Kakke
JF-Expert Member
- Dec 4, 2010
- 1,883
- 1,482
Mbunge wa Kahama (CCM),James Lembeli
Na Ashton Balaigwa
1st April 2014
Mbunge wa Kahama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM),James Lembeli
Mjumbe wa Bunge Maalum la Katiba ambaye pia ni Mbunge wa Kahama kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), James Lembeli, amesema msimamo wake kwenye mchakato wa kutunga Katiba mpya ni kuona Muungano wa Tanzania unakuwa wa muundo wa serikali tatu.
Lembeli alitoa msimo huo jana wakati akizungumza na waandishi wa habari nje ya ukumbi wa Bunge mjini Dodoma baada shughuli za Bunge kuahirishwa.
Alisema licha ya chama chake kuwa na msimamo wa kuwa na muundo wa serikali mbili, yeye binafsi hayuko tayari kwa hilo na kwamba atapambana ndani ya Bunge hilo kutaka muundo wa serikali tatu upitishwe.
Alisema miongoni mwa kazi atakazozifanya ili kufanikisha lengo hilo ni pamoja na kuwashawishi wabunge wenzake wakubali muundo wa serikali tatu kwa lengo la kumaliza kabisa kero za Muungano ambazo alisema nyingi zimesababishwa na muundo wa serikali mbili.
Lembeli alisema kuwa hata Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alikwisha kusema kupitia hotuba zake kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko na wasipoyapata ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM.
Tukifuata hata maelekezo ya Baba wa Taifa, Mwalimu Nyerere, alituasa kuwa Watanzania wanahitaji mabadiliko na akasema wazi kuwa wasipoyapata mabadiliko ndani ya CCM watayatafuta nje ya CCM, sasa mimi naona hii ilikuwa ni fursa kwa chama changu kuwapatia Watanzania mabadiliko, lakini bado msimamo wake siyo wa mabadiliko ndiyo sababu mimi nimeona nianze kuonyesha njia ya kuelekea kwenye mabadiliko, alisema Lembeli.
Alisema hayuko tayari kuunga mkono na kupitisha Rasimu ya Katiba yenye muundo wa serikali mbili kama chama chake kinavyotaka kwa sababu hayo siyo mabadiliko, hivyo atahakikisha anashawishi wajumbe wenzake wafanye mabadiliko kwa kuingia kwenye muundo wa serikali tatu.
Alisema hata Rais Jakaya Kikwete katika hotuba ya uzinduzi wa Bunge hilo Machi 21, mwaka huu alisema kuwa wajumbe wasikubali kufuata mawazo ya kuambiwa pekee, bali watumie pia na akili zao, hivyo yeye pamoja na misimamo ya kuambiwa na chama chake pia atakuwa na msimamo wa serikali tatu ambao ni akili zake mwenyewe.
Katika hotuba yake Rais Kikwete alisema kuwa akili za kuambiwa changanya na zako upate majibu, sasa chama changu kimeniambia kuwa msimamo ni serikali mbili, nimechanganya na akili zangu na nimeona msimamo wangu ni serikali tatu, alisema Lembeli.
Lembeli ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Kudumu ya Bunge la Jamhuri ya Muungano ya Ardhi, Maliasili na Mazingira, alisema Muungano wa sasa una changamoto nyingi na malalamiko kutoka pande zote, hivyo ili kuondoa malalamiko na changamoto hizo ni lazima ziwepo serikali tatu za Tanganyika, Zanzibar na ya Muungano.
Mimi ni mmoja wa waumini wa kudai serikali ya Tanganyika, hilo naliweka wazi na wala siogopi, nataka Watanzania wajue kuwa tunachopigania ni Muungano wa usawa kwa pande zote za Muungano, kama ipo Serikali ya Mapinduzi Zanzibar, sioni sababu ya kuikataa Serikali ya Tanganyika, alisema Lembeli.
Rasimu ya Katiba iliyopendekezwa na iliyokuwa Tume ya Mabadiliko ya Katiba na kuwasilishwa kwenye Bunge Maalum la Katiba na Mwenyekiti wake, Jaji Joseph Warioba, Machi 18, mwaka huu inapendekeza kuwapo kwa muundo wa serikali tatu ambazo zitaondoa kero za Muungano.
Hata hivyo, Rais Kikwete katika hotuba yake ya kulizindua Bunge hilo, aliweka msimamo wake wazi kwamba muundo wa serikali tatu hauwezi kutekelezeka kwa kuwa serikali ya Muungano haitakuwa na mapato ya kuiendesha, hali inayoweza kusababisha Jeshi kuiangusha serikali.
Suala la muundo wa Muungano limeibua mjadala nchini pamoja na kusababisha mgawanyiko miongoni mwa Wajumbe wa Bunge la Katiba.
Wajumbe kutoka CCM wanatetea serikali mbili wakati wa kutoka upinzani na baadhi ya wawakilishi wa makundi na taasisi wanataka serikali tatu.
Ni kutokana na mgawanyiko huo Bunge hilo lililazimika kuziweka kiporo kanuni za 37 na 38 ambazo zinahusu utaratibu wa kura za kupitisha vifungu vya rasimu kama uwe wa kura ya siri au ya wazi.
Wajumbe wa CCM walitaka itumike kura ya wazi, msimamo ulioonyesha kwamba lengo lake lilikuwa ni la kuepusha wajumbe wake wasikisaliti chama hicho wakati wa kupigia kura muundo wa Muungano huku wajumbe wa upinzani na baaadhi kutoka makundi, asasi wakitaka kura ya siri.
Hata hivyo, kanuni hizo zilipitishwa Ijumaa iliyopita baada ya Kamati ya Mashauriano kuamua zitumike kura zote, za wazi na siri na Bunge liliridhia.
CHANZO: NIPASHE