LHRC: Waliotishiwa maisha watoe taarifa polisi

BARD AI

JF-Expert Member
Jul 24, 2018
3,376
8,118
1689052497365.png

Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), kimekemea vikali matukio ya kutishiwa maisha kwa baadhi ya Watanzania wanaoonekana kuwa na mlengo au maoni tofauti.

Sambamba na hilo, LHRC imekemea vitendo vya baadhi ya viongozi wa Serikali hususani mawaziri kutoa maonyo ambavyo yanaashiria kuwatishia Watanzania wanaotekeleza uhuru wao wa kutoa maoni kupitia majukwaa mbalimbali ikiwemo mitandao ya kijamli.

Katika taarifa ya kituo hicho iliyotolewa leo Jumatatu Julai 10, 2023 imeeleza kuna malalamiko ya watu wanaotishiwa maisha yao na watu wasiojulikana kwa sababu maoni yao yanakinzana na yale ya upande mwingine hasa kwenye mijadala inayohusu maslahi mapana ya Taifa.

Taarifa hiyo ambayo imesainiwa na Mkurugenzi MKuu wa LHRC, Anna Henga imeeleza kwa takribani juma moja sasa imepita ambapo kumekuwa na mjadala wa baadhi ya Watanzania kulalamika kutishiwa maisha yao na watu waliodai wasiojulikana kutokana na misimamo yao kwenye mambo mbalimbali yanayogusa masiahi ya umma.

“Uhuru wa kujieleza unalindwa na kuhifadhiwa kwa mujibu Ibara ya 19 ya Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa wa Mwaka 1966, Ibara ya 9 ya Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu wa mwaka 1989, ambapo Tanzania ni nchi mwanachama wa mikataba hii mtawalia.

“Wakati huo huo uhuru wa kujieleza unalindwa na kuhifadhiwa na Ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 kama ilivyofanyiwa marekebisho mara kadhaa,” imeeleza taarifa hiyo.

Kufuatia hilo, LHRC imewataka watu wote waliopokea vitisho kutoa taarifa kwa Polisi ili hatua zichukuliwe ikiwa pamoja na upelelezi ili wahusika wajulikane na wafikishwe mbele ya sheria.

Pia, imeitaka Serikali kulinda, kuhifadhi na kuheshimu uhuru wa Watanzania kutoa maoni yao kwa mujibu wa sheria sambamba na uhuru wa kukusanyika.

“Serikali iruhusu mawazo mbadala kwa maslahi ya Taifa na Watanzania watumie uhuru wao wa kujieleza kwa kuzingatia ibara ya 18 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, 1977 pamoja na sheria za nchi bila kutweza utu wa mtu mwingine kwa vigezo vya jinsia, jinsi, udini, ukabila, hadhi, ulemavu au rangi ya mtu,” imeeleza taarifa hiyo.

MWANANCHI
 
Back
Top Bottom