Kyela Ibasa Festival yatoa msaada wa mafuta na miwani kwa wenye Ualbino

Roving Journalist

JF Roving Journalist
Apr 18, 2017
2,812
11,987
Umoja wa Wazawa wa Wilaya ya Kyela Mkoani Mbeya, waishio ndani na nje ya wilaya hiyo Kyela Ibasa Festival, wametoa msaada wa mafuta ya kupakaa na miwani kwa ajili ya watu wenye Ualbino.

Msaada huo umekabidhiwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Jamii, Vanessa Nyesyenge kwa niaba ya wanaibasa ambao kwa umoja wao walichangishana fedha kwa ajili ya kuisaidia jamii ya wilaya yao ikiwa ni utaratibu waliojiwekea kila inapofika mwisho wa mwaka kusaidia sekta ya afya, elimu, kuenzi utamaduni kwa kuandaa ngoma za asili na kutembelea vivutio vya utalii ikiwemo fukwe ya Matema Beach.

Watu 35 wenye Ualbino wamepatiwa mafuta maalum kwa ajili ya kuwasaidia kuwakinga na ngozi pamoja na miwani kwa wale wenye matatizo ya macho ambao wanapimwa na kupatiwa.
1f6e955d-8470-4487-8205-98d4a8dfdb70.jpeg

4da7df8f-6bfd-4d7c-9db5-91627e3c8765.jpeg
Akipokea msaada huo, Mwenyekiti wa Chama cha Watu wenye Ualbino Wilaya ya Kyela, Bwigane Mwamasangula, amesema walikuwa wanakabiliwa na tatizo kubwa la ngozi kwa sababu ya kukosa mafuta hasa kipindi hiki cha jua kwa sababu ya kukosa fedha ya kununua bidhaa hiyo.

Amesema yatawasaidia kulinda na kutunza ngozi zao pamoja na miwani waliyopewa, pia ameuomba umoja huo kuendelea kuwasaidia kwa sababu hawana fedha za kudumu gharama za mafuta hayo ambayo alidai yanauzwa kwa bei ghali.

“Tunawashukuru sana Ibasa kwa msaada huu hakika mnarudisha fadhila nyumbani, kutokana na hali zetu duni tumeshindwa kabisa kumudu gharama za ununuzi wa mafuta ya kulinda ngozi zetu wilaya yetu ni ya joto na jua kali kwa hali zetu tunajikuta tunapata mateso sambamba na miwani asilimia kubwa sisi macho yetu yanashida hivyo miwani mliotupatia itatusaidia sana, tunaomba muendelee kutukumbuka,” amesema Mwamasangula.

Katika hatu nyingine Kyela Ibasa imetoa msaada wa vifaa tiba, vitendanishi na mashuka 20 kwa ajili ya Zahanati ya Njisi kwa ajili ya kusaidia upatikanaji bora wa huduma za matatibu.

Mganga Mfawidhi wa Zahanati ya Njisi, Johson Mganyizi amesema msaada huo utasaidia kuondoa tatizo ya uhaba wa vifaa tiba ambavyo licha ya serikali kuvinunua lakini mahitaji yamekuwa makubwa kutokana na kituo hicho kuhudumia idadi kubwa ya wananchi.

Kiasi cha Sh. Milioni 4.9 kimetolewa na Kyela Ibasa kwa ajili ya kusaidia jamii katika sekta ya afya ambapo walitoa mashuka, vifaa tiba, vitendanishi, mafuta na miwani kwa ajili ya watu wenye ualbino pamoja na sekta ya elimu kwa kununua vitabu ya masomo mbalimbali kusaidia watoto wanasoma Shule ya Sekondari Njisi.
 
Back
Top Bottom