa Waziri wa Nishati na Madini wakati mradi wa Richmond ukiingizwa nchini.
Wakati yote yakiendelea, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda ameweka bayana kwamba atatekeleza kwa nguvu zote mapendekezo ya Kamati ya Mwakyembe, na kwamba hatoogopa wala kumuonea haya mtu yeyote, kauli ambayo inaonekana kuwa mwiba kwa wanaothubutu kujitetea ama kujisafisha mbele ya jamii.
Hii Inaonesha ni jinsi gani UROHO wa madaraka unaweza kumtia mtu upofu mpaka akawa haoni hata zile rangi za msingi.
Ifuatilieni hii news kama source inavyoonesha.
Ila kwa taarifa tu, ni kuwa shughuli imeanza na hakuna kulala mpaka wapate wanachokitaka...