Rejea ya andiko lifuatalo
KANISA LIPO KWA AJILI YA KITETEA HAKI NA MASLAHI WATU WOTE KATIKA JAMII!
Wapendwa Watanzania!
Kuna watu wanalalamika kuwa sisi maaskofu tunamuandama Rais Samia kwa kuwa yeye ni Muislamu. Wanalalamikia matamko ya kupinga Mkataba wa Bandari wakidai kuwa tumefanya hivyo kwa kuwa Rais Rais Samia ni Muislamu. Wanasema hatukumpinga Rais Magufuli kwa kuwa yeye alikuwa ni Mkristo. Huo ni uwongo ambao usingestahili kujibiwa na Askofu. Lakini kwa kuwa kuna baadhi ya watu hawakufuatilia au wamesahau, basi tumeona tuwakumbushe.
Hakuna taasisi ambayo iliuandama utawala wa Magufuli kama Kanisa. Ushahidi wa haya ni:
1. Mwaka 2018 Kanisa Katoliki lilitoa Waraka wa Pasaka ambao ulimchukiza sana Magufuli
2. Mwaka 2018: Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) pia lilitoa Waraka wa Pasaka uliomchukiza sana Rais Magufuli.
3. Askofu Severine Niwemugizi wa Kanisa Katoliki Dayosisi ya Rulenge-Ngara aliandamwa sana kwa sababu aliionya serikali ya Magufuli.
4. Rev. Fr. Sabah (RIP) wa Kanisa Katoliki naye aliandamwa sana na utawala wa Magufuli.
5. Askofu Zakaria Kakobe wa Full Gospel Bible Fellowship aliandamwa sana na utawala wa Magufuli baada ya yeye kuukaripia.
6. Askofu Emmaus Mwamakula wa Kanisa la Moravian la Uamsho Tanzania aliandamwa sana na hata kuwekwa kizuizini baada kupinga udikiteta wa utawala wa Magufuli.
7. Askofu Dkt. Stephen Munga wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Kaskazini Mashariki aliandamwa sana kiasi cha kufikia hatua kukimbilia Afrika Kusini kwa matibabu yaliyookoa uhai wake.
8. Askofu Josephat Gwajima alipata utulivu baada ya kukubali kuhamia CCM lakini kabla ya hapo ilikuwa ni tabu.
Kwa hiyo, sisi maaskofu tumejenga utamaduni wa kuonya mamlaka kila zinapotenda mambo ambayo tunadhani hayana manufaa kwa jamii. Tunafanya hivyo kwa njia mbalimbali ikiwemo maonyo ya faragha, nyaraka, kutuma ujumbe maalum (delegation), nk.
Sisi tunaamini kuwa Mkataba wa Bandari umeingiwa na serikali ya Tanzania na wala sio na watu wa kabila au dini fulani. Kwa hiyo, sisi tumemtaka Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ili Serikali isikilize maoni na kelele za wananchi wake tukiwemo sisi, wala hatujatoa shinikizo kwa Rais wa Kabila au Rais wa Dini.
Kama kuna makundi mengine yana hoja juu ya Mkataba wa Bandari hayajazuiwa kuwasilisha hoja zao. Katika kupinga mkataba sisi tulijikita katika kuchambua yaliyomo katika mkataba ambavyo. Tunatarajia kuwa makundi mengine nayo yatafanya hivyo badala ya kuangalia sura, nasaba, koo, kabila au dini.